• HABARI MPYA

    Sunday, November 02, 2014

    VIONGOZI SIMBA SC WAKIKUBALI KUENDELEA KUPAPASA KIZANI, WAWE TAYARI KUJITIA ‘NAJISI’

    AJIRA ya kocha Patrick Phiri iko shakani katika klabu ya Simba SC, kufuatia timu hiyo kucheza mechi sita bila kushinda hata moja, ikitoa sare zote.
    Simba SC jana imetoa sare ya sita, baada ya kufungana bao 1-1 na wenyeji Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
    Kabla ya mchezo huo, uongozi wa Simba SC ulitoa angalizo, ukisema unampa Phiri mechi mbili, ya jana na ya wiki ijayo kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri, vinginevyo atavunjiwa Mkataba.
    Mechi ya kwanza ametoa sare, na sasa anarejea Dar es Salaam kuanza kuandaa timu kwa ajili ya mchezo na Ruvu Shooting Uwanja wa nyumbani, Taifa. 
    Ikumbukwe kabla ya mchezo huo, Simba SC ilisimamisha wachezaji wake watatu, wote viungo Shaaban Kisiga ‘Malone’, Amri Kiemba ‘Jeshi la Jiwe’ na Haroun Chanongo kwa sababu tofauti.
    Kisiga alituhumiwa kuwatolea maneno ya kifedhuli viongozi, wakati Kiemba na Chanongo walituhumiwa kucheza chini ya kiwango, tofauti na wanavyokuwa timu ya taifa.
    Wachezaji wote walitakiwa kufika katika kikao cha Kamati ya Nidhamu Alhamisi kujibu tuhuma zao, baada ya kurudishwa Dar es Salaam, timu ikiwa Mbeya siku moja baada ya mchezo na Prisons, ulioisha kwa sare ya 1-1. 
    Lakini kwa mujibu wa Rais wa klabu, Evans Aveva wachezaji hao hawakutokea, Kisiga pekee akitoa udhuru wa kukwama kwenye foleni, wakati Chanongo na Kiemba hawakutoa taarifa yoyote.
    Inaonekana na wachezaji wenyewe wamechoshwa na wako tayari kwa lolote- hata kufukuzwa katika klabu, jambo ambalo hakuna uhakika sana kama uongozi wa Simba SC upo tayari, kwa sababu wachezaji hao ni wazuri na dhahiri watachukuliwa na wapinzani wao tu, kama Yanga, basi Azam FC.
    Kwa ujumla hamkani si shwani ndani ya Simba SC kutokana na matokeo haya na uongozi wa Simba SC unaonekana kupapasa kizani.
    Unatoka kufukuza wachezaji ambao uliamini ni sababu ya matokeo hayo, na unatoa angalizo kwa kocha asipopata matokeo mazuri ndani ya mechi mbili, ataondolewa.
    Pekee hii inatosha kutilia shaka maamuzi ya uongozi wa Simba SC juu ya adhabu ya akina Kiemba- labda wawe na sababu za ndani zaidi ambazo hawataki kuziweka basi.

