• HABARI MPYA

    Sunday, October 05, 2014

    YANGA WAANZA KUPAA TARATIBU, WAICHAPA JKT 2-1…YONDAN AFUNGA BAO SAFI, NIYONZIMA NAYE…

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya jioni ya leo kuichapa JKT Ruvu mabao 2-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ushindi huo, unaifanya timu ya Mbrazil Marcio Maximo itimize pointi sita baada ya mechi tatu, ikifungwa moja na Mtibwa Sugar 2-0 ugenini na kushinda 2-1 na Prisons. 
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Refa Martin Saanya wa Morogoro aliyesaidiwa na Hassan Kilindo wa Dar es Salaam na Grace Wamara wa Kagera, Yanga SC ilikwenda kupumzika ikiwa inaongoza 1-0.
    Bao hilo lilifungwa na beki Kevin Patrick Yondan dakika ya 35, aliyefumua shuti kali baada ya kupokea pasi maridadi ya kiungo Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima.
    Andrey Coutinho na Nadir Haroub 'Cannavaro' kushoto wakimpongeza Kevin Yondan (katikati) baada ya kufunga bao la kwanza
    Haruna Niyonzima akimtoka beki wa JKT Ruvu, Haruna Shamte 

    Shambulizi lililozaa bao hilo lilianzishwa na yeye mwenyewe Yondan, baada ya kufanikiwa kuuzuia mpira wa Iddi Mbaga mbele kidogo ya boksi lao na kupanda nao hadi mbele ya mstari wa kuugawa Uwanja kabla ya kumpasia Niyonzima.
    Niyonzima alimiliki vizuri mpira huo, huku akidhibitiwa na beki Napho Zuberi na hata hivyo akafanikiwa kumhadaa na kumpasia Yondan aliyekuwa kwenye nafasi nzuri- akafunga kwa shuti kali.
    Kipindi cha pili, mchezo uliendelea kuwa wa kasi, nguvu na mashambulizi ya pande zote mbili- huku makipa wote wa timu zote mbili, Jackson Chove wa JKT na Deo Munishi ‘Dida’ wa Yanga wakifanya kazi ya ziada.
    Yanga ilifanikiwa kupata bao la pili dakika ya 74, mfungaji Haruna Niyonzima kwa mpira wa adhabu kutoka umbali wa mita 19- baada ya kiungo Hassan Dilunga kuchezewa rafu na Jabir Aziz.
    Shambulizi lililozaa bao hilo lilianzishwa na Mrisho Ngassa aliyetokea benchi kipindi cha pili kumbadili Andrey Coutinho. Ngassa alipokea pasi ya Yondan akapanda vizuri akiwatoka wachezaji wa JKT, kabla ya kuangushwa nje kidogo ya boksi.
    Niyonzima akamuanzishia mpira mfupi Dilunga, ambaye akachezewa tena rafu na kuwa faulo iliyosabisha bao la ushindi.    
    Jabir Aziz aliifungia JKT inayofundishwa na Fredy Felix Minziro bao la kufutia machozi dakika ya 89 kwa shuti la umbali wa mita 23 baada ya wachezaji wa Yanga kuzubaa.  
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Edward Charles/Salum Telela dk55, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Mbuyu Twite, Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima/Nizar Khalfan dk82, Genilson Santana Santos ‘Jaja’, Andrey Coutinho/Mrisho Ngassa dk59 na Simon Msuva.
    JKT Ruvu; Jackson Chove, Ramadhani Shamte, Napho Zuberi, Madenge Ramadhani, Mohamed Fakhi, George Minja, Nashon Naftali, Jabir Aziz, Iddi Mbaga, Reliant Lusajo/Ally Bilal dk46 na Gido Simon/Amos Mgisa dk50.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WAANZA KUPAA TARATIBU, WAICHAPA JKT 2-1…YONDAN AFUNGA BAO SAFI, NIYONZIMA NAYE… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top