• HABARI MPYA

  Jumapili, Oktoba 30, 2016

  YANGA KIBOKO, MBAO WAMEKUFA 3-0 KAMA WAMESIMAMA

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mhoalanzi wa Mholanzi Franciscus Johannes ‘Hans’ van der Pluijm amerejea na mguu mzuri baada ya leo kuiwezesha timu hiyo kuendeleza ubabe katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa ushindi wa 3-0 dhidi ya Mbao FC ya Mwanza Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.  
  Kwa ushindo huo uliotokana na mabao ya beki Mtogo, Vincent Bossou, viungo Mkongo Mbuyu Twite na mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe, Yanga inafikisha pointi 27 baada ya mechi 12 ikiendelea kushika nafasi ya pili, nyuma ya Simba SC yenye pointi 32 za mechi 12 pia. 
  Ijumaa Yanga ilimuandikia barua ya kumuomba kurudi kazini kocha Pluijm, aliyejiuzulu mapema wiki hii baada ya kukerwa na uongozi wa klabu kuleta kocha mpya, Mzambia George Lwandamina bila kumtaarifu, akisema huko ni kumvunjia heshima.
  Wachezaji wa Yanga wakifurahia ushindi wao mnono wa leo
  Mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa akimiliki mpira mbele ya beki wa Mbao
  Winga wa Yanga, Simon Msuva akiwania mpira dhidi ya beki wa Mbao
  Mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe akipiga mpira pembeni ya beki wa Mbao
  Kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima (kulia) akimtoka beki wa Mbao 
  Beki wa Yanga, MwinyinHajji (kulia) akimtoka beki wa Mbao FC, Steve Mganya 

  Kocha huyo akakataa hadi nafasi ya Ukurugenzi wa Ufundi amabyo inasemekana Yanga ilitaka kumpa baada ya kumleta Lwandamina kuwa kocha Mkuu.
  Lakini baada ya kuwaaga wachezaji siku moja kabla ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya JKR Ruvu timu ikishinda 4-0 Jumatano, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba aliingilia kati suala hilo na kuwasuluhisha hadi wakaamua kurejeana.
  Uongozi wa Yanga ulitaka kumuondoa Pluijm na Wasaidizi wake wote, Juma Mwambusi, kocha wa makipa Juma Pondamali na Meneja Hafidh Saleh wote wazalendo na kuwaleta Mzambia Lwandamina atakayekuwa Kocha Mkuu, akisaidiwa na wazalendo Charles Boniface Mkwasa, Manyika Peter kocha wa makipa na Meneja, Sekilojo Chambua.  
  Huo unakuwa ushindi wa 78 katika mechi 125 kwa Pluijm tangu aanze kuinoa Yanga mwaka 2014 aliporithi mikoba ya Mholanzi mwenzake, Ernie Brandts akiwa ametoa sare 25 na kufungwa mara 22.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na Ludovick Charles wa Tabora aliyesaidiwa na Makame Mdogo wa Shinyanga na Agnes Pantaleo wa Arusha, hadi mapumziko hakukuwa na bao.
  Lakini ni Yanga waliotawala mchezo na kupoteza nafasi nyingi kuanzia dakika ya saba winga Simon Msuva alipounganishia nje krosi ya Deus Kaseke na dakika ya 41 Mrundi Amissi Tambwe alipopiga nje baada ya pasi ya Msuva.
  Beki Mtogo Vincent Bossou akaifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 49 kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na kiungo kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima.
  Kipa wa Mbao, Emmanuel Mseja aliudondoshea mpira nyavuni mwake dakika ya 55 katika harakati za kuokoa mpira uliorushwa na beki Mkongo Mbuyu Twite.
  Kinara wa mabao wa Yanga, Amissi Joselyn Tambwe akaifungia timu yajke bao la tatu dakika ya 75 akimalizia pasi safi ya Haruna Niyonzima.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deogratius Munishi 'Dida', Hassan Kessy/Thabani Kamusoko dk64, Mwinyi Hajji Mngwali, Andrew Vincent, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amisi Tambwe, Obrey Chirwa/Donald Ngoma dk71 na Deus Kaseke/Juma Mahadhi dk57.
  Mbao FC; Emmanuel Mseja, Steve Mganya, Steve Kigocha, Asante Kwesi, David Majinge, Youssouf Ndikumana, Dickson Ambundo, Salmin Hoza/ Emmanuel Mvuyekure dk61, Venance Ludovic/Frank Damas dk52, Hussein Swedy/ Boniface Maganga dk42 na Pius Buswita. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA KIBOKO, MBAO WAMEKUFA 3-0 KAMA WAMESIMAMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top