• HABARI MPYA

  Wednesday, September 25, 2013

  AZAM FC YASEMA JEBA BADO MCHEZAJI WAO HALALI NA ANAPATA HAKI ZAKE ZOTE, COASTAL..

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA SEPTEMBA 25, 2013 SAA 3:29 ASUBUHI
  AZAM FC imesema kwamba kiungo Ibrahim Rajab ‘Jeba’ bado ni mali yao na anaendelea kutekelezewa haki zake zote za msingi, hivyo klabu yoyote itakayomtaka italazimika kumalizana nao kwanza.
  Katibu Mkuu wa Azam FC, Nassor Idrisa Mohammed ‘Father’ ameiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, Jeba amepewa mapumziko kwa sasa kutokana na ushauri wa madaktari bingwa waliomfanyia uchunguzi wa kiafya nchini India.
  Father alisema Jeba hatakiwi kucheza mpira kwa sasa kutokana na matatizo yake kiafya na kwa kuheshimu hilo, ndiyo maana klabu imeendelea kumtimizia haki zake zote za msingi akiwa mapumziko.
  Kushoto kabisa Jeba akiwa na John Bocco na Himid Mao

  Hata hivyo, Father alistaajabishwa na habari kwamba, mchezaji huyo amejiunga na Coastal Union ya Tanga, ambayo imeripotiwa kutaka kumsajili wakati wa dirisha dogo.
  “Sisi tumeona afya ya huyu mchezaji ni bora zaidi, kuliko kulazimisha kumtumia bila kujali afya yake. Lakini nasikia kuna watu wanataka kumpeleka Coastal. Inashangaza sana, ila sisi hatuna neno, kwa kuwa huyu ni mchezaji wetu, waje tu tumalizane,”alisema Father. 
  Father alisema Jeba alikuwa Dar es Salaam akiendelea kupumzika huku akihudumiwa vizuri na klabu kuanzia suala la tiba na mahitaji yote, lakini hivi karibuni akaomba kwenda kupumzika nyumbani kwao.  
  “Hivi ninavyozungumza na wewe, hadi mshahara wake wa mwezi huu (Septemba) umekwishatayarishwa na amekuwa akilipwa mishahara yake siku zote za matatizo yake, hatuna shaka Jeba ni mchezaji wetu halali,”alisema.
  Jeba ni mchezaji aliyepandishwa kutoka timu ya vijana ya Azam, Azam Akademi msimu uliopita, lakini akashindwa kucheza kutokana na matatizo ya kiafya.
  Awali, kabla ya kupandishwa timu ya wakubwa ya Azam, mchezaji huyo alikwenda kujiunga na Simba SC, lakini akalazimika kurejea kwa sababu ya Mkataba wake. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: AZAM FC YASEMA JEBA BADO MCHEZAJI WAO HALALI NA ANAPATA HAKI ZAKE ZOTE, COASTAL.. Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top