• HABARI MPYA

  Jumatano, Oktoba 26, 2016

  YANGA IMETUMIA VIGEZO VIPI KUMUONDOA PLUIJM?

  MRENO Jose Mourinho ni kocha wa nne kufanya kazi Manchester United tangu mwaka 2013 alipojiuzulu Sir Alex Ferguson.
  Baada tu ya kuondoka Ferguson aliyefanya kazi kuanzia mwaka 1986 hadi 2013, David Moyes akawa kocha wa Manchester United.
  Na Moyes alikuwa pendekezo la Sir Ferguson mwenyewe, lakini bahati mbaya hakudumu, kwani ndani ya mwaka moja akafukuzwa. 
  Hakumaliza msimu na aliyekuwa Msaidizi wake, Ryan Giggs akawa kocha wa muda kumalizia msimu.
  Baada ya hapo, United ikamuajiri Mholanzi mwenye heshima kubwa katika dunia ya soka, Louis van Gaal ambaye pamoja na kuvumiliwa sana, lakini alifanya kazi kwa miaka miwili tu (2014–2016).
  Mei mwaka huu Man United ikaandika zama mpya chini ya Mreno mwenye mbwembwe na majivuno mengi, Jose Mourinho.
  Hata kabla hajamaliza nusu mwaka, au nusu msimu tayari Mourinho naye amekwishaanza kuzungumziwa kuondoka na hiyo ni baada ya kipigo cha 4-0 kutoka kwa Chelsea mwishoni mwa wiki.
  Na kwa ujumla, pamoja na kusajili wachezaji wa bei kubwa akiwemo kiungo Mfaransa, Paul Pogba aliyevunja rekodi ya klabu na Ligi Kuu kwa ujumla, Mourinho hajawa na mwanzo mzuri Manchester United.
  Alishinda Ngao ya Jamii katika mechi ya kufungua pazia la msimu, lakini hiyo si kitu sana kwa mashabiki wa Masheta Wekundu ambao wanaanzia kuhesabu kudorora kwa timu hiyo tangu alipoondoka Ferguson hadi sasa.
  Kitu kimoja tunaweza kukubaliana wengi ni kwamba Manchestrer United wanahangaika na benchi la Ufundi tangu kuondoka kwa Ferguson.
  Hawakutaka kuufuata ushauri wa Ferguson juu ya Moyes wakaona wawafuate makocha wakubwa, lakini matokeo yake ni kuendelea kubadilisha makocha.
  Jana kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm aliwaaga wachezaji wa Yanga kwenye mazoezi ya asubuhi.  
  Pluijm alizungumza na wachezaji wa Yanga kwa dakika kadhaa Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, Dar es Salaam na akawatakia kila la heri chini ya kocha mpya ajaye.
  Pluijm amejiuzulu baada ya kukerwa na uongozi wa klabu kuleta kocha mpya, Mzambia George Lwandamina bila kumtaarifu, akisema huko ni kumvunjia heshima.
  Kocha huyo akakataa hadi nafasi ya Ukurugenzi wa Ufundi ambayo inasemekana Yanga ilitaka kumpa baada ya kumleta Lwandamina kuwa kocha Mkuu, akisema;.
  “Sipendelei hiyo kazi. Nataka kufanya kazi na wachezaji kila siku kwa matakwa ya moyo wangu. Ninaondoka, mimi ni kocha mkubwa na nina wasifu mzuri. Nitapata timu,”alisema.
  Pluijm aliagana na wasaidizi wake pia Juma Mwambusi, anayeiongoza timu kwa sasa, kocha wa makipa Juma Pondamali, Meneja Hafidh Saleh, Mtunza Vifaa vya timu, Mahmoud Omar ‘Mpogolo’ na Dk Edward bavu.
  Yanga ilirejea juzi kutoka Mwanza, ilikopita ikitokea Bukoba, mkoani Kagera ambako Jumamosi ilishinda 6-2 dhidi ya wenyeji Kagera Sugar katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.⁠
