• HABARI MPYA

  Jumanne, Oktoba 25, 2016

  PLUIJM AWAAGA WACHEZAJI WA YANGA, AWATAKIA KILA LA HERI CHINI YA KOCHA MPYA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KOCHA Hans van der Pluijm amevalia mkanda nje na kwenda kuwaaga wachezaji wa Yanga leo kwenye mazoezi ya asubuhi.  
  Pluijm alizungumza na wachezaji wa Yanga kwa dakika kadhaa Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, Dar es Salaam na akawatakia kila la heri chini ya kocha mpya ajaye.
  Pluijm amejiuzulu baada ya kukerwa na uongozi wa klabu kuleta kocha mpya, Mzambia George Lwandamina bila kumtaarifu, akisema huko ni kumvunjia heshima.
  Kocha huyo akakataa hadi nafasi ya Ukurugenzi wa Ufundi amabyo inasemekana Yanga ilitaka kumpa baada ya kumleta Lwandamina kuwa kocha Mkuu.
  Pluijm amezungumza na wachezaji wa Yanga kwa dakika kadhaa leo Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, Dar es Salaam na akawatakia kila la heri chini ya kocha mpya
  Pluijm alizungumza faragha pia na aliyekuwa msaidizi wake namba moja, Juma Mambusi
  Pluijm akizungumza na wachezaji chini ya mti Kurasini leo
   

  “Sipendelei hiyo kazi. Nataka kufanya kazi na wachezaji kila siku kwa matakwa ya moyo wangu. Ninaondoka, mimi ni kocha mkubwa na nina wasifu mzuri. Nitapata timu,”alisema.
  Pluijm aliagana na wasaidizi wake pia Juma Mwambusi, anayeiongoza timu kwa sasa, kocha wa makipa Juma Pondamali, Meneja Hafidh Saleh, Mtunza Vifaa vya timu, Mahmoud Omar ‘Mpogolo’ na Dk Edward bavu.
  Yanga ilirejea jana kutoka Mwanza, ilikopita ikitokea Bukoba, mkoani Kagera ambako Jumamosi ilishinda 6-2 dhidi ya wenyeji Kagera Sugar katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.⁠
  Uongozi wa Yanga unamuondoa Pluijm na Wasaidizi wake wote, Juma Mwambusi, kocha wa makipa Juma Pondamali na Meneja Hafidh Saleh wote wazalendo wataondoka pia kuwapisha Mzambia Lwandamina atakayekuwa Kocha Mkuu, akisaidiwa na wazalendo Charles Boniface Mkwasa, Manyika Peter kocha wa makipa na Meneja, Sekilojo Chambua.  
  Ikumbukwe, Pluijm yupo katika kipindi cha pili kufundisha Yanga baada ya awali kufundisha kwa nusu msimu mwaka 2014, akimpokea Mholanzi mwenzake, Ernie Brandts.
  Alikwenda Al Shoalah FC ya Saudi ya Arabia na nafasi yake ikachukuliwa na Mbrazil, Marcio Maximo ambaye naye alifanya kazi kwa nusu msimu kabla ya Pluijm kurejeshwa Januari mwaka jana. 
  Saudi Arabia ambako alikwenda na aliyekuwa Msaidizi wake, Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa – Pluijm  aliondoka baada ya kutofautiana na uongozi wa timu uliotaka kumsajilia wachezaji asiowataka.
  Franciscus Johannes ‘Hans’ van der Pluijm alizaliwa Januari 3 mwaka 1949 na alianzia kwenye kucheza soka akiwa kipa.
  Enzi zake aliidakia kwa miaka 28 klabu ya FC Den Bosch akicheza mechi 338 ndani ya misimu 18 na alipostaafu baada ya kuumia goti akawa kocha wa timu hiyo.
  Alianza vyema ukocha akiiwezesha FC Den Bosch kutwaa ubingwa wa Daraja la Kwanza na kupanda Ligi Kuu na ndiye aliyempa nafasi ya kwanza mshambuliaji Ruud van Nistelrooy akiwa kinda wa miaka 17 tu kucheza kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
  Aprili mwaka 1995, alisaini Mkataba wa miaka miwili na SBV Excelsior kabla ya kutimuliwa Januari 1997 na nafasi yake ikachukuliwa na Msaidizi wake, John Metgod. 
  Hiyo ilifuatia timu hiyo ya Rotterdam kushinda mechi mbili tu na sare tatu katika mechi 17 za msimu mzima.
  Baada ya kuboronga Ulaya, ndipo akahamia Afrika mwaka 1999, alipokwenda kufundisha Ashanti Gold SC ya Ghana, akianza na Mkataba wa mwaka mmoja. 
  Ajax ya Uholanzi ikanunua hisa katika klabu hiyo Ijumaa ya Juni 18, mwaka 1999 asilimia 51 naye akatupiwa virago na kuhamia Saint-George SA ya Ethiopia kabla ya mwaka 2010 kujiunga na B-Juniors Feyenoord ya Ghana, ambayo ni tawi la timu hiyo ya Rotterdam.
  Mwaka 2012 alijiunga na Berekum Chelsea ambako pia alifukuzwa mwaka juzi na kuhamia Medeama ya Ghana pia ambako nako alifukuzwa baada ya mechi saba tu, kufuatia matokeo mabaya mwanzo mwa msimu, akivuna pointi nane kati ya 21.
  Pluijm anaondoka Jangwani baada ya kuiongoza Yanga katika jumla ya mechi 124, akishinda 77, sare 25 na kufungwa 22.
  Katika mechi 19 za nusu msimu mwaka 2014, alishinda 11, sare sita na kufungwa mbili, wakati katika mechi 106 za tangu mwaka jana, alisema 66, sare 19 na kufungwa 20.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: PLUIJM AWAAGA WACHEZAJI WA YANGA, AWATAKIA KILA LA HERI CHINI YA KOCHA MPYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top