• HABARI MPYA

    Wednesday, June 25, 2014

    WAFUASI WA WAMBURA WAMEENDA MAHAKAMANI KUZUIA UCHAGUZI SIMBA SC, SIYO MPANGO WAKE HUU KWELI?

    WAKATI Michael Richard Wambura anajitokeza kuchukua fomu za kugombea Urais wa Simba SC, alisindikizwa na kundi la wanachama wa klabu hiyo, wakiwemo wale maarufu na wa siku nyngi.
    Waliingia makao makuu ya klabu hiyo, Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam kwa maandamano yaliyopambwa na shangwe kuchukua fomu.
    Sura zile zile za watu wale wale waliomsindikiza Wambura kuchukua fomu, zikajitokeza tena kumsindikiza mgombea huyo kurejesha fomu.

    Sura zile zile zikamsindikiza tena mgombea huyo, kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo kumuengua Wambura.
    Ikumbukwe Wambura alienguliwa na Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti Wakili Dk Damas Daniel Ndumbaro kwa tuhuma kwamba si mwanachama halali.
    Hata hivyo, Wambura alikata rufaa Kamati ya Rufani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya Mwenyekiti Wakili Julius Lugaziya akashinda na kurejeshwa.
    Kamati ya Uchaguzi ya Simba SC ikamuengua tena Wambura kwa kosa la kutumia maneno ambayo yalionekana kuwa ya kikampeni kabla ya muda, wakati akizungumzia uamuzi wa Jaji Lugaziya kumrejesha kugombea.
    ‘Kidume’ akakata tena rufaa, lakini safari hiyo akakwama na hivyo kuenguliwa moja kwa moja katika mbio za Urais wa Simba SC Juni 29, mwaka huu, akiwaacha Evans Elieza Aveva akichuana na Andrew Peter Tupa.
    Mara baada ya uamuzi huo, sura zile zile za watu wale wale ambao wamekuwa bega kwa na Wambura tangu anachukua fomu, anarudisha, anapinga kuenguliwa na harakati nyingine zote, zikaibuka na hoja ya kwenda Mahakama Kuu kuzuia uchaguzi huo.
    Kisa nini? Wanadai Kamati ya Uchaguzi imekiuka baadhi ya mambo ya kikatiba katika mchakato huo.
    Tayari wamekwishafika Mahakama Kuu na kesi yao ipo katika mlolongo wa kusikilizwa.
    Kwa hoja zao na hali halisi ya zoezi hilo chini ya Kamati ya Ndumbaro, hawawezi kushinda, labda wawe na hoja nyingine.
    Lakini tu wasiwasi ni kwamba, iwapo kesi hiyo haitatupwa ina maana Uchaguzi wa Simba SC hauwezi kufanyika Juni 29 kama ilivyopangwa, bali hadi hapo kesi hiyo itakapomalizika.
    Hili litawaumiza sana wana Simba SC walio wengi, ambao kwa sasa wanataka tu uchaguzi, klabu yao ipate viongozi wapya na kuingia katika zama mpya baada ya kipindi kigumu cha miaka takriban mitatu iliyopita. 
    Wakati wa harakati za kufungua kesi, wanachama wote waliokuwa na Wambura bega kwa bega walikuwepo nje ya Mahakama Kuu barabara ya Kivukoni na wakazungumza na vyombo vya habari juu ya msimamo wao, wazi wakionekana kumtetea Wambura.
    Kwa sasa, Wambura anakabiliwa na pingamizi juu ya uanachama wake, baada ya yeye mwenyewe kuipeleka klabu hiyo mahakamani wakati wa uchaguzi uliouweka madarakani uongozi unaomaliza muda wake chini ya Alhaj Ismail Aden Rage miaka minne iliyopita.
    Hata wakati Wakili Lugaziya anamrejesha Wambura mara ya kwanza kugombea Simba SC, hakukataa kama aliipeleka klabu hiyo mahakamani, bali alisema kuna makosa yaliyofanyika- kwamba baada ya kosa hilo, akaruhusiwa kuendelea kulipia kadi ya uanachama wake kushiriki mikutano na hata kuteuliwa katika Kamati ya Utendaji.
    Ina maana kwa mlolongo huo, pamoja na kosa alilofanya, lakini kama ameendelea kushiriki shughuli za klabu kama mwanachama halali, huwezi kumzuia kugombea.
    Lakini kosa lipo pale pale. Kumbukumbu zipo, Wambura alipeleka masuala ya soka mahakamani, jambo ambalo FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa) inakataza.
    FIFA imejiwekea utaratibu wa kusuluhisha masuala yote ya mpira wa miguu ndani ya mfumo wake- mtu anapopeleka kesi za soka kwenye mahakama za dola anakuwa amefanya kosa.
    Wafuasi wa Wambura wanakwenda mahakamani, wakati  yeye mwenyewe amekaa kimya na hajakemea hilo- maana yake anafurahia kwa sababu wale ni watu wake.
    Na kwa mazingira halisi na historia yao, huwezi kusita kuhisi labda watu hao wametumwa na Wambura huyo huyo- kwa sababu labda ameogopa kurudia yeye mwenyewe kufanya kosa la kuipeleka klabu mahakamani.
    Na kwa nini unaweza kuhisi wametumwa na Wambura? Siku ya kwanza kabisa Wambura anakwenda kuchukua fomu nani aliwaambia wale jamaa hadi wakaenda kumsindikiza kwa maandamano. Ulikuwa mpango.
    Na wakati anakwenda kurudisha fomu, muda na siku ya kurudisha fomu yake, nani aliwaambia wale jamaani kama siyo yeye mwenyewe? Ulikuwa ni mpango.
    Na wakati anakwenda kupinga kuenguliwa kugombea na Kamati ya Ndumbaro, nani aliwaambia wale jamaa wakenda klabu hadi kufunga ofisi kama si yeye mwenyewe? Ulikuwa ni mpango.
    Na hata sasa, hawa jamaa wanakwenda mahakamani, nani kawatuma kama si yeye mwenyewe? Utakuwa ni mpango. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WAFUASI WA WAMBURA WAMEENDA MAHAKAMANI KUZUIA UCHAGUZI SIMBA SC, SIYO MPANGO WAKE HUU KWELI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top