• HABARI MPYA

    Saturday, June 28, 2014

    MIKWARA YA KUSAJILI WACHEZAJI NA MABURUNGUTU YA ‘HELA’ MEZANI IMEISHIWA WAPI?

    Na Michael Maurus, DAR ES SALAAM
    MCHAKATO wa usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, umeanza kwa mbwembwe ambapo klabu kadhaa zimeanza kuanika majina ya walioingia nao mikataba.
    Tayari klabu za Simba, Yanga, Azam na nyinginezo za Ligi Kuu Bara zimeshaanza kutangaza kuingia mikataba na wachezaji kwa ajili ya msimu ujao unaotarajiwa kuanza Septemba mwaka huu.
    Kwa kawaida, kipindi hiki cha usajili huwa kinatawaliwa na mbwembwe za kila aina, kwa viongozi wa klabu, hasa za Simba na Yanga, kuonyeshana ubabe katika suala zima la usajili.
    Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa ya Yanga SC, Seif Ahmed 'Magari' kulia akimsainisha beki Kevin Yondan kutoka Simba SC miaka miwili iliyopita mjini Dar es Salaam na chini ni viongozi wa Simba SC wakimsainisha kaka wa kiungo Amri Kiemba.

    Leo unaweza kuona picha ya kiongozi wa Simba akiwa amepiga picha akimsainisha mkataba mchezaji, huku mezani yakionekana mabunda ya fedha, kesho ikiwa hivyo kwa upande wa Yanga.
    Hilo lilifanyika ili tu kila upande kuonyesha jeuri yao ya fedha, lakini pia kuuthibitishia umma wa wapenda soka nchini kuwa ni kweli wamemsajili mchezaji husika.
    Kila mpenzi wa soka hapa nchini, ni shahidi wa hilo kwani wapo wachezaji wengi waliosainishwa mikataba na viongozi wa Simba na Yanga, huku mabunda ya noti yakiwa mezani.
    Tofauti na misimu iliyopita, safari hii kumekuwa na mabadiliko katika suala zima la usainishaji mikataba kwa wachezaji, ambapo mtindo wa kufanya hivyo, huku mabunda ya noti yakiwa mezani, umepotea.
    Ndani ya wiki hizi mbili, Yanga imetangaza kuwasainisha mikataba wachezaji wawili ambao ni beki Pato Ngonyani, kiungo mkabaji Said Juma na Saleh Abdallah.
    Binafsi sijashuhudia picha yoyote inayoonyesha kiongozi wa klabu hiyo akiwasainisha wachezaji hao tofauti na ilivyokuwa misimu iliyopita.
    Lakini Simba wao wameanika hadharani picha zinazoonyesha wakiwasainisha mikataba wachezaji wao. Miongoni mwa wachezaji walioonyeshwa katika picha wakisainishwa mikataba na viongozi wa Simba, ni Joram Mgeveke na Mohammed Hussein ‘Shabalala’.
    Nimekuwa nikijiuliza kulikoni safari hii wanasoka wanasajiliwa bila kuonyeshwa kwa mabunda ya noti mezani, hatimaye nikapata jibu. Azam FC ndiyo klabu iliyozitoa ‘tongotongo’ Simba na Yanga katika hilo.
    Klabu hiyo ya Azam, imeendelea kuwa mfano wa kuigwa na klabu za soka hapa nchini kutokana na utaratibu wao wa kuendesha shughuli za soka ‘kiprofesheno’.
    Japo imeanza kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2008/09, ilijikuta ikizitoa jasho timu zinazoitwa vigogo wa soka ya Tanzania, baada ya msimu wa 2011/12 kumaliza ligi ikiwa nafasi ya pili na hivyo kufuzu kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho mwaka 2013 kama ilivyokuwa msimu uliofuata wa 2013/14.
     Ni kuanzia wakati huo, Azam sasa imekuwa mmoja ya klabu kubwa hapa nchini, japo wengine wamefika mbali zaidi kwa kudai hiyo ndiyo klabu inayostahili jina hilo, Simba na Yanga zikibaki na jina lao la ukongwe pekee.
    Moja ya mambo yanayoifanya Azam kupewa heshima kiasi cha kutakiwa kuwa mfano wa kuigwa na klabu nyinginezo hapa nchini, zaidi ikiwa ni Simba na Yanga, ni kitendo chake cha kuwekeza vilivyo katika soka kwa kujenga viwanja wa na viwanja, mmoja ukiwa tayari umeshaanza kutumika ukiwa katika hadhi ya kimataifa.
    Lakini pia, klabu hiyo imewekeza vilivyo katika soka ya vijana, ikiwa na makundi ya vijana wa umri mbalimbali, pamoja na kuwa na vifaa karibu vyote vinavyotakiwa kuwapo katika klabu yoyote ya soka.
    Na katika suala zima la usajili, Azam FC imeonekana kuwa kiooo kwa klabu za Simba na Yanga kutokana na kuufanya mchakato huo ‘kiprofesheno’ tofauti na ilivyo kwa wenzao hao.
    Katika kumbukumbu yangu, hata siku moja sijawahi kuwaona viongozi wa Azam wakisajili mchezaji huku mezani wameweka mabunda ya noti.
    Wanachofanya ‘matajiri’ hao wa soka ya Tanzania, mara baada ya kukubaliana na mchezaji, fedha zake humwekea benki na kwamba siku ya kusaini mkataba, kinachofanyika ni kukabidhiwa jezi tu na kupeana naye mikono ya pongezi baada ya kufanikisha tukio hilo.
    Azam FC iliwanasa Frank Domayo na Mbuyu Twite kutoka Yanga, lakini walionyesha picha ambazo wachezaji hao walikuwa wakisaini mikataba na wala hatukuona mabunda ya noti mezani. Jiulize ingekuwa ni Simba au Yanga ingekuwaje hasa kwa Domayo?
    Viongozi wa Simba na Yanga wanaonekana kuelewa somo hilo la Azam FC katika suala zima la usajili wa wachezaji kwa kutoanika mezani mabunda ya noti za usajili wa mchezaji husika na badala yake kumalizana naye faragha kama ilivyo Ulaya na kwingineko.
    Tumeliona hilo kwa Simba ambao hivi karibuni tumeona picha wakiwasainisha baadhi ya wachezaji wao bila kuwapo kwa mabunda ya noti mezani. Bila shaka huo ni mwanzo tu wa viongozi wa klabu zetu nchini, hasa Simba na Yanga kuendesha shughuli zao ‘kiprofesheno’ bila kujali kama kuwakifanya jambo fulani wataonekana wameiiga klabu nyingine.
    Mwisho wa siku, wapenzi wa klabu zetu na wengineo hapa nchini, watataka kuona timu zao zikifanya kweli kwenye michuano mbalimbali na si miburungutu ya noti walizipewa wachezaji wao.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MIKWARA YA KUSAJILI WACHEZAJI NA MABURUNGUTU YA ‘HELA’ MEZANI IMEISHIWA WAPI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top