• HABARI MPYA

    Sunday, May 10, 2015

    MCHEZAJI WA ZAMANI WA TP MAZEMBE AFARIKI DUNIA, ALIICHEZEA DRC KOMBE LA DUNIA 1974

    Na George Akpayen, KINSHASA
    BEKI wa zamani wa kimataifa wa Zaire (sasa DRC), na klabu ya TP Mazembe, Joseph Mwepu Ilunga (pichani kushoto) amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.
    Ilunga amefariki akiwa ana umri wa miaka 66 katika hospitali ya Saint Joseph Hospital mjini Kinshasa, mji Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo jana Ijumaa.
    Huyo ni miongoni mwa nyota walioipeleka Kongo Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1974, ambako alifanya kituko kwa kutoka katika mstari wa ukuta wa timu yake kwenda kuupiga mpira wa dhabu ambao wachezaji wa Brazil walikuwa wanajiandaa kupiga kabla ya filimbi ya refa.
    Klabu yake ya zamani, TP Mazembe ambayo kikosi chake cha sasa kina Watanzania wawili, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, imeelezea machungu yake juu ya msiba huo.
    "TP Mazembe imepokea kwa machungu makubwa taarifa za kifo cha Mwepu ILUNGA, ambaye alichezea klabu yetu kuanzia mwaka 1969 hadi 1980 na akafundisha timu ya vijana ya TPM,”. 
    Winga wa DRC na Crystal Palace ya Uingereza, Yannick Bolasie, ambaye alifundishwa na Ilunga timu ya taifa, ametuma salamu za rambirambi juu ya msiba huo.
    “Habari za kuhuzunisha, kifo cha Mwepu Ilunga, wakati wote alikuwa ananipa ushauri, natumai kuifanyia makubwa nchi kama alivyofanya nyeye (ili kumuenzi),” amesema mchezaji huyo wa Crystal Palace.
    Kabla ya kifo chake jana, Ilunga alikuwa Kocha Msaidizi wa DRC, chini ya kocha Mkuu, Florent Ibenge wakati wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2015 nchini Equatorial Guinea.
    Ilunga alikuwamo kwenye kikosi cha TP Mazembe kilichoshinda Kombe la Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa) mara mbili mfululizo mwaka 1967 na 1968.
    Pia alikuwa sehemu ya kikosi kilichopata mafanikio zaidi Zaire mwishoni mwa miaka ya 1960 na mwanzoni mwa miaka ya 1970 ambacho kilitwaa Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1968 na 1974. Pumzika kwa amani Ilunga, Wakongo wataendelea kukumbuka.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MCHEZAJI WA ZAMANI WA TP MAZEMBE AFARIKI DUNIA, ALIICHEZEA DRC KOMBE LA DUNIA 1974 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top