• HABARI MPYA

    Saturday, October 04, 2014

    KIVUMBI LIGI KUU BARA, SIMBA NA STAND TAIFA, AZAM NA PRISONS MBEYA....YANGA KESHO TAIFA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    LIGI Kuu ya Vodadom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo katika viwanja vitano, mabingwa watetezi Azam FC wakiwa wageni wa Prisons Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, huku vigogo Simba SC wakiikaribisha Stand United Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Uwanja wa Jamhuri, Morogoro Polisi watacheza kwa mara ya kwanza nyumbani msimu huu watakapoikaribisha Kagera Sugar ya Bukoba ambayo itacheza ugenini kwa mara ya tatu mfululizo.
    Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Coastal Union watacheza kwa mara ya kwanza nyumbani watakapoikaribisha Ndanda FC ambayo itakuwa ikicheza mechi ya tatu mfululizo ugenini.
    Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Mbeya City watacheza mechi ya kwanza ugenini msimu huu watakapokuwa wageni wa Ruvu Shooting, ambao huo kwao utakuwa mchezo wa pili nyumbani.
    Ligi hiyo, inatarajiwa kuendelea kesho, wakati Yanga SC watakapomenyana na JKT Ruvu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Mtibwa Sugar wakiikaribisha Mgambo JKT ya Tanga.
    Macho na masikio ya wengi yanatarajiwa kuelekezwa kwenye mechi ya mabingwa Azam FC dhidi ya Prisons mjini Mbeya na vigogo Simba SC dhidi ya Stand kwa leo- wakati kesho watu watasikilizia Yanga SC.
    Simba SC watamenyana na Stand United Uwanja wa Taifa leo

    AZAM FC V PRISONS
    Baada ya kushinda mechi mbili mfululizo nyumbani 3-1 na Polisi Moro na 2-0 na Ruvu Shooting, mabingwa watetezi, Azam leo watacheza ugenini kwa mara ya kwanza.
    Azam FC inayowakosa nyota wake majeruhi, Frank Domayo, Joseph Kimwaga, Leonel Saint-Preux, John Bocco ‘Adebayor’ leo itakutana na Prisons tofauti na ya msimu ulioita.
    Baada ya kunusurika kushuka daraja msimu uliopita, timu ya jeshi la Magereza Tanzania, imeonekana kujiimarisha msimu huu ikianza kwa ushindi wa 2-0 ugenini dhidi ya Ruvu Shooting kabla ya kufungwa 2-1 kwa mbinde na Yanga SC, tena ikimpoteza beki wake Jacob Mwakalobo kipindi cha kwanza aliyetolewa kwa kadi nyekundu.
    Lakini Azam FC itashuka kwenye Uwanja wa Sokoine ikiwa na kumbukumbu nzuri mara ya mwisho ilipocheza huku iliifunga 2-1 Mbeya City na kutangaza ubingwa ikiwa na mechi moja mkononi.

    SIMBA SC V STAND UNITED
    Baada ya sare mbili mfululizo 2-2 na Coastal Union ikitoka kuongoza 2-0 hadi mapumziko na 1-1 na Polisi Moro pia ikiongoza hadi baada ya kipindi cha kwanza, Simba SC itajaribu kusaka ushindi wa kwanza leo dhidi ya timu iliyopanda msimu huu, Stand.
    Tayari Stand wamekwishaonja ladha ya ushindi katika Ligi Kuu kufuatia kushinda 1-0 katika mchezo wao uliopita dhidi ya wenyeji Mgambo JKT mjini Tanga.
    Lakini ikumbukwe Stand ilianza na kipigo cha nyumbani cha mabao 4-1 kutoka kwa Ndanda waliopanda nao Ligi Kuu msimu huu. Mshambuliaji Amisi Tambwe aliyeumia juzi, jana alifanya mazoezi Simba wakati Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ na Haroun Chanongo hawako tayari kwa mchezo wa leo.

    COASTAL UNION V NDANDA FC:
    Baada ya kuambulia pointi moja katika mechi zake mbili za ugenini, Coastal leo watasaka ushindi wa kwanza dhidi ya Ndanda, ambayo katika mechi zake mbili za awali, imeshinda moja na kufungwa moja, zote ugenini.
    Wakati Coastal ilidroo 2-2 na Simba SC mjini Dar es Salaam kabla ya kufungwa 1-0 na Mbeya City, Ndanda yenyewe ilianza na ushindi wa 4-1 Shinyanga mbele ya Stand United kabla ya kufungwa 3-1 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Manungu, Turiani mjini Morogoro. 

    POLISI MORO V KAGERA SUGAR:
    Baada ya kuambulia pointi moja katika mechi mbili za ugenini, ikifungwa 3-1 na Azam FC na kutoa sare ya 1-1 na Simba SC, Polisi itakuwa mawindoni leo.
    Kagera Sugar nayo ilianza kwa kuchapwa 1-0 na Mgambo mjini Tanga kabla ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Ruvu.

    RUVU SHOOTING V MBEYA CITY      
    Ikitoka kushinda 1-0 nyumbani dhidi ya Coastal Union, Mbeya City wataanza mawindo ya ugenini leo kwa kuwa wageni wa Ruvu Shooting.
    Mbeya City, ambayo ililazimishwa sare ya bila mabao na JKT Ruvu katika mchezo wake wa kwanza, itakutana na Ruvu Shooting ambayo imepoteza mechi zote mbili za kwanza.
    Ruvu ilifungwa 2-0 na Prisons Uwanja wa Mabatini katika mchezo wa kwanza, kabla ya kufungwa 2-0 na Azam FC, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
       
    YANGA SC V JKT RUVU
    Baada ya kushinda kwa mbinde dhidi ya Prisons, Yanga SC watajaribu kuendeleza wimbi la ushindi kesho wakicheza nyumbani kwa mara ya pili mfululizo.
    Yanga SC ilianza Ligi Kuu kwa kichapo cha mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza kutoka kwa Mtibwa Sugar ya Morogoro.
    Na kesho Yanga SC itataka kuwadhihirishia wapenzi wake kwamba iliteleza tu katika mchezo wa kwanza mjini Morogoro.

    MTIBWA SUGAR V MGAMBO JKT:
    Baada ya kushinda mechi mbili mfululizo, 2-0 dhidi ya Yanga SC Uwanja wa Jamhuri na 3-1 dhidi ya Ndanda FC Uwanja wa Manungu.
    Mtibwa Sugar itakutana na Mgambo JKT, ambayo imecheza mechi mbili awali nyumbani na kushinda 1-0 dhidi ya Kagera Sugar kabla ya kufungwa 1-0 na Stand United.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIVUMBI LIGI KUU BARA, SIMBA NA STAND TAIFA, AZAM NA PRISONS MBEYA....YANGA KESHO TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top