• HABARI MPYA

    Friday, October 03, 2014

    WAKILI NDUMBARO AMBAYE PIA NI MJUMBE WA BODI YA LIGI AILIMA BARUA TFF

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMPUNI ya Uwakili ya Meleta & Ndumbaro imeliandikia barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kulizuia kukata asilimia tano ya fedha za udhamini wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ikidai kuombwa kufanya hivyo na klabu.
    Katika barua iliyosainiwa na Dk. Damas Daniel Ndumbaro, kampuni hiyo imeitaka TFF kutofanya hivyo kwa sababu ni kinyume cha mikataba ya Vodacom, wadhamini wakuu wa Ligi Kuu na Azam Media Limited, walionunua haki za matangazo ya Televisheni. 
    Hata hivyo, katika barua ya Ndumbaro hakuna klabu iliyotajwa kuomba hilo- zaidi imesema klabu za Ligi Kuu zimeomba kampuni hiyo iwasaidie kuzuia mpango wa TFF kukata asilimia tano ya fedha za udhamini.
    Dk Ndumbaro kulia, ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Ligi, ameilima barua TFF kupitia kampuni yake ya Uwakili, meleta & Ndumbaro

    Mapema jana, Rais wa TFF, Jamal Malinzi alitoa ufafanuzi mzuri juu ya sakata hilo, akisema lengo la kufanya hivyo na kuanzisha mfuko wa Maendeleo ya vijana na akaitaka Bodi ya Ligi kuhakikishia inasimamia ukusanywaji wa fedha hizo. 
    Akizungumza na Waandishi wa Habari mchana wa jana, makao makuu ya TFF, Dar es Salaam- Malinzi alisema kwamba Bodi ya Ligi haina mamlaka ya kupinga maamuzi yoyote ya Kamati ya Utendaji na kwamba chombo pekee chenye uwezo wa kupinga maamuzi ya Kamati ya Utendaji ya TFF ni Mkutano Mkuu.
    Malinzi amesema fedha hizo zinatarajiwa kuingia kwenye mfuko maalum wa maendeleo ya vijana ulioundwa na Kamati yake ya Utendaji, chini ya Mwenyekiti, Leodegar Tenga ambaye ni rais wa zamani wa TFF.
    Amesema Mfuko huo utasimamia timu mbili za vijana chini ya umri wa miaka 12 itakayoanza kuandaliwa mara moja kwa ajili ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa 17 mwaka 2019, ambazo Tanzania wameomba uenyeji pamoja na U14 ambayo itawania tiketi ya Fainali za U17 mwaka 2017 nchini Madagascar.
    “Hizi timu zitaundwa mara moja na kuingia kambini, U12 watakwenda shule ya Alliance Academy (Mwanza) na wale U14 watakwenda shule ya Lord Burden (Bagamoyo) ambako watakuwa wanasoma na kufanya mazoezi kuandaliwa kwa michuano,”amesema 
    Kuhusu ‘mikwara’ ya eti klabu zitaenda mahakamani iwapo TFF itakata asilimia tano kwenye pato lao, Malinzi amesema Bodi ya Ligi Kuu ipo chini ya utaratibu.
    “Bodi ya Ligi Kuu ina vikao vyake halali kwa mujibu wa utaratibu, wanatakiwa wafuate utaratibu huo katika. Lakini pia nataka niseme, Bodi ya Ligi haijasaini Mkataba wowote wa udhamini, mikataba yote imesainiwa baina ya wadhamini na TFF,”amesema.
    Hata hivyo, Malinzi amesema wakati wa upitishwaji wa kanuni hiyo ya kukata asilimia tano kwenye pato la wadhamini wa Ligi Kuu, viongozi wa Bodi ya Ligi- Mwenyekiti Hamad Yahya na Makamu wake, Sheikh Said Muhammad pamoja na Mtendaji wa kuajiriwa, Silas Mwakibinga walikuwepo.
    Ndumbaro anafanya yote hayo, yeye mwenyewe akiwa Mjumbe wa kuteuliwa wa Bodi ya Ligi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WAKILI NDUMBARO AMBAYE PIA NI MJUMBE WA BODI YA LIGI AILIMA BARUA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top