• HABARI MPYA

  Jumatatu, Juni 30, 2014

  FREE STATE YAIONGEZA DAU YANGA SC ILI KUMSAJILI NGASSA, MALINZI ASIKITIKA AFRIKA KUSINI, SAINTFIET ASEMA MRISHO ATATISHA PSL

  Na Mahmoud Zubeiry, BETHLEHEM
  KLABU ya Free State Stars ya Afrika Kusini itaongeza ofa yake kidogo katika jitihada za kujaribu kumnunua mshambuliaji Mrisho Khalfan Ngassa, baada ya Yanga SC kukataa ofa ya awali ya dola za Kimarekani 80,000 zaidi ya Sh. Milioni 130.
  Ngassa tayari yuko hapa Bethlehem akifanya mazoezi na timu hiyo ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini, iliyomuajiri kocha wa zamani wa Yanga SC, Mbelgiji, Tom Saintfiet. 
  Yanga SC iliiambia Free State inataka dola 150,000 zaidi ya Sh. Milioni 240 kwa ajili ya kumuuza mchezaji huyo wa kimataifa wa Tanzania na awali, klabu hiyo iliamua kusitisha mpango huo.
  Mrisho Ngassa akifanya vitu vyake kwenye mazoezi ya Free State Stars jioni ya leo Uwanja wa Beigedia J.D. Potgieter mjini Bethlehem, Afrika Kusini leo.

  Lakini kwa shinikizo la kocha Saintfiet, Free State imeamua kujaribu bahati yake kwa mara ya mwisho, ikisema itaongeza kidogo ofa yake kutoka dola 80,000 kwa ajili ya mchezaji huyo anayemaliza Mkataba wake Jangwani Mei mwakani.  
  Ngassa mwenyewe ameonyesha nia ya kubaki Afrika Kusini na tangu ameambiwa dili la kuhamia PSL limeshindikana amekuwa hana raha.   
  Mapema leo, BIN ZUBEIRY ilikutana na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa O R Tambo mjini Johannesburg, Afrika Kusini ambaye alisikitishwa na suala la mchezaji huyo kupata timu, lakini anashindwa kujiunga nayo.
  “Hii inasikitisha, vijana wanapata nafasi za kucheza nchi zilizoendelea kisoka, watu wanawarubuni kwa magari na fedha nyingi warudi nyumbani, inafikia wakati wachezaji wengine wanabadilisha uraia ili wacheze nje, taifa linapoteza,”alisema Malinzi.
  Malinzi hakuweza kuzungumza zaidi kwa kuwa alikuwa anawahi kuunganisha ndege nyingine kuendelea na safari.   


  Kocha Tom Saintfiet akiongoza mazoezi ya Free State leo
  Kocha mpya wa Free States, Saintifiet amesema kwamba Ngassa ni mchezaji mzuri ambaye akipata nafasi ya kucheza Ligi Kuu ya hapa, PSL atafanikiwa zaidi. 
  “Kwanza Free State wenyewe hawatakaa naye, watamuuza ndani ya mufa mfupi, rahisi sana hata kuondokea hapa kwenda Ulaya, si rahisi mchezaji kutoka Tanzania kwenda Ulaya, lakini hapa, inawezekana,”amesema.
  Ameishauri Yanga SC kuzungumza vizuri na Free States ili wamalizane. “Ngassa kabakiza mwaka mmoja tu katika Mkataba wake, Yanga kama watakataa hiyo ofa leo, anaweza kuondoka bure kuja hapa akimaliza Mmataba wake,”alisema Mtakatifu Tom. 
  Ngassa aliondokea katika kambi ya timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ikiwa inajiandaa kwa safari ya Botswana kuweka kambi ya wiki mbili kujiandaa mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika (AFCON) dhidi ya Msumbiji (Mambas) itakayochezwa Julai 20 mwaka huu Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: FREE STATE YAIONGEZA DAU YANGA SC ILI KUMSAJILI NGASSA, MALINZI ASIKITIKA AFRIKA KUSINI, SAINTFIET ASEMA MRISHO ATATISHA PSL Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top