  Baada ya Pluijm, Wasaidizi wake wote, Juma Mwambusi, kocha wa makipa Juma Pondamali na Meneja Hafidh Saleh wote wazalendo wataondoka pia kuwapisha Mzambia Lwandamina atakayekuwa Kocha Mkuu, akisaidiwa na wazalendo Charles Boniface Mkwasa, Manyika Peter kocha wa makipa na Meneja, Sekilojo Chambua.  
  Ikumbukwe, Pluijm alikuwa katika kipindi cha pili kufundisha Yanga baada ya awali kufundisha kwa nusu msimu mwaka 2014, akimpokea Mholanzi mwenzake, Ernie Brandts kabla ya kwenda Uarabuni.
  Alikwenda Al Shoalah FC ya Saudi ya Arabia na nafasi yake ikachukuliwa na Mbrazil, Marcio Maximo ambaye naye alifanya kazi kwa nusu msimu kabla ya Pluijm kurejeshwa Januari mwaka jana. 
  Saudi Arabia ambako alikwenda na aliyekuwa Msaidizi wake, Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa – Pluijm  aliondoka baada ya kutofautiana na uongozi wa timu uliotaka kumsajilia wachezaji asiowataka.
  Pluijm anaondoka Jangwani baada ya kuiongoza Yanga katika jumla ya mechi 124, akishinda 77, sare 25 na kufungwa 22.
  Katika mechi 19 za nusu msimu mwaka 2014, alishinda 11, sare sita na kufungwa mbili, wakati katika mechi 106 za tangu mwaka jana, alishinda 66, sare 19 na kufungwa 20.
  Na anaondoka baada ya msimu mzuri uliopita, akibeba mataji yote matatu, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC).
  Pluijm pia aliiwezesha Yanga kufika hatua ya makundi ya michuano ya Afrika (Kombe la Shirikisho) kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998 na mara ya pili kihistoria. Yanga ilifika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka huu baada ya mwaka 1998 kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.
  Na kwa mafanikio hayo, haikuwa ajabu Pluijm akishinda tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwishoni mwa msimu uliopita. 
  Lakini kwa Yanga yote hayo si kitu na Mholanzi huyo anaondolewa, kitu ambacho siyo tu kumvunjia heshima mwalimu huyo, bali ni kuwadharau hadi mashabiki wa timu hiyo.
  Wana Yanga wanatakiwa kujua kama kuna sababu nyingine za ndani zinafanya Pluijm aondolewe kama si za kiufundi na kitaalamu, ambazo zinaonyesha alikuwa mtu sahihi kwa nafasi hiyo kuendelea na kazi.
  Maana alisaini mkataba mpya wa miaka miwili mwezi Julai tu mwaka huu, inakuwaje miezi mitatu baadaye tu anaondolewa?
  Kwa vyovyote Yanga ilihitaji kumpa nafasi Pluijm baada ya kuiwezesha kutwaa mataji yote msimu uliopita, kuwapa tiketi ya hatua ya makundi michuano ya Afrika kwa mara ya kwanza tangu 1998.
  Na zaidi katika hatua ya makundi mwaka huu, Yanga imeweka rekodi ya kushinda mechi, wakati mwaka 1998 ilifungwa na kutoa sare tu nyumbani na ugenini.
  Chini ya Pluijm kwa mara ya kwanza Yanga imezifunga timu za Kaskazini mwa Afrika (Al Ahly ya Misri na MO Bejaia ya Algeria zote 1-0) jambo ambalo timu haikuweza kabla tangu ina ‘Kompyuta’ ya mpira, Sunday Manara miaka 1970, baba wa Msemaji wa Simba, Hajji.
  Hivyo ndivyo vitu ambavyo wenzetu Wazungu na nchi nyingine zilizoendelea wanaangalia – rekodi kabla ya kufikia maamuzi.
  Je, Yanga wametumia vigezo gani kumuondoa Pluijm?
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA IMETUMIA VIGEZO VIPI KUMUONDOA PLUIJM? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top