• HABARI MPYA

    Thursday, October 02, 2014

    BALAA GANI HILI SIMBA SC, TAMBWE AUMIA MAZOEZINI LEO, HOFU YATAWALA…AVEVA NA PHIRI WOTE ‘VIROHO JUU’

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa Simba SC, Amisi Tambwe leo amezua hofu kwa kocha Patrick Phiri na rais wa klabu hiyo, Evans Elieza Aveva baada ya kuumia mazoezi Uwanja wa Boko Veterani, Dar es Salaam.
    Tambwe aliumia goti baada ya kugongana na beki Abdi Banda na kushindwa kuendelea na mazoezi hadi akafungwa barafu baada ya kutibiwa kwa muda na Dk Yassin Gembe.
    Kocha Phiri alionekana mwenye wasiasi na kufuatilia kwa karibu hali ya mchezaji huyo wakati akitoka nje.
    “Hakikisha anakuwa vizuri, ni mchezaji wangu nayemtegemea,”alisema Phiri kumuambia Dk Gembe wakati anatoka nje na mchezaji huyo.

    Pigo; Amisi Tambwe akiwa nje baada ya kuumia goti mazoezini leo na kufungwa barafu. Kulia ni Issa Rashid 'Baba Ubaya'
    Tambwe akitoka nje baada ya kuumia mazoezini, huku kocha Phiri akifuatilia kwa karibu
    Tambwe akiugulia maumivu baada ya kuumia, huku kocha Msaidizi, Suleiman Matola akimtazama

    Mfungaji huyo bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita hakuweza kuendelea na mazoezi akaenda kuketi nje pamoja na beki Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ ambaye anaendelea na mazoezi mepesi baada ya kupata ahueni ya maumivu yake yaliyomuweka nje kwa wiki tatu sasa.
    Viongozi wa Simba SC wakiongozwa na Rais Aveva walikuwepo mazoezini pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Kassim Mohamed Dewji na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Mohammed Nassor ‘Steven Seagal’.
    Wote walipatwa hofu baada ya Tambwe kuumia na walitumia muda mwingi kuzungumza na kocha Phiri baada ya mazoezi.
    Dk Gembe alisema baada ya mazoezi kwamba hatarajii maumivu ya Tambwe kama yatakuwa makubwa na ana matumaini anaweza kuendelea na mazoezi kesho.
    Simba SC haijashinda mechi hata moja kati ya mbili ilizocheza katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ikitoa sare ya 2-2 na Coastal Union na 1-1 na Polisi Morogoro, zote Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Rais Aveva kulia akizungumza na kocha Phiri baada ya mazoezi

    Na Jumamosi, Wekundu hao wa Msimbazi watacheza Stand United ya Shinyanga, timu nyingine iliyopanda Ligi Kuu msimu huu kwa mara ya pili mfululizo baada ya sare na Polisi.
    Stand imekwishavuna pointi tatu katika Ligi Kuu, baada ya kuifunga 1-0 Mgambo JKT katika mchezo wake uliopita Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kufuatia kuanza ligi kwa kuchapwa 4-2 nyumbani na Ndanda iliyopanda nayo msimu huu. 
    Tayari Simba SC inamkosa mshambuliaji Mkenya, Paul Kiongera aliyeumia goti pia ambaye anatakiwa kuwa nje kwa wiki sita- hivi sasa akiwa amemaliza wiki mbili.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BALAA GANI HILI SIMBA SC, TAMBWE AUMIA MAZOEZINI LEO, HOFU YATAWALA…AVEVA NA PHIRI WOTE ‘VIROHO JUU’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top