• HABARI MPYA

  Jumapili, Oktoba 23, 2016

  SIMBA YA MWAKA HUU ISIKIE TU, TOTO LA YANGA LIMEKUFA 3-0

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SAFARI ya ubingwa imeshika kasi Simba SC. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya Wekundu wa Msimbazi kuendeleza wimbi la ushindi leo katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Simba SC imeibugiza 3-0 Toto Africans hivyo kufikisha pointi 29 baada ya kucheza mechi 11 na sasa wanawazidi mabingwa watetezi, Yanga walioa nafasi ya pili kwa pointi nane. 
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na Erick Onoka wa Arusha aliyesaidiwa na Khalfan Sika wa Tanga na Mohammed Mkono wa Tanga, hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa 1-0.
  Bao hilo lilifungwa na kiungo Muzamil Yassin aliyeunganisha vizuri krosi pasi ya mshambuliaji Frederick Blagnon kutoka Ivory Coast dakika ya 42.
  Muzamil alifunga bao hilo akitoka kukosa bao la wazi dakika ya 35 baada ya kuunganishia nje kona iliyopgwa na beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
  Kiungo Muzamil Yassin akikimbia kushangilia baada ya kuifungia Simba SC mabao mawili, moja kila kipindi katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Toto Africans ya Mwanza kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Bao lingine la Simba SC lilifungwa na Mrundi, Laudit Mavugo kipindi cha pili.
  Mpishi wa bao la kwanza la Simba SC, Frederick Blagnon (kulia) akimtoka beki wa Toto Yussuf Mgeta (kushoto)
  Beki wa Simba, Mohammed Hussein 'Tshabalala' akipiga kichwa mbele ya mchezaji wa Toto, Soud Mohammed
  Kiungo wa Simba SC, Muzamil Yassin akimtoka beki wa Toto, Salum Chuku 
  Winga wa Simba, Shizza Kichuya akimtoka Salum Chuku wa Toto

  Mapema dakika ya 18 Salum Chuku wa Toto aliunganishia juu ya lango la Simba krosi ya Jamal Soud kabla ya Shizza Kichuya naye kupiga pembeni ya lango dakika ya 25 kufuatia pasi ya kiungo Mwinyi Kazimoto.
  Kipindi cha pili, Simba SC ilianza na mabadiliko baada ya Blagnon kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Mrundi Laudit Mavugo dakika ya 48.
  Dakika tatu tu baada ya kuingia, Mavugo akaifungia Simba SC bao la pili dakika ya 51 akimalizia pasi safi ya Muzamil Yassin.
  Kiungo Muzamil Yassin akawainua tena vitini mashabiki wa Simba baada ya kufunga bao la tatu dakika ya 74 akimalizia kona ya winga Kichuya mchezaji mwenzake wa zamani wa Mtibwa Sugar.
  Mnyate aliunganishia nje ya lango krosi ya kiungo mwenzake waliyetokea naye benchi kipindi cha pili, Said Ndemla dakika ya 83.
  Jaffar Mohammed akaikosesha Toto bao la kufutia machozi dakika ya 87 baada ya kumdakisha kwa shuti dhaifu kipa Vincent Angban.
  Kikosi cha kilikuwa; Vincent Angban, Janvier Bukungu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Method Mwanjali, Juuko Murshid, Jonas Mkude, Muzamil Yassin, Mwinyi Kazimoto/Jamal Mnyate dk58, Frederic Blagnon, Mohamed ‘Mo’ Ibrahim, Shizza Kichuya/Said Ndemla dk69.  
  Toto Africans; Mussa Kirungi, Salum Chuku, Yussug Mgeta, Carlos Protas/Ramadhani Malima dk60, Yussuf Mlipili, Hamim Abdallah, Jamal Soud, Reliant Lusajo, Waziri Junior, Jaffar Mohamed na Soud Mohammed/Frank Sekule dk40.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA YA MWAKA HUU ISIKIE TU, TOTO LA YANGA LIMEKUFA 3-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top