• HABARI MPYA

  Jumanne, Juni 24, 2014

  NGASSA AULA AFRIKA KUSINI, FREE STATE STARS WAFIKA BEI, WAHAHA KUMNG’OA YANGA SC

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa Yanga SC, Mrisho Khlafan Ngassa amefuzu majaribio baada ya siku moja tu katika klabu ya Free State Stars ya Afrika Kusini, ambayo sasa inafanya utaratibu wa kumnunua.
  Ngassa aliondoka jana asubuhi Dar es Salaam na jioni ya jana akafanya mazoezi na klabu hiyo na moja kwa moja akakubalika.
  BIN ZUBEIRY inafahamu hivi sasa Free State Stars imeanza mawasiliano na uongozi wa Yanga juu kumnunua mchezaji huyo hodari.
  Mrisho Ngassa yuko mbioni kujiunga na Free State Stars ya Afrika Kusini

  Akizungumza kutoka Afrika Kusini leo, Ngassa amesema; “Nilidhani yatakuwa majaribio ya muda mrefu, lakini nimefika tu baada ya kufanya nao mazoezi mara moja, wakasema wewe si wa kujaribiwa, umekuja hapa kusajiliwa,”amesema Ngassa.
  Ngassa alikwenda mwenyewe Afrika Kusini kwa gharama zake baada ya kuambiwa klabu hiyo inatafuta winga.
  “Kuna rafiki yangu aliniambia hii timu inatafuta winga, akaniambia ananiunganishia mpango wa kwenda majaribio na nijiamini nitafuzu, nikakubali nimekuja na mambo safi,”alisema.
  Ngassa amesema kwamba kwa sasa Free State wanawasiliana na Yanga SC juu ya mpango wa kumhamishia huko. “Naipenda sana Yanga, nimecheza pale kwa moyo wangu wote, lakini naomba tu wawe wepesi kuniruhusu kuja kujiendeleza huku,”amesema.     
  Free State imetuma barua Yanga SC kutoa ofa ya bei wanayotaka kumnunua Ngassa na sasa inasubiri majibu kwa ajili ya hatua zaidi.
  Ngassa ameshindwa kwenda na timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kambini Botswana kwa ajili ya mpango huo wa kuhamia Afrika Kusini.
  Stars imeondoka alfajiri ya leo kwa ndege ya shirika la Afrika Kusini kwenda Gaborone, Botswana ambapo kitapiga kambi ya wiki mbili.
  Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imeweka kambi hiyo chini ya Kocha Mart Nooij ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi yake ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika (AFCON) dhidi ya Msumbiji (Mambas) itakayochezwa Julai 20 mwaka huu Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
  Mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi kutoka Misri wakiongozwa na Mahmoud Ashor wakati Kamishna atakuwa Felix Tangawarima kutoka Zimbabwe.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NGASSA AULA AFRIKA KUSINI, FREE STATE STARS WAFIKA BEI, WAHAHA KUMNG’OA YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top