• HABARI MPYA

  Jumamosi, Juni 28, 2014

  AVEVA AFUNGA KAMPENI KEMPINSKI NA KUSEMA; SIMBA ITASAJILI WAKALI KWELI NA SI ‘MARIJEKTI’

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MGOMBEA Urais wa Simba SC, Evans Elieza Aveva amefunga kampeni zake leo kwa kusema kwamba atahakikisha klabu hiyo inasajili wacheza wa kigeni, ambao wana ubora zaidi ya wachezaji wa nyumbani.
  Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari mchana wa leo hoteli ya Hyatt Regency, zamani Kilimanjaro Kempinski, Dar es Salaam, Aveva amesema kwamba  anataka Simba SC irejeshe makali yake.
  Aveva akizungumza wakati wa kufunga kampeni leo 

  Simba SC inatarajiwa kufanya uchaguzi wake Mkuu kesho kwenye ukumbi wa bwalo la maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam na leo Aveva alisindikizwa na memba wenzake wa kundi la Friends Of Simba (F.O.S.) kuhitimisha kampeni zake.
  “Mwaka 2003 wakati Simba SC inaitoa Zamalek ya Misri (wakiwa mabingwa wa Afrika), ilikuwa na mchezaji mmoja tu wa kigeni, Ramadhani Wasso. Sasa nikiingia madarakani, nitahakikisha mchezaji wa kigeni anayesajiliwa, anakuwa na uwezo wa juu kuliko wachezaji wa Tanzania,”amesema Aveva.
  Membaz wa F.O.S
  Hans Poppe akizungumza 

  Mwenyekiti wa zamani wa F.O.S., Salim Abdallah ‘Try Again’ alianza kumuelezea Aveva kama kiongozi anayefaa na ambaye atarejesha heshima ya Simba SC.
  Salim alisema kuwa Aveva ndiyo tumaini jipya ndani ya klabu hiyo ya Wekundu wa Msimbazi.
  Mwenyekiti wa sasa wa F.O.S., Zacharia Hans Poppe akafuatia akielezea maana na dhana halisi ya kundi hilo, kwamba ni wakereketwa haswa wa klabu hiyo na ambao kiu yao ni kuona klabu inafanya vizuri.
  Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Simba SC, Hassan Dalala naye akazungumza akimwagia sifa Aveva kwamba atarejesha umoja na kuleta mafanikio ya ndani na nje ya Uwanja.
  Lakini pia, Dalali akasema huyo ndiye kiongozi ambaye atawafanya wapinani wao wa jadi, Yanga SC wawe wanalala mapema.   
  Katika uchaguzi huo kesho, Aveva anatarajiwa kuchuana na Andrew Peter Tupa baada ya Michael Richard Wambura kuenguliwa kwa kukiuka kanuni za uchaguzi, baada ya kukutwa na hatia ya kufanya kampeni kabla ya muda.
  Kwa mujibu wa  Kamati ya Uchaguzi iliyoko chini ya Dokta, Damas Ndumbaro,  wanachama wa Simba wanatakiwa kufika katika ukumbi huo wa uchaguzi  huo kuanzia saa moja asubuhi ili kuanza zoezi la kuhakiki kadi zao. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AVEVA AFUNGA KAMPENI KEMPINSKI NA KUSEMA; SIMBA ITASAJILI WAKALI KWELI NA SI ‘MARIJEKTI’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top