• HABARI MPYA

    Saturday, November 01, 2014

    SIMBA SC SARE TENA, MANYIKA MDOGO AOKOA PENALTI YA LUHENDE 1-1 NA MTIBWA MOROGORO

    Na Mahmoud Zubeiry, MOROGORO
    SIMBA SC imetoa sare ya sita mfululizo tangu kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kufungana bao 1-1 na Mtibwa Sugar, Uwanja wa Jamhuri, Morogoro jioni ya leo.
    Ushindi huo, unawafanya Mtibwa wafikishe pointi 14 kileleni mwa ligi hiyo, wakati Simba SC inaokota pointi ya sita baada ya timu zote kucheza mechi sita. 
    Simba SC ilikwenda kupumzika ikiwa tayari inaongoza kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na beki wa kimataifa wa Uganda, Joseph Owino dakika ya 35 kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Emmanuel Okwi.
    Kiungo wa Simba SC, Awadh Juma akipambana na viungo wa Mtibwa Sugar leo Uwanja wa Jamhuri

    Kipa Peter Manyika alifanya kazi nzuri dakika ya 44, baada ya kuokoa mkwaju wa penalti wa beki David Luhende. Penalti hiyo ilitolewa na refa Amon Paul wa Mara baada ya kiungo Awadh Juma kumchezea rafu kwenye eneo la hatari mshambuliaji Ame Ally.   
    Kipindi cha pili, Mtibwa Sugar walicharuka na kuanza kupeleka mashambulizi ya nguvu zaidi langoni mwa Simba SC.
    Hali hiyo iliwafanya vinara wa hao wa Ligi Kuu wapate bao la kusawazisha dakika ya 58, mfungaji Mussa Hassan Mgosi aliyetumia makosa ya beki wa kulia, William Lucian ‘Gallas’ kuchanganyana na kipa wake, Manyika Jr.
    Manyika alitoka vizuri angoni kuufuata mpira, lakini Gallas akawahi kuukaribia na kipa huyo akarudi nyuma, lakini beki wake akazembea hivyo kumpa mwanya Mgosi kuifunga timu yake zamani kiulaini. 
    Baada ya bao hilo, Simba SC walicharuka na kuanza kushambulia mfululizo langoni mwa Mtibwa kujaribu kujinasua kwenye balaa la sare, lakini uimara wa safu ya ulinzi wa Wakata Miwa hao, chini ya kipa Said Mohamed uliwanyima mabao.
    Mtibwa Sugar; Said Mohammed, Hassan Ramadhani, David Luhende, Andrew Vincent, Salim Mbonde, Shaaban Nditi, Mussa Ngosi, Mohamed Ibrahim, Ame Ally, Mussa Nampaka na Ally Shomary.
    Simba SC; Peter Manyika, William Lucian ‘Gallas’, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Joseph Owino, Jonas Mkude, Ramadhani Singano ‘Messi’, Awadh Juma, Elias Maguri/Amisi Tambwe dk76, Said Ndemla na Emmanuel Okwi/Uhuru Suleiman dk75.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC SARE TENA, MANYIKA MDOGO AOKOA PENALTI YA LUHENDE 1-1 NA MTIBWA MOROGORO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top