• HABARI MPYA

  Ijumaa, Juni 27, 2014

  MAHAKAMU KUU YAGOMA KUZUIA UCHAGUZI SIMBA SC, NGOMA JUMAPILI KAMA KAWAIDA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  UCHAGUZI Mkuu wa Simba SC utafanyika kama ilivyopangwa Jumapili wiki ya Juni 29, 2014, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeamua.
  Mahakamhiyo, imekataa kuzuia Uchaguzi Mkuu wa Simba kwa sababu maombi ya wanachama wa Simba yaliwasilishwa kabla ya muda.
  Uamuzi huo umetolewa leo na Jaji Augustine Mwarija baada ya mvutano mkali wa kisheria uliotokea mahakamani hapo wakati pande mbili zilizokuwa zinapingana kuungana katika hoja.
  Wanachama wa Simba SC watachua viongozi wapya Jumapili Dar es Salaam

  “Mahakama inakubali wanachama kufungua kesi, inakataa kuzuia uchaguzi wa Simba kwa sababu hakuna kesi ya msingi ya madai iliyowasilishwa mahakamani hivyo ombi la zuio lililetwa kabla ya muda.
  “Kutokana na hoja hiyo mahakama inayatupilia mbali maombi ya kuzuia uchaguzi wa Simba unaotarajiwa kufanyika Jumapili,”alisema Jaji Mwarija.
  Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo Wakili wa Rais wa Simba, Aden Rage na Bodi ya wadhamini, Juma Nassoro alidai kasikitishwa na uamuzi wa mahakama kwani makubaliano yao ya kutaka uchaguzi uzuiwe yalikuwa yakilenga kuona klabu ya Simba inakuwa na amani.
  “Katika suala la uchaguzi kwa sasa, uongozi wa Simba ndio utakaokuwa na mamlaka ya kuamua uendelee au hapana, hilo liko mikononi mwa Simba,”alidai Nassoro.
  Kabla ya kufikia uamuzi huo mapema asubuhi walipoingia mahakamani, Wakili Nassoro aliiambia mahakama kwamba baada ya kupokea hati ya kuitwa mahakamani walishauriana na mteja wake Rage pamoja na Baraza la Wadhamini na kukubaliana kwamba wanaunga mkono maombi ya kuzuia uchaguzi.
  “Sisi tunaomba tupate zuio, maombi hayo hatuyapingi kwa sababu tunaona ndio amri inayoweza kuepusha shari inayoweza kutokea.
  “Tumefanya maridhiano pande zote mbili tumekubaliana kulizungumza suala hili nje ya mahakama, wagombea walioondolewa katika uchaguzi warejeshwe kugombea pamoja na kuendelea kufanya kampeni,”alidai Nassoro.
  Wakili wa walalamikaji alidai kwamba wasioruhusiwa kugombea ni wale wasiofikia kiwango cha elimu hivyo walikubaliana kuondoa maombi yao mahakamani.
  Makubaliano hayo waliyaweka kwa maandishi na kuyawasilisha mahakamani huku wakipendekeza kusogeza uchaguzi hadi Julai 13 mwaka huu.
  Kutokana na uamuzi huo wa mahakama matakwa ya pande mbili zilizoungana hayakufikiwa baada ya Jaji Mwarija kuzikaa hoja zao kwa madai kwamba hazikuwepo katika maombi yaliyopo mahakamani na zuio haliwezi kutolewa kwa sababu hakukuwa na madai ya msingi yaliyowasilishwa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MAHAKAMU KUU YAGOMA KUZUIA UCHAGUZI SIMBA SC, NGOMA JUMAPILI KAMA KAWAIDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top