• HABARI MPYA

    Monday, October 31, 2016

    POLISI YAZUNGUMZIA KIFO CHA MASHALI, FAMILIA YATAJA TAREHE YA MAZISHI

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    JESHI la Polisi Kanda Maalum, Kinondoni, Dar es Salaam limethibitisha bondia Thomas Fabian Mashali maarufu ‘Simba Asiyefungika’ kufariki dunia usiku wa kuamkia leo baada ya ugomvi uliotokea eneo la Kimara Bonyokwa.
    Kamanda wa Polisi wa Kanda maalum ya Kinondoni, Dar es Salaam, Susan Kaganda amesema leo kwamba taarifa za uchunguzi wa awali zinaonyesha Mashali amefariki kwenye ugomvi uliotokea Kimara Bonyokwa dhidi ya watu wasiojulikana.
    Baba wa bondia huyo, Christopher Mashali amesema mazishi yatafanyika Jumatano kwenye Makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam kuanzia saa 7.00 mchana na kwamba marehemu ameacha watoto watano.
    Thomas Mashali amefariki dunia usiku wa kuamkia leo baada ya ugomvi uliotokea eneo la Kimara Bonyokwa

    Hadi anakutwa na umauti, Mashali alikuwa amepigana jumla ya mapambano 26 ya ngumi za kulipwa akishinda 19, kushindwa matano, sare moja na moja lilifutwa ulingoni.
    Enzi za uhai wake, Mashali alikuwa mkali kweli ulingoni akishinda mataji tofauti kuanzia la Afrika Mashariki na KatiOktoba 14, mwaka 2012 kwa kumpiga Med Sebyala wa Uganda kwa pointi ukumbi wa Friends Corner, Dar es Salaam.
    Akalitetea taji hilo kwa kumpiga Mkenya Bernard Mackoliech Januari 12, mwaka 2013, ukumbi wa Friends Corner, hivyo kupata nafasi ya kwenda kuwania taji la IBF Afrika, ambalo hata hivyo alilikosa kwa kupigwa na Mtanzania mwenzake, Francis Cheka Mei 1, mwaka 2013 kwa Knockout (KO) raundi ya saba ukumbi wa PTA, Dar es Salaam.
    Mashali akashindwa pia kutwaa taji la Mabara la UB Novemba 16, mwaka 2013 baada ya kupigwa na Mrusi Arif Magomedov ukumbi wa Ivanhoe Country Club, mjini Podolsk, Urusi kwa KO raundi ya saba.
    Akasahihisha makosa yake na kufanikiwa kutwaa taji la UBO Afrika kwa kumpiga kwa pointi Mtanzania mwenzake, Japhet Kaseba Machi 29, mwaka 2014 ukumbi wa PTA, Dar es Salaam.
    Akatetea taji hilo kwa kumpiga Alibaba Ramadhani Oktoba 5, mwaka 2014 kwa KO raundi ya tisa pambano la raundi 12 Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, kabla ya kwenda kupigwa na Mrusi Apti Ustarkhanov kwa KO raundi ya pili ukumbi wa Colosseum Sport Hall, mjini Grozny, Urusi Machi 5, 2016.
    Mashali akarudisha heshima Mei 14 mwaka huu kwa kumpiga Sajjad Mehrabi wa Iran kwa pointi Uwanja wa Ndani wa Taifa, Dar es Salaam na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa dunia wa UBO uzito wa Super Middle.
    Julai 9, mwaka huu alishindwa kutwaa taji la WBO Oriental uzito huo huo wa Super Middle baada ya kupigwa na Mchina Zulpikar Maimaitiali kwa KO raundi ya sita ukumbi wa Multi-Functional Hall, Water Cube mjini Beijing, China.
    Akaweka kumbumbu ya kushinda pambano la mwisho kabla ya kifo chake, kwa kumpiga Shaaban Kaoneka kwa pointi ukumbi wa Chee Kwa Chee Pub, Bagamoyo mkowani Pwani Septemba 12, mwaka huu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: POLISI YAZUNGUMZIA KIFO CHA MASHALI, FAMILIA YATAJA TAREHE YA MAZISHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top