• HABARI MPYA

  Jumamosi, Juni 28, 2014

  MASIKINI NGASSA, YANGA YAMKOSESHA ULAJI HIVI HIVI, FREE STATE YASITISHA MPANGO WA KUMNUNUA BAADA YA KUTAJIWA DAU KUBWA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Free State Stars ya Afrika Kusini imeachana na mpango wa kumnunua mshambuliaji Mrisho Khalfan Ngassa, baada ya kutajiwa dau kubwa na klabu yake, Yanga SC.
  Free State ilikuwa tayari kutoa dola za Kimarekani 80,000 kiasi cha Sh. Milioni 130 za Tanzania, lakini Yanga SC ikataka dola 150,000 zaidi ya Sh. Milioni 240,000.
  Pamoja na kwamba Ngassa aliyebakiza Mkataba wa mwaka mmoja Yanga SC alikwishafuzu vipimo vya afya katika klabu hiyo, lakini Free State inamrudisha Tanzania.
  Ngassa amesikitishwa na hali hiyo, lakini amesmhukuru Mungu na amesema anarudi nyumbani kwa roho safi, akiamini haikuwa ‘riziki’ yake.
  Kila kitu ilikuwa safi; Ngassa alikwishafaulu hadi vipimo vya afya, lakini Free State imeshindwa dau la Yanga SC

  “Yanga ndiyo wameshika kisu kwenye makali, na mimi ninaheshimu Mkataba wangu, narudi nyumbani, roho imeniuma sana, kwa sababu huku nilikuwa napewa maslahi mazuri na pia kucheza katika mazingira mazuri,”amesema Ngassa alipozungumza na BIN ZUBEIRY kutoka Afrika Kusini leo.  
  Hata hivyo, Ngassa amesema hatakata tamaa, anarudi nyumbani kucheza kwa bidii ili aendelee kuwa katika kiwango cha juu, labda siku moja atatimiza ndoto za kucheza nje.
  Ngassa alifuzu majaribio baada ya siku moja tu katika klabu ya Free State Stars ya Afrika Kusini, ambayo ilikuwa tayari kabisa kumnunua.
  Ngassa aliondoka mwanzoni mwa wiki hii Dar es Salaam na baada ya kufanya mazoezi na klabu hiyo mara moja, akakubalika.
  Ngassa alikwenda mwenyewe Afrika Kusini kwa gharama zake baada ya kuambiwa klabu hiyo inatafuta winga.
  Free State tayari imemuajiri kocha wa zamani wa Yanga SC, Mbelgiji, Tom Saintfiet. 
  Ngassa alishindwa kwenda na timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kambini Botswana kwa ajili ya mpango huo wa kuhamia Afrika Kusini.
  Stars iliondoka katikati ya wiki kwa ndege ya shirika la Afrika Kusini kwenda Gaborone, Botswana ambapo kitapiga kambi ya wiki mbili.
  Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imeweka kambi hiyo chini ya Kocha Mart Nooij ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi yake ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika (AFCON) dhidi ya Msumbiji (Mambas) itakayochezwa Julai 20 mwaka huu Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
  Mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi kutoka Misri wakiongozwa na Mahmoud Ashor wakati Kamishna atakuwa Felix Tangawarima kutoka Zimbabwe.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MASIKINI NGASSA, YANGA YAMKOSESHA ULAJI HIVI HIVI, FREE STATE YASITISHA MPANGO WA KUMNUNUA BAADA YA KUTAJIWA DAU KUBWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top