• HABARI MPYA

    Wednesday, June 04, 2014

    TUMEWABAHATISHA ZIMBABWE, TUNAJIPANGAJE KWA MSUMBIJI?

    KIPA Deogratius Munishi ‘Dida’ alifungwa mabao mawili, lakini akachupia michomo ya hatari kama 10 na kuokoa katika mchezo ambao Tanzania ilitoka sare ya 2-2 na wenyeji Zimbabwe Jumapili Uwanja wa Taifa, Harare.
    Matokeo hayo yaliifanya Tanzania isonge mbele hatua ya mwisho ya kuwania kupangwa kwenye makundi ya kupigania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco kwa ushindi wa jumla wa 3-2, baada ya awali kushinda 1-0 nyumbani Dar es Salaam. 
    Zimbabwe, Worriers wana kila sababu ya kulaumiana kwa sare hiyo ya nyumbani, kwani walitawala mchezo na kufanya mashambulizi mengi, lakini wakakosa umakini au bahati katika kumalizia.

    Ni kama tu ilivyokuwa katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam, Zimbabwe pia walitengeneza nafasi nzuri kadhaa na wakakosa mabao mawili ya wazi, ambayo mabeki wa Stars waliokoa mipira iliyokuwa imekwishampita Tanzania One wetu wa leo, Dida na kuelekea kutinga nyavuni.
    Yote kwa yote, Tanzania sasa imetinga hatua ya mwisho ya mchujo na itamenyana na Msumbiji mwezi ujao, ambayo imeitoa Sudan Kusini, mechi yake kwanza ikichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Julai 19 na 20, wakati mechi ya marudiano itafanyika Msumbiji kati ya Agosti 2 na 3 mwaka huu.
    Unapoona unamaliza mchezo ukiwa umeshambuliwa zaidi na kukoswakoswa mabao mengi ya wazi maana yake ulielemewa na ungeweza kufungwa.
    Unapoona kipa wako anachupia michomo mingi ya hatari kuokoa na mabeki wake wanakuwa bize muda wote kudhibiti mashambulizi, maana yake ulizidiwa nguvu mchezoni.
    Unapoona timu yako inacheza mchezo wa ujanja ujanja, kuzuia zaidi na kushambulia kwa kuibia- maana yake bado haijiamini.  
    Unapoona timu yako inaongoza mabao 2-1 halafu inacheza kwa kupoteza muda, wachezaji wakijiangusha mara kwa mara na kufanya hila nyingi, maana yake hata ushindi wenyewe waliubahatisha, ndiyo maana wanaulinda.
    Na hiyo ndiyo hali halisi kwa timu yetu ya taifa kwa sasa, imefuzu mtihani mgumu sana kwa kuitoa Zimbabwe. Ilikuwa ni sawa na mwanafunzi wa shule ya msingi kupewa mtihani wa kidato cha Nne na akafanya vizuri. 
    Zimbabwe inashika nafasi ya 101katika msimamo wa viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), wakati Tanzania ni ya 127.
    Hii si mara ya kwanza Tanzania kuziangusha timu zilizo juu yake kiuwezo, huko nyuma tumekwishazifunga timu kibao zinazotuzidi uwezo, lakini bahati mbaya tunakuwa tunabahatisha na zaidi tunalewa na matokeo.
    Viongozi wanalewa, kadhalika na wachezaji na mashabiki pia, tukijiona kama tumefuzu Kombe la Dunia- huku tukisahau kabisa hali halisi kwamba tunatakiwa kutengeneza timu.
    Matokeo yake siku tukicheza nyuma ya bahati na kufungwa tunaigeuka timu yetu na kuichukia kabia, hata uwanjani hatuendi ikicheza tena.
    Ni mwaka jana tu, timu yetu ilivifunga vigogo kama Cameroon, Morocco na kusifiwa ilicheza vizuri dhidi ya Ivory Coast licha ya kufungwa mabao 3-2 Dar es Salaam.
    Lakini mwaka huo huo, tukafungwa nyumbani na Uganda 1-0 katika kuwania tiketi ya CHAN kabla ya kwenda kufungwa tena 3-1 katika mchezo wa marudiano Kampala.
    Baada ya hapo, Stars imekuwa ikicheza mechi zake katika mazingira magumu nyumbani, mashabiki hawajitokezi na hao wachache wanaojitokeza, wanakwenda kuzomea timu.
    Ukweli ni kwamba, miaka mingi tumekuwa tukicheza soka bila mpangilio, bora liende, ili mradi tuna ligi, ni wanachama wa CAF na FIFA, basi tunashiriki mashindano tu.
    Maandalizi tunayoyajua ni kuweka timu kambini, ifanye mazoezi baada ya hapo ikacheze mechi, lakini bado hatujawa na kile kitu kinaitwa maandalizi ya kisayansi.
    Zaidi ya hapo, sisi ni hodari wa kufukuza makocha kwa matokeo mabaya, bila kuzingatia hali halisi ya matokeo yenyewe.
    Mwisho wa siku, hata hao walimu wa kigeni tunaowaleta nchini, ukocha ni kazi yao inayowapatia riziki ya kuendesha maisha yao, kama watakuwa wanawasilisha programu na hazifanyiwi kazi, nao wanaamua kufanya kama viongozi wanavyotaka, bora liende, ili waingize siku.   
    Huyu kocha wa sasa, Mholanzi Mart Nooij amekuja nchini amepewa tu wachezaji, hakuwahi kuwaona kabla wakicheza, maana alifika tumekwishamaliza Ligi Kuu.
    Lakini kwa kuwaona mazoezini anajaribu kuenda nayo timu hivyo hivyo na hata ameweza kuiongoza kuitoa Zimbabwe. Ni mwalimu mzuri, anajiamini. 
    Baada ya mechi ya kwanza Stars ikipata ushindi mwembamba wa 1-0, Waandishi wa Habari waliuliza maswali ya kuonyesha wamekata tamaa, lakini aliwajibu kwa kujiamini na hatimaye amefanikiwa. 
    Inatakiwa Nooij baada ya kuwa na timu kwa takriban mwezi mmoja, kabla ya kuvaana na Msumbiji awe na kikao na TFF kujadili maandalizi ya timu, tena yawe maandalizi ya kisayansi.
    Wachezaji wetu wanakwenda majumbani kwao kupumzika baada ya kuitoa ZImbabwe, maana hatuna mashindano kwa sasa nchini, je wataingia kambini wiki mbili au moja kabla ya mechi wakitokea kwa wake zao na tukacheze na Msumbiji tupate matokeo mazuri?  
    Unaweza kuona kabisa baada ya kuitoa Zimbabwe kwa ‘bahati bahati’ tunapaswa kumshukuru Mungu na kuanza mapema maandalizi kwa ajili ya mtihani ufuatao, badala ya kujiona ‘sisi ndio sisi’ na kubweteka. Tutakataana kwa Msumbiji. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TUMEWABAHATISHA ZIMBABWE, TUNAJIPANGAJE KWA MSUMBIJI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top