• HABARI MPYA

    Saturday, June 21, 2014

    TFF YABARIKI RASMI UCHAGUZI SIMBA SC BILA YA ‘KOMREDI’ MICHAEL RICHARD WAMBURA

    Na Waandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) baada ya kupokea na kuzingatia maombi ya Simba (barua imeambatanishwa), na kwa kuzingatia Ibara ya 26 ya Kanuni za Uchaguzi za TFF toleo la 2013 limeiruhusu klabu hiyo kuendelea na mchakato wa uchaguzi wao uliopangwa kufanyika Juni 29 mwaka huu.
    Taarifa ya TFF iliyotumwa leo imesema kwamba inawahimiza wanachama wa klabu ya Simba kuwa watulivu na wafanye uchaguzi wao kwa amani.
    Ikumbukwe TFF ilisimamisha mchakato wa uchaguzi wa Simba SC hadi hapo klabu hiyo itakapounda Kamati ya Maadili ambayo itasikiliza masuala ya kimaadili kuelekea uchaguzi huo.
    Katiba ndiyo kila kitu; Rais wa TFF, Jamal Malinzi akiwa ameshika Katiba ya TFF. Kiongozi huyo ameruhusu uchaguzi wa Simba SC uendelee

    Malinzi alisema mwishoni mwa wiki kwamba Simba SC inatakiwa kuwa imekwishaunda Kamati ya Maadili hadi kufika Juni 30, mwaka huu, hatua ambayo alidai imefuatia TFF kupokea malalamiko mengi juu ya ukiukwaji wa maadili kwa baadhi ya wagombea na wanachama wa klabu hiyo.
    Malinzi alisema kwamba baada ya kuundwa kwa Kamati hiyo Maadili itasikiliza malalamiko yote ya kimaadili yanayougubika mchakato wa udhaguzi huo, ambao ulipangwa kufanyika Juni 29, mwaka huu.
    Aliagiza Kamati ya Utendaji ya Simba SC iliyopo madarakani chini ya Mwenyeiiti wake, Rage iendelea kuiongoza klabu hiyo hadi hapo mchakato wa uchaguzi utakapokamilika.    
    Lakini mwanzoni mwa wiki, Kamati ya Uchaguzi ya Simba SC ilimpinga Malinzi, ikisema TFF haina mamlaka ya kusimamisha uchaguzi huo na Jumanne, Rage akamuomba raisi huyo wa TFF aache mchakato wa zoezi hilo uendelee kwa manufaa ya Simba SC.
    Juzi Kamati ya Rufani ya TFF iliitupilia mbali rufaa ya Michael Wambura kupinga kuenguliwa kugombea urais katika uchaguzi wa klabu ya Simba unaotarajiwa kufanyika baadaye mwezi huu.
    Wambura aliwasilisha rufani yake mbele ya Kamati hiyo iliyokutana siku hoyo (Juni 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam chini ya Kaimu Mwenyekiti Wakili Mwita Waissaka kupinga uamuzi wa kumwengua katika kinyang’anyiro hicho uliofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya Simba kwa kufanya kampeni kabla ya muda uliopangwa.
    Baada ya kupitia vielelezo, kanuni na sheria, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF imeridhika kuwa mrufani (Michael Wambura) alifanya kampeni kabla ya muda kinyume na Ibara ya 6(1)(a) na (g), Ibara ya 6(1)(l) pamoja na Ibara ya 14(3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF toleo la 2013.
    Kwa mujibu wa ibara hizo, Kamati ya Uchaguzi ya Simba inayo mamlaka ya kumwengua (disqualify) mgombea anayefanya kampeni ama kukiuka maagizo halali ya Kamati ya Uchaguzi.
    Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF imeziagiza kamati zote za uchaguzi za wanachama wa TFF kufuata kanuni za uchaguzi kama zilivyoainishwa katika Katiba zao ili kuepusha rufani za mara kwa mara.
    Uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF umezingatia Katiba ya TFF pamoja na kanuni zake, na pia Katiba ya Simba na kwa taarifa ya leo ya shirikisho hilo, Simba SC wanarudi rasmi kukimbizana na muda kuawahi uchaguzi wao.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YABARIKI RASMI UCHAGUZI SIMBA SC BILA YA ‘KOMREDI’ MICHAEL RICHARD WAMBURA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top