    SAHIHI KUMFUKUZA PHIRI HATA ASIPOSHINDA DHIDI YA RUVU SHOOTING?
    Mzambia huyo hakuwemo kabisa kwenye mipango ya timu hiyo msimu huu, bali Mcroatia Zdravko Logarusic ndiye aliyeandaliwa kuwa mwalimu wa Simba SC.
    Logarusic aliongezewa Mkataba Julai mwaka huu baada ya ule wa awali wa miezi sita, tangu Desemba mwaka jana kumalizika.
    Loga ndiye aliyeiandaa timu kabla ya msimu hadi alipoamini imeiva, ikaanza kucheza mechi za kujipima nguvu.
    Lakini baada ya kufungwa mabao 3-0 katika mchezo wa Simba Day, Agosti mwaka huu akafukuzwa ghafla, Aveva akisema Mcroatia huyo haendani na maadili ya klabu.
    Wakati Simba SC ikiwa chini ya kaimu kocha, Suleiman Matola aliyekuwa Msaidizi wa Loga, uongozi ukafanya mpango wa haraka wa kumsaka Phiri, ambaye aliifundisha klabu hiyo kwa awamu tatu tofauti awali na kwa mafanikio.
    Bahati nzuri kwao, kwa historia nzuri ya nyuma baina yao, mwalimu huyo akakubali kuja tena Dar es Salaam kufanya kazi.
    Sijui ni ripoti gani ya maandalizi ya timu alipewa Phiri, lakini baada ya kuanza kazi, alionekana kuipa timu mazoezi ya kawaida sana na si ya kujenga stamina ya wachezaji.
    Labda aliambiwa kazi hiyo tayari ilikwishafanyika chini ya Loga- lakini bahati nzuri au mbaya, alipoingia kwenye mechi za majaribio alifanya vizuri. 
    Watu walifurahia kiwango cha Simba SC katika michezo ya kirafiki chini ya Phiri, wachezaji wapya, Pierre Kwizera, Elius Maguri, Ibrahim Hajibu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Paul Kiongera wote walionyesha mwanzo mzuri kwenye michezo hiyo.
    Lakini katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu, Simba SC iliongoza 2-0 hadi mapumziko kabla ya kurudishiwa mabao yote kipindi cha pili na kupata sare ya 2-2 nyumbani.
    Mechi mbili zilizofuata, Simba SC iliongoza tena kwa bao 1-0 dhidi ya Polisi Moro na baadaye Stand United, kabla ya kurudishiwa mabao kipindi cha pili pia.
    Sare ya tatu ikaanza kuleta hali ya mshituko na ‘wataalamu’ wakaanza kuichambua timu- lakini kikubwa ambacho wengi tulikiona, Simba SC haikuwa na stamina ya kucheza dakika 90.
    Timu ilionekana kuanza kutepeta baada ya dakika 70 na hata mabadiliko yaliyokuwa yakifanyika hayakuweza kuleta tija.
    Wakati huo huo, likaingia tatizo la majeruhi mfululizo, wachezaji ambao walikuwa kwenye mipango ya Phiri kwa ajili ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza wakaanza kuumia mfululizo.
    Dhahiri Phiri akaingia kwenye mwanzo mgumu, ingawa timu ilionyesha mabadiliko taratibu na hata ikatoa sare tatu zaidi katika michezo ambayo kihistoria ni migumu kwa Simba SC.
    Simba SC dhidi ya Yanga SC, au kucheza Mbeya na Prisons na Mtibwa Sugar Morogoro, zote ni mechi ngumu hizi.
    Mabingwa Azam FC, walilazimishwa sare na Prisons mjini Mbeya, washindi wa pili wa Ligi Kuu msimu uliopita, Yanga SC walifungwa 2-0 na Mtibwa Morogoro.
    Mechi tatu za mwanzo, Simba SC ilikubali sare kwa mapungufu yenye kuonekana, lakini sare zilizofuata ni za kimchezo zaidi kulingana na hali halisi.
    Sitarajii, Phiri atashindwa kupata pointi tatu mbele ya Ruvu Shooting japo kwa ushindi mwembamba- lakini hiyo itategemea na hali itakavyokuwa ndani ya timu.
    Baada ya mchezo wa jana, wachezaji wa Simba SC walilia- hadi kuinuliwa kuondoka Uwanja wa Jamhuri, dhahiri na wao hawaridhishwi na hali inayoendelea.
    Emmanuel Okwi aliumia kipindi cha pili na Dk Yassin Gembe akaona hawezi kuendelea, lakini Mganda huyo alilazimisha kubaki uwanjani kuipigania ushindi timu, kabla ya kocha Phiri kumuita nje, yeye mwenyewe akiwa hajaridhishwa na hilo.
    Ninachokiona, viongozi wa Simba SC wanahitaji kuungana na wachezaji na benchi lao la Ufundi katika kipindi hiki kigumu, kuwa kitu kimoja kupigania matokeo mazuri, pasipo kuvurugana.
    Kuna mechi moja zaidi kabla ya mapumziko ya takriban mwezi mzima na tayari Simba SC wametangaza watafanya kambi Afrika Kusini kujiandaa kumalizia ligi.
    Hiyo itakuwa fursa nzuri kwa klabu kujipanga upya- baada ya mwanzo huo mbaya, lakini kufikiria kumfukuza Phiri wakati huu itakuwa ni kuirudisha nyuma timu.
    Kila mwalimu ana falsafa zake, kuitoa timu kwa Loga tu akiwa amesajili aina ya wachezaji aliotaka yeye hadi kuipeleka kwa Phiri, tayari lilikuwa kosa kiufundi, lakini baada ya muda ambao Mzambia huyo amekaa na timu, bila shaka amepiga hatua fulani.
    Ushauri wa bure kwa Simba SC, wasifikirie kumfukuza Phiri kwa sasa, bali wampe muda zaidi- na zaidi watarajie mambo mazuri msimu ujao.  Kupapasa kizani ni hatari, unaweza kugusa ‘najisi’- Simba watambue hilo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: VIONGOZI SIMBA SC WAKIKUBALI KUENDELEA KUPAPASA KIZANI, WAWE TAYARI KUJITIA ‘NAJISI’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top