• HABARI MPYA

  Jumamosi, Oktoba 22, 2016

  YANGA NA KAGERA SUGAR NDANI YA KAITABA YA NYASI BANDIA LEO

  Na Mwandisji Wetu, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi, Yanga SC leo watashuka kwenye Uwanja wa wa nyasi bandia wa Kaitaba, Bukoba kumenyana na Kagera Sugar katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Yanga ambayo Jumatano ilipata ushindi wa 2-0 dhidi ya Toto Africans Uwanja CCM Kirumba, Mwanza itahitaji kuendeleza wimbi la ushindi ili kupunguza idadi ya pointi wanazozidiwa na mahasimu, Simba.
  Kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm alisema jana katika mazungumzo na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE kutoka Bukoba kwamba wamefika salama na wanaendelea vizuri na maandalizi yao kuelekea mchezo wa leo.
  “Hapa ninavyozungumza na wewe nipo kwenye mazoezi Uwanja wa Kaitaba kwa maandalizi ya mwisho wa mchezo wetu,”alisema Pluijm.
  Na kocha huyo wa zamani wa Berekum Chelsea ya Ghana akasema kwamba, mshambuliaji wake Mrundi, Amissi Tambwe aliyekosekana katika mechi mbili zilizopita anaweza kurejea leo. “Tambwe yuko fiti kabisa sasa, na anaweza kucheza kesho (leo),”alisema Pluijm.
  Tambwe aliumia katika mchezo na Mtibwa Sugar Oktoba 12 Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam Yanga ikishinda 3-1 na tangu hapo amekosa mechi mbili, dhidi ya Azam FC Oktoba 16 na Toto Oktoba 19.
  Kwa ujumla, Ligi Kuu raundi ya 12 inaendelea leo kwa michezo sita ukiwemo huo wa mabingwa watetezi Yanga kwenye Uwanja wa Kaitaba ulioko Bukoba mkoani Kagera.
  Mjini Dar es Salaam, katika Uwanja wa Uhuru African Lyon itakuwa mwenyeji wa Mbeya City ya Mbeya ilihali Mwadui ya Shinyanga itasafiri hadi Mtwara kucheza na Ndanda Fc kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona wakati Stand United itakuwa mgeni wa Mtibwa Sugar ya Morogoro kwenye mchezo utaofanyika Uwanja wa Manungu, ulioko Turiani – Mvomero.
  Majimaji itakuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting ya Pwani kwenye Uwanja wa Majimaji huko Songea. Michezo yote mitano hapo juu itaanza saa 10.00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki lakini mchezo kati ya Azam FC na JKT Ruvu itaanza saa 1.00 usiku kwenye Uwanja wa Azam huko Chamazi-Mbagala Dar es Salaam.
  Jumapili itakuwa ni zamu ya kinara wa ligi hiyo, Simba ambayo itaikaribisha Toto Africans ya Mwanza kwenye Uwanja wa Uhuru wakati Tanzania Prisons itapambana na Mbao FC kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
  Michezo yote ya Dar es Salaam, mfumo wa kuingia utabaki kuwa ni uleule wa kutumia kadi za Selcom kununua tiketi za kielekroniki. Viingilio kwenye mechi za Uwanja wa Uhuru ni Sh 30,000 kwa Jukwaa Kuu (VIP-A), VIP-B na C Sh 20,000 na mzunguko ni Sh 5,000 wakati Kiingilio Uwanja wa Azam ni Sh 10,000 kwa VIP na Mzunguko ni Sh 3,000.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA NA KAGERA SUGAR NDANI YA KAITABA YA NYASI BANDIA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top