• HABARI MPYA

  Jumamosi, Oktoba 22, 2016

  SIMBA SC: UBINGWA UPO TUNAKOPITA SISI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imetamba kwamba ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara upo kwenye njia yao baada ya kufanikiwa kuvuna pointi nne kwa wapinzani wakuu, Azam na Yanga.
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Hajji Sunday Manara alisema jana katika mazungumzo na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE kwamba sasa timu yao imekaa vizuri katika mbio za ubingwa dhidi ya Azam na Yanga.
  “Kama unataka ubingwa, lazima uwashinde wapinzani wako wakuu na kushinda mechi nyingine zote. Sisi tumefanikiwa kuvuna pointi nne kwa wapinzani wetu, baada ya kutoa sare na Yanga na kuwafunga Azam, sasa maana yake ubingwa upo kwenye njia yetu zaidi,”alisema.
  Aidha, Manara alisema kwamba Simba SC inaendelea vizuri na maandalizi yake ya mchezo wake wa kesho wa Ligi Kuu dhidi ya Toto Africans ya Mwanza.
  Simba SC watawakaribisha Toto kesho Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam katika mfululizo wakitoka kushinda 1-0 dhidi ya timu nyingine ya Mwanza, Mbao FC Alhamisi.
  Ushindi wa juzi ulikuwa wa mbinde, kwani timu ya kocha Joseph Marius Omog ililazimika kusubiri hadi dakika ya 87 wakati kiungo Muzamil Yassin aliyesajiliwa msimu huu kutoka Mtibwa Sugar alipofunga akimalizia krosi ya mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Frederick Blagnon.
  Simba SC ndiyo inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 26 baada ya kucheza 10 ikishinda nane na kutoa sare mbili – hivyo kuendelea kuwazidi kwa pointi sita Stand United walio nafasi ya pili, wakati mabingwa watetezi, Yanga wana pointi 18 za mechi tisa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC: UBINGWA UPO TUNAKOPITA SISI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top