• HABARI MPYA

  Tuesday, September 17, 2013

  REFA WA PWANI KUCHEZESHA YANGA NA PRISONS KESHO SOKOINE

  Na Boniface Wambura, