• HABARI MPYA

    Monday, April 14, 2014

    MWAIKIMBA: SOKOINE? NILIJUA NITAFUNGA

    Na Mahmoud Zubeiry, Mbeya
    MSHAMBULIAJI wa Azam FC ya Dar es Salaam, Gaudence Exavery Mwaikimba amesema kwamba anamshukuru Mungu kwa kuendeleza rekodi yake nzuri ya kufunga mabao kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Mwaikimba alifunga bao la kwanza katika ushindi wa 2-1 dhidi ya wenyeji Mbeya City Council (MCC) katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwenye Uwanja huo na Azam imetangaza ubingwa wa Ligi Kuu.
    Hongera mwana; Gauence Mwaikimba akipongezwa na Said Mourad baada ya kufunga jana

    “Nasikia furaha sana, nilijua nitafunga, na nilipigana kufunga, kwa kweli niseme tu namshukuru Mungu, nimeweza kuendeleza rekodi yangu ya kufunga katika Uwanja huu,”alisema na kuongeza, “Mbeya ni nyumbani, nimecheza sana hapa tangu nipo mdogo sana, Uwanja huu naujua vizuri, uzuri nina bahati ya kufunga hapa,”.
    Mapema kabla ya mechi hiyo, BIN ZUBEIRY ilimnukuu mshambuliaji huyo wa zamani wa Tukuyu Stars na Prisons zote za Mbeya akisema kwamba anakubalika sana Mbeya na ana mashabiki wengi, ambao hao humuunga mkono anapokuwa amevaa jezi ya timu yoyote.
    Azam FC imejihakikishia ubingwa wa Ligi Kuu inayofikia tamati Aprili 19, mwaka huu kwa kufikisha pointi 59 baada ya kucheza mara 25, ikiwafunga tela waliokuwa mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 55 za mechi 25 pia na Mbeya City yenye pointi 46 za mechi 25.  
    Yanga SC itamaliza na mahasimu Simba SC Uwanja wa Taifa, wakati Azam itamaliza na JKT Ruvu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Hata hivyo, Yanga SC wana malalamiko Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) dhidi ya mchezaji Mohamed Netto wa JKT Mgambo aliyecheza siku wanafungwa mabao 2-1 na timu hiyo ya Jeshi la Kujenga Taifa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
    Lakini kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu, malalamiko hayo hayawezi kupangua matokeo iwapo madai ya Yanga yataonekana yana ukweli, bali zitatolewa adhabu tu kwa ama kwa timu au mchezaji.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWAIKIMBA: SOKOINE? NILIJUA NITAFUNGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top