• HABARI MPYA

  Ijumaa, Juni 27, 2014

  AMINA POYO APANIA KUFANYA MAKUBWA AKICHAGULIWA SIMBA SC

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  SERA za maendeleo ya klabu ndiyo nyumbani kwake- chochote anachozungumza Amina Hussein Poyo ni juu ya kuleta maafanikio ndani ya klabu ya Simba ya Dar es Salaam.
  Mgombea huyo wa nafasi ya Ujumbe upande wa wanawake, miongoni mwa anayotaka kufanya ni kuifufua timu ya wanawake ya Simba SC, maarufu kama Simba Queens ili iweze kuwa tishio za kuzalisha vipaji.
  “Itapendeza tunakuwa na timu imara ya Simba Queens, inafanya vizuri kwenye mashindano, tunatoa wachezaji wa timu ya taifa na hata ikibidi kuuza wengine nje, hii itaiongezea umaarufu klabu,”anasema katika mahojiano na BIN ZUBEIRY.
  Chagua huyu mama; Amina Poyo ni Simba damu na anatokea familia ya Simba SC tangu enzi za Sunderland

  Lakini Simba Queens si mwisho wa fikra za Amina, bali pia amesema atatumia nafasi yake kama Mjumbe wa Kamati ya Utendaji kushawishi harakati za maendeleo ndani ya klabu kwa ujumla.
  “Tunataka mafanikio ya uwanjani, kushinda mataji kuanzia ya nyumbani na ya kimataifa. Mimi watu wa Simba wananijua kwa takriban miaka nane iliyopita nimekuwa mstari wa mbele kusaidia na kuhamasisha timu ifanye vizuri.
  Ninakwenda hadi kambini ninafanya kazi za timu kwa kujitolea kwa mapenzi yangu, nasafari ndani na nje ya nchi, kwa kweli katika hilo nitafanya zaidi kwa sababu furaha ya kwanza ya wapenzi wa timu ni ushindi wa uwanjani,”anasema.
  Amina pia anasema anapenda kuiona Simba SC inakuwa klabu yenye mafanikio ya nje ya uwanja pia kwa kujinufaisha na ukubwa wa jina lake na umaarufu wake kwa kutumia nembo ya klabu kuingiza fedha.
  “Hapo namaanisha vitu vingi sana, tunaweza kuuza jezi, fulana, kofia, kanga na vikorokoro vingine vyenye nembo ya Simba SC na tukapata fedha nyingi tu kuisaidia klabu,”anasema.
  Amina anasema kwamba atajitolea zaidi kushawishi makampuni mbalimbali yajitokeze kuidhamini timu, akiamini hali ya kiuchumi itakapokuwa nzuri zaidi ndani ya klabu na mambo yatakwenda vizuri.
  Kujenga umoja ndani ya klabu na kuondoa makundi na matabata na kuleta maana halisi ya Simba SC “Nguvu Moja” ndiyo ndoto nyingine za Amina Poyo.
  Amina anasema kwamba akichaguliwa ndani ya Kamati ya Utendaji ya Simba SC, atahamasisha mradi wa ujenzi wa Uwanja wa klabu hiyo eneo la Bunju, Dar es Salaam ukamilishwe.
  Amina Hussein Poyo aliyezaliwa Sikonge mkoani Tabora Julai 11, mwaka 1967 ni mwanachama wa Simba SC tangu mwaka 2008, lakini alianza kuipenda klabu hiyo tangu mdogo kwa sababu anatokea familia ya Simba tangu enzi za Sunderland.
  Baba yake marehemu Mikidadi Maruzuku alikuwa mwanachama na mkereketwa maarufu wa Simba SC mjini Mwanza. Amina tayari  ana uzoefu wa kuongoza, hivi sasa akiwa Mwenyekiti wa tawi la Simba la Platinum Saporters. “Chagua Amina Poyo kwa maendeleo ya Simba SC,”anamalizia mwanamama huyo katika mahojiano na BIN ZUBEIRY jana Kigamboni, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AMINA POYO APANIA KUFANYA MAKUBWA AKICHAGULIWA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top