• HABARI MPYA

    Monday, October 13, 2014

    MICHO: BADO NINA IMANI NA OKWI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KOCHA wa Uganda, Milutin Sredojevic ‘Micho’ amesema kwamba bado ana imani na mshambuliaji Emmanuel Okwi na anampa muda zaidi wa kurudisha kiwango chake, kabla ya kumuita tena kikosini mwake.
    Mwalimu huyo wa soka wa Kiserbia, jana alimuengua kikosini mwake Okwi baada ya kuonyesha kiwango cha chini akiichezea The Cranes dhidi ya Togo Jumamosi, lakini amesema ana bado ana imani sana na mchezaji huyo kwamba atarudi katika kiwango chake.
    Uganda iliondoka jana jioni kwenda Togo kwa ajili ya mchezo wa marudiano Kundi E Kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika huku Okwi akirejea Dar es Salaam tayari kwenda kuungana na klabu yake Simba SC, iliyopo Afrika Kusini.
    Okwi kushoto akiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe wakati anatangazwa kutejea Simba SC Agosti mwaka huu

    “Namuheshimu sana Emmanuel na nina imani naye, lakini tumemuengua kwa sasa kwa sababu hakidhi mahitaji yetu kwenye timu na haimaanishi si mchezaji wa The Cranes tena, ni kwa sasa tu”alisema Micho akizungumza na BIN ZUBEIRY jana kutoka Kampala, Uganda.
    Micho pia amemuacha Nahodha wake, Andy Mwesigwa, ambaye anatumikia adhabu baada ya beki huyo wa FC Ordabasy ya Kazakhstan kufikisha kadi mbili za njano ikiwemo ya jana, Uganda ikilala 1-0 Uwanja wa Namboole.
    Kikosi cha Uganda kilichoondoka jana ni, makipa; Robert Odongkara na Dennis Onyango, mabeki; Dennis Guma, Godfrey Walusimbi, Savio Kabugo, Isaac Isinde, Martin Kizza na Murushid Jjuuko, viungo ni: Tonny Mawejje, Aucho Khalid, Geoffrey 'Baba' Kizito, Brian Majweja, Kizito Luwagga na Moses Oloya, wakati washambuliaji ni Geofrey Massa (Nahodha), Daniel Sserunkuma, Yunus Sentamu na Brian Umony.
    Baada ya kutemwa na Uganda, Okwi sasa atalazimika kuwahi kambi yake ya klabu yake, Simba SC nchini Afrika Kusini ambayo imejificha kujiandaa na mchezo dhidi ya watani, Yanga SC Oktoba 18, Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MICHO: BADO NINA IMANI NA OKWI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top