• HABARI MPYA

    Wednesday, September 04, 2013

    SERIKALI IKAE IKIJUA KUNA MATATIZO KWENYE NGUMI ZA KULIPWA, NA ISIPOCHUKUA HATUA, YETU MACHO NA MASIKIO!

    IMEWEKWA SEPTEMBA 4, 2013 SAA 1:47 ASUBUHI
    BONDIA wa kulipwa Ibrahim Maokola amekwama Italia akidai kutelekezwa na promota Shomary Kimbau aliyempeleka huko kwa ajili ya kupigana. 
    Bondia huyo anaomba msaada wa tiketi aweze kurejea nyumbani, akidai watu wanaomuhifadhi huko wamekwishamchoka na wanataka kumfukuza.
    Bondia Mmarekani Phil Williams ameondoka nchini mikono mitupu baada ya pambano lake la ubingwa wa dunia dhidi ya Mtanzania, Francis Cheka Ijumaa iliyopita ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.

    Sasa jeshi la Polisi nchini linambana promota Jay Msangi aliyeandaa pambano hilo atoe fedha hizo zitumwe Marekani kwa bondia huyo. Iliripotiwa mabondia karibu wote wa nyumbani waligoma kupanda ulingoni hadi walipwe kwanza fedha zao na timu ya waandaaji wa mapambano ikalazimika kuwashawishi kukubali kupigana.
    Bado mabondia wengi wanalalamika kupelekwa kupigana nje ya nchi kwa malipo duni na wanapodai malipo makubwa, mapromota huwatenga na kufuata mabondia wengine, hata kama uwezo wao ni mdogo.
    Asilimia kubwa ya mabondia wanaopelekwa kupigana nje ni wenye uwezo mdogo na wanaishia kupigwa kwa Knockout (KO) za mapema, kwa sababu wahusika wanakwepa mabondia mazuri kwa kuwa wanataka fedha nyingi.
    Hapa nchini kwenyewe karibu katika kila pambano mabondia wanadhulumiwa fedha- kuna promota amekwishawahi kutangaza pambano Francis Cheka atacheza na Japhet Kaseba, kumbe mapema tu hakukuwa na makubaliano ya pambano hilo.
    Watu wakamiminika kwa wingi Uwanja wa Taifa na matokeo yake Cheka hakupanda ulingoni, ingawa alitokea uwanjani kama watazamaji wengine.
    Kuna matatizo kwenye ngumi za kulipwa na umefika wakati sasa serikali ikafanya uchunguzi wa kina juu ya chanzo cha matatizo.
    Miaka ya nyuma kulikuwa kuna chama kimoja tu cha ngumi za kulipwa, ambacho kilisimamia na kuratibu mchezo huo nchini. Kila bondia aliyekwenda nje ya Tanzania, ilitokana na ridhaa ya BUT (Boxing Union Of Tanzania) na hakukuwahi kutokea kesi za bondia kutelekezwa nje au kulipwa kidogo.
    Lakini baadaye ukatokea utitiri wa vyama vya ngumi na kukawa hakuna utaratibu tena kuanzia wa kuandaa mapambano hapa nchini wala usimamizi wa mchezo wenyewe kwa ujumla.
    Mabondia wanakwenda holela nje na sasa zinatokea kesi kama hizi za kutekelezwa na kulipwa kidogo. Dhahiri, tatizo linaanzia hapa. Angalia katika soka, kuna chama kimoja tu, TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) na mchezaji akitaka kwenda nje, basi inaeleweka.
    Inafahamika, TFF ni mwanachama wa FIFA tu, bodi pekee ya kimataifa ya soka duniani, lakini katika ngumi kuna bodi nyingi za kimataifa- hivyo utaratibu wake pia ni tofauti.
    Lakini bado pamoja na kuwa na utitiri wa vyama vya ngumi nchini, tunaweza kuwa na bodi kuu ya kusimamia na kuratibu mchezo huo nchini ambayo ndiyo itakuwa inawajibika moja kwa moja.
    Hii kwa kiasi kikubwa itapunguza matatizo yenye kuepukika. Itakuwa na wajibu wa kujua kila kitu kuhusu bondia kabla ya kupanda ndege kwenda nje, juu ya maslahi yake na usalama wake kwa ujumla.
    Kadhalika bodi hii itakuwa na wajibu wa kujiridhisha kwa kila kitu juu ya mchezo wowote utakaoandaliwa nchini kabla ya kufanyika. Lakini kwa sasa iwapo Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo, haitachukua hatua, basi tusubiri mengine zaidi baada ya haya. Siku njema.     
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SERIKALI IKAE IKIJUA KUNA MATATIZO KWENYE NGUMI ZA KULIPWA, NA ISIPOCHUKUA HATUA, YETU MACHO NA MASIKIO! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top