• HABARI MPYA

    Thursday, November 13, 2014

    KASEJA ‘AWATALIKI’ YANGA SC KUPITIA KWA WAKILI

    Na Abdul Salim, DAR ES SALAAM
    MLINDA mlango Juma Kaseja amewasilisha barua kwa mwajiri wake, Yanga SC kutoa taarifa ya kuvunja makataba wake, uliobakiza mwaka mmoja.
    Kwa mujibu wa habari kutoka Yanga SC, Kaseja ameandika barua akitaja sababu ya kuvunjwa Mkataba huo ni kukiukwa kwa masharti yaliyokubaliwa wakati wa kusainiwa Novemba 8, mwaka jana.
    Barua ya Kaseja iliyotumwa kupitia wakili wake, Mbamba & Co Advocates, Kaseja amesema wakati wa kusainiwa Mkataba huo ilikubaliwa malipo ya Sh. Milioni 40 yafanyike kwa awamu mbili.
    Amesema awamu ya kwanza, alilipwa Sh. Milioni 20 baada ya kusaini Mkataba huo, na ikakubaliwa fungu lililobaki apatiwe Janauri 15, mwaka huu na kwa sababu malipo ya fedha ndio msingi wa Mkataba wenyewe, kushindwa kulipa fedha hizo kunaondoa uhalali wake.
    Kaseja amesema kwa kuwa Mkataba baina yake na Yanga SC umevunjwa rasmi, sasa anaamua kutafuta klabu nyingine.
    Juma Kaseja amewaandikia barua Yanga SC kupitia wakili kuwataarifu kuvunja nao Mkataba

    Kauli ya Kaseja, inakuja siku moja baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe kusema kwamba milango iko wazi kwa mlinda mlango huyo kurejea nyumbani Msimbazi. 
    Hans Poppe alisema hawajafanya mawasiliano yoyote na kipa huyo wa Yanga SC, bali wamekuwa wakisoma tu kwenye vyombo vya habari juu ya kurejea kwake, Simba SC.
    “Hatujawahi kuzungumza na Kaseja, ila yeye kama anataka kurudi hapa, ni nyumbani. Alikuwepo, akaenda Yanga SC, akarudi na ameenda tena huko, hakuna ubaya akirudi, anakaribishwa tu,”alisema.
    Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) amesema hata mara ya mwisho Kaseja hakuondoka vibaya Simba SC, hivyo anakaribishwa wakati wowote.
    “Mara ya mwisho aliondoka hapa baada ya Mkataba wake kwisha. Yeye akaona atafute sehemu yenye maslahi zaidi, amekwenda. Ila hapa ni nyumbani kwake, akitaka kurudi wakati wowote milango iko wazi,”aliongeza.
    Tayari Yanga SC imekwishapata pigo kwa kupuuzia makubaliano ya kimkataba na wachezaji wake, baada ya mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi naye kuvunja Mkataba wake Julai mwaka huu kwa sababu kama za Kaseja.
    Siku Kaseja aliposaini Yanga SC, hapa akiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Usajili, Abdallah Bin Kleb

    Kesi ya Okwi na Yanga SC ilifikishwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambako Mganda huyo alishinda na kwenda kusaini timu yake ya zamani, Simba SC. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KASEJA ‘AWATALIKI’ YANGA SC KUPITIA KWA WAKILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top