• HABARI MPYA

    Thursday, October 02, 2014

    KIPA YANGA SC ASEMA LIGI YA OMAN SI MCHEZO

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    KIPA wa zamani wa Yanga SC na Coastal Union ya Tanga, Juma Mpongo amesema soka ya Oman ni ya ushindani mkubwa, tofauti na alivyokuwa akifikiria awali.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY kutoka Muscat, Oman leo, Mpongo aliyewahi pia kucheza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), amesema Ligi Kuu ya Oman ni ngumu.
    “Mwanzoni nilikuwa nafikiri mpira wa huku rahisi, kumbe nilijidanganya. Nimekuja hapa, nimejionea. Jamaa wana Ligi moja nzuri na ngumu sana, timu nyingi ziko vizuri na zina wachezaji wazuri pia,”amesema.
    Mpongo anayedakia Seeb ya Ligi Kuu ya nchini humo amesema anaamini kucheza Oman kutamsaidia kuongeza uwezo wake kutokana na ushindani uliopo.
    Juma Mpongo kulia akiwa mazoezini Seeb mjini Muscat, Oman

    Mlinda mlango huyo aliyejiiunga na timu hiyo mwezi uliopita amesema kwamba hadi sasa amekwishadaka mechi tatu moja wakitoa sare ya bila kufungana leo na Al Musanaha wakati mbili za awali Seeb ilipoteza kwa kufungwa 1-0 dhidi ya Al Shabab na Saham.
    “Isipokuwa kuna kitu nimegundua, wakati ninafika timu yetu haikuwa na maandalizi mazuri, kwa sababu hivi sasa ndiyo tunaanza kuchanganya na ninaamini tutafanya vizuri baadaye,”amesema.
    Kikosi cha Seeb kilichoroa sare ya 0-0 na Al Musanah leo

    Mpongo amesema anamshukuru sana aliyekuwa kocha wa makipa wa Seeb, Mtanzania mwenzake, Manyika Peter aliyemuunganishia nafasi ya kusajiliwa na klabu hiyo.
    “Hii timu ilikuwa inataka kipa na kama utakumbuka Manyika alikuwa kocha wa makipa hapa ambaye kutokana na kazi yake nzuri walimuamini na wakampa jukumu la kuwatafutia kipa. Kwa sababu (Manyika) anajua uwezo wangu, akaniunganishia,”amesema.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIPA YANGA SC ASEMA LIGI YA OMAN SI MCHEZO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top