Na Vincent Malouda, NAIROBI
LICHA ya kupuuza amri ya mahakama na kucheza mechi za ufunguzi wa ligi kuu ya taifa la Kenya, mfululizo wa kesi kortini majuma mawili yaliyopita yamefanya ligi kuu Kenya kusitishwa hadi tarehe 13 Machi wakati hakimu Roselyn Aburili atakapo fanya uamuzi wa mwisho.
Aburili anatarajiwa kufanya uamuzi kuhusu amri iliyotolewa kwa kampuni inayosimamia ligi kuu kusitisha ligi hiyo kufuatia ombi la Shirikisho la Soka, FKF, baada ya wadau hao kutoelewana kuhusu jumla ya timu zitakazoshiriki ligi kuu msimu wa 2015.
Mabingwa wa Kenya, Gor Mahia ndiyo wapinzani wakuu wa FKF
Kwenye hafla ya kusikiza kesi hiyo tarehe 3 Machi, Aburili alizipa pande zote mbili yaani KPL na FKF kuafikiana chini ya masaa 48 la sivyo atasukumwa kufanya uamuzi kwa mujibu wa sheria jambo ambalo halukutendeka kwani mawakili wa FKF na KPL walishindwa kuafikiana na kupelekea Aburili kutaka pande zote mbili kuwasilisha maombi yao kufikia siku ya jumatatu tarehe 9 Machi aliposikiza tena pande hizo hapo jana Alhamisi.
"Kwa vile pande zote mbili zimeshindwa kutatua suala hili nje ya mahakama, sisi hatuna budi ila kuendelea kusikia maombi yao. Natumaini hilo ndilo jambo la mwisho manake watu wote wana mchecheto wa kujua uamuzi wa mahakama,” Aburili alisema baada ya kusikiza kesi hizo.
Wakati huo huo, makamu mwenyekiti wa FKF Sammy Sholei na mjumbe wa FKF tawi la Nairobi Dan Shikanda ambao walipigwa marufuku na shirikisho hilo chini ya rais Sam Nyamweya kwa kumshitaki katika korti za kawaida mwaka 2012 pia waliomba kujumlishwa katika kesi hiyo kama pande zenye matakwa ya kibinafsi.
Maombi ya wawili hao yameweza kukubaliwa leo, Ijumaa na sasa watakuwa mojawapo wa KPL kwenye kesi hiyo dhidi ya FKF juma lijalo.
FKF inawakilishwa na mwenyekiti wa chama cha wanasheria Kenya, LSK, Eric Mutua huku KPL ikiwakilishwa na wakili Geoffrey Obura nao Sholei na Shikanda wanasimamiwa na wakili Hellen Ngesa.
Zaidi ya mashabiki 100 walijumuika katika majengo ya mahakama hiyo kuu yaliyopo Milimani, Nairobi hapo jana kusikiliza kesi hiyo ili kutatua migogoro ya soka juu ya muundo wa Ligi Kuu msimu huu baada ya FKF na KPL kwa mara nyingine tena kushindwa kukubaliana ndani ya masaa aliyotoa Aburili.
Huku ligi kuu ya Kenya ikiwa imesimamishwa, ligi mkabala ya FKF inaendelea ino wikiendi huku jumla ya mechi nane zikiwa zimeratibiwa kupigwa, zote ziking’oa nanga saa tisa alasiri.



.png)
0 comments:
Post a Comment