• HABARI MPYA

    Thursday, November 06, 2014

    PHIRI AMPA WOSIA MKUDE; “BAKI SIMBA, UKIENDA YANGA AU AZAM UTAJIMALIZA”

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KOCHA wa Simba SC, Patrick Phiri amemuasa kiungo Jonas Mkude asifikirie kuondoka katika klabu hiyo kwa sasa kama anahitaji kukuza kiwango chake.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo, Phiri amesema kwamba kwanza amefurahishwa na hatua ya uongozi wa Simba SC kutaka kumuongezea mkataba mchezaji huyo- lakini pia anamuasa Mkude awe tayari kusaini mkataba wa Wekundu hao wa Msimnazi. 
    “Huu si wakati mwafaka kwake (Mkude) kuondoka hapa (Simba SC), anatakiwa kubaki ili kuimarisha kipaji chake na kukuza akili. Nafurahi viongozi wapo katika mchakato huo,”amesema Phiri.
    Jonas Mkude kushoto ameshauriwa kubaki Simba SC na kocha Phiri

    Mzambia huyo amemuasa Mkude kwamba endapo atavutiwa na ofa za Yanga SC au Azam FC, ajue akikubali kwenda kusaini huko atakuwa amekwenda kuua kipaji chake. “Simba ndiyo sehemu sahihi kwake,”amesema. 
    Mkude ambaye Mkataba wake unaisha ndani ya miezi sita Simba SC, amesema anataka Sh. Milioni 80 ili kusaini Mkataba mpya na amefungua milango kwa klabu nyingine pia itakayojimudu kutoa dau hilo.
    Lakini Mkude amesema kwamba anatoa kipaumbele kwa klabu yake, Simba SC katika hilo iwapo watakuwa tayari kumpa Milioni 80 za Tanzania.
    Mkude alipandishwa kikosi cha kwanza cha Simba SC mwaka 2011 akitokea timu ya vijana ya klabu hiyo na tangu kifo cha kiungo Patrick Mafisango yeye ndiye ameziba pengo hilo katika nafasi ya kiungo wa ulinzi.
    Kwa sasa, Mkude ni mchezaji kipenzi cha wapenzi wa Simba kutokana na juhudi zake na kujituma awapo uwanjani.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PHIRI AMPA WOSIA MKUDE; “BAKI SIMBA, UKIENDA YANGA AU AZAM UTAJIMALIZA” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top