• HABARI MPYA

    Friday, June 27, 2014

    VICTOR COSTA: NILITUMWA NA VIONGOZI WA SIMBA NIKAIHUJUMU YANGA MWAKA 2005

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    BEKI wa zamani wa Simba SC, Victor Costa ‘Nyumba’ amesema kwamba alipanga na viongozi wa klabu hiyo aende Yanga mwaka 2005 kuwahujumu na alipomaliza kazi yake, akarejea nyumbani.
    Costa amesema hayo Kigamboni, Dar es Salaam juzi, wakati alipokuwa akimpigia kampeni mke wake, Jasmine anayewania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo.
    Wagombea mbalimbali waliozuru tawi la Kigamboni kuomba kura walijieleza mbele ya wanachama akiwemo Jasmine, lakini Costa akaomba naye kuzungumza.
    Mpeni kura mke wangu; Victor Costa amesema alipanga na viongozi wa Simba aende kuhujumu Yanga mwaka 2005. Chini ni Jasmine anayegombea Ujumbe 

    “Naombeni sana mumpe kura mke wangu Jasmine, namuamini ni mpiganaji na ataisaidia timu, hali sasa ni mbaya, Simba SC miaka mitatu hakuna ubingwa, imefikia hadi Mbeya City wanapanda ndege, Simba tupo, inasikitisha, mpeni kura mke wangu atasaidia timu,”alisema Costa.
    Hata hivyo, mwanachama mmoja wa tawi hilo akamuuliza Coasta kwa nini alisaliti timu na kuhamia Yanga mwaka 2005? 
    Coasta akajibu; “Ile sisi tulipanga na viongozi niende kule kuwahujumu, nilipomaliza nikarudi,”.
    Costa alitoa kali mwaka 2005 aliposaini Yanga SC na kujiunga nayo ikiwa inashiriki Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar, lakini timu hiyo ya Jangwani iliporudi Dar es Salaam akaibukia kwenye mazoezi ya Simba SC.  
    Costa aliyekuwa benchi na jezi ya Yanga wakati inacheza fainali ya Kombe hilo na kufanikiwa kubeba Kombe, aliibuka Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini katika mazoezi ya Simba na jezi iliyoandikwa Malinzi mgongoni.
    Rais wa sasa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi wakati huo alikuwa Katibu wa Yanga na ndiye aliyefanikisha usajili wa beki huyo wa kati.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: VICTOR COSTA: NILITUMWA NA VIONGOZI WA SIMBA NIKAIHUJUMU YANGA MWAKA 2005 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top