• HABARI MPYA

    Sunday, October 12, 2014

    HAPA SASA TUNAZUNGUMZA LUGHA YA SOKA, SUBIRA ITALETA KHERI ‘INSHAALLAH’

    WADAU watatu walipishana katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dar es Salaam kutoa maoni yao juu ya mustakabali wa soka ya Tanzania mwaka 1997.
    Nakumbuka alianza aliyewahi kuwa Mfadhili wa Simba SC, Azim Dewji akafuatia kocha maarufu, Syllersaid Mziray (sasa marehemu) na baadaye Mmarekani mwenye asili ya Tanzania, Alexander Otaqs Kajumulo.
    Hiyo ilifuatia Tanzania kutolewa na Burundi katika mechi ya kuwania tiketi ya Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1998 kwa kufungwa 1-0 nyumbani na ugenini.
    Maoni ya wadau wote hao yalifanana- walishauri Tanzania ijitoe kwa muda kwenye soka ya kimataifa na kuanza kujenga msingi imara wa soka yake kwanza kwa kuanzia kuwekeza kwenye soka ya vijana.

    Walisema kati ya miaka sita na nane, ingetosha Tanzania kuwa tayari na timu imara ya taifa ya ushindani kwa ajili ya kuwania tiketi za fainali za michuano mikubwa.
    Wakati ushauri huo unatolewa- ilikuwa ni miaka 17 tangu Tanzania icheze Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1980 nchini Nigeria, lakini leo imetimia miaka 24 bado tunasotea nafasi hiyo tena.
    Wamepita makocha wasiopungua 10 wazalendo na wa kigeni, lakini soka ya Tanzania haijaweza kujitutumua kuinuka tena na matokeo yake mashujaa wa taifa wameendelea kuwa wale wale waliokwenda Lagos mwaka 1980.
    Hao ni akina Leodegar Tenga (Nahodha), Athumani Mambosasa (marehemu), Idd Pazi, Juma Pondamali, Willy Kiango, Daud Salum ‘Bruce Lee’, Leopold Mukebezi, Ahmed Amasha, Mohamed Kajole (marehemu), Salim Amir, Jella Mtagwa, Mtemi Ramadhani, Mohamed ‘Adolph’ Rishard, Hussein Ngulungu, Juma Mkambi ‘Jenerali’ (marehemu), Omari Hussein ‘Keegan’ au Kakakuona, Thuwein Ally, Mohamed Salim, Peter Tino, Rashid Iddi Chama, Kocha Mkuu Slomir Wolk, Msaidizi wake Joel Bendera, Daktari Katala, Meneja wa timu, Mzee Mwinyi na Stanford Nkondora aliyekuwa Mkuu wa Msafara.
    Wote hao watatunukiwa nishani katika sherehe za miaka 50 ya uanachama wa Shirikisho la Tanzania (TFF) kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) baadaye mwaka huu.
    Tuna kingine cha kujivunia zaidi ya hilo la Lagos mwaka 1980 na kuendelea kulisimulia kwa mbwembwe na madaha bao la Peter Tino mjini Ndola katika sare ya 1-1 na wenyeji Zambia lililotupa tiketi hiyo? 
    Tumekuwa tukiwachoka haraka viongozi wa TFF kwa sababu Stars imeshindwa kurudia mafanikio hayo na kila kiongozi anayeingia madarakani, jitihada zake za awali ni kuhakikisha anakuwa na timu bora ya taifa.
    Viongozi wengine walithubutu kuita hadi wachezaji wacheza wa mabonanza na ‘Ligi za mchangani’ Ulaya wakiamini watakuja kuisaidia timu, lakini wapi!
    Jamal Emil Malinzi aliyeingia madarakani Oktoba mwaka jana akimpokea Leodegar Tenga baada ya Stars kukosa tiketi ya AFCON mwakani nchini Morocco, amekuja na dira mpya.
    Malinzi alianza na mpango wa maboresho ya Taifa Stars, akiunda jopo kuzunguka nchi nzima kusaka vipaji vipya vya kuchezea Stars, lakini kutokana na Watanzania kutokuwa na subira, mpango huo ukaonekana hauna maana, naye akaamua kuachana nao.
    Lakini sasa amekuja na dira mpya, ambayo ni mpango wa programu ya vijana inayolenga Fainali za Afrika za U17 mwaka 2019.
    Malinzi amesema katika utelezaji wa programu hiyo, wataanza na mashindano ya vijana chini ya umri chini ya miaka 12 yatakayofanyika Desemba mwaka huu mjini Mwanza, ambayo yatashirikisha kombaini za mikoa yote nchini.
    Mashindano hayo yatafanyika kuanzia Desemba 6 hadi 12 mwaka huu, na timu zinatakiwa kuwasili Mwanza, Desemba 5 mwaka huu. Bajeti ya mashindano hayo ni Sh. Milioni 350 na Malinzi amewashukuru Wakurugenzi wa shule za Alliance (James Bwire) na Lord Baden Powell (Kanali mstaafu Idd Kipingu) kwa kukubali shule zao kuwa za kwanza kuanzia programu hiyo ya vijana.
    Pia aliishukuru kampuni ya Symbion ambayo imetoa Sh. Milioni 100 kwa ajili ya kuunga mkono mashindano hayo ya U12. Symbion ni miongoni mwa wadau wanaoshirikiana na TFF katika mpango wa miaka mitano ya programu za vijana.
    Mkurugenzi wa Symbion, Stewart John Hall aliwaonyesha Waandishi wa habari programu hiyo. Wazi sasa tunaanza kurudi kule kule kwenye mawazo yaliyotolewa na akina Kajumulo, Mziray na Dewji mwaka 1997- kujenga msingi imara wa soka yetu.
    Wachezaji wetu wa Ligi Kuu kwa sasa na wachache wanaocheza nje, waendelee kuunda timu yetu ya taifa kwa sasa ya kuendelea kubahatisha, lakini timu ya uhakika tutarajie kutokana na mpango huu. Na mpango huu, unapaswa kuwa endelevu, ili wakati wote tumudu kuwa na timu imara kuanza za vijana hadi za wakubwa. Alamsiki. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HAPA SASA TUNAZUNGUMZA LUGHA YA SOKA, SUBIRA ITALETA KHERI ‘INSHAALLAH’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top