• HABARI MPYA

  Jumatano, Juni 25, 2014

  KOCHA WA ZAMANI YANGA ATUA AFRIKA KUSINI KUPIGA KAZI TIMU YA NGASSA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  ALIYEWAHI kuwa kocha wa Yanga SC, Mbelgiji Tom Saintfiet ametua klabu ya Free State Stars ya Afrika Kusini ambayo iko mbioni kumsajili mshambuliaji Mrisho Khalfan Ngassa.
  Tom alitua Yanga SC Julai mwaka 2012, na mara moja akaiwezesha kutwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
  Hata hivyo, baadaye baada ya kulalamikia utendaji wa viongozi wa Yanga na kutojali kuhusu timu ikiwemo malazi na huduma bora wakati wa mechi za mikoani, akasitishiwa mkataba akidaiwa ameonyesha utovu wa nidhamu Septemba.
  Tom Saintfiet kushoto akiwa na Mtendaji Mkuu wa BIN ZUBEIRY Blog, Mahmoud Zubeiry kulia

  Baada ya hapo alikwenda timu ya taifa ya Yemen alikofanya kwa muda kabla ya kuchukuliwa na timu ya taifa ya Malawi alikoacha kazi baada ya miezi miwili kutokana na kutoridishwa na mazingira.
  Tom aliyezaliwa Machi 29, mwaka 1973 mjini Mol, Ubelgiji ambaye awali alizifundisha timu za madaraja ya chini humo, enzi zake pia alicheza soka katika nafasi ya kiungo klabu za K.V.C. Westerlo, K.F.C. Lommel S.K na K.F.C. Verbroedering Geel za kwao, ingawa alilazimika kuacha mapema baada ya kuumia.
  Klabu alizofundisha mbali na Yanga ni F.C. Satelitte Abidjan, B71 Sandur, Stormvogels Telstar, Al-Gharafa, BV Cloppenburg, FC Emmen na Shabab Al-Ordon.
  Amefundisha pia timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 ya Qatar, timu za wakubwa za Namibia, Zimbabwe, Ethiopia mbali na Yemen na Malawi.
  Hata hivyo, Saintfiet hakuwahi kufanya kazi na Ngassa, kwani wakati Mbelgiji huyo akiwa Yanga SC, Ngassa alikuwa anachezea Azam FC.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KOCHA WA ZAMANI YANGA ATUA AFRIKA KUSINI KUPIGA KAZI TIMU YA NGASSA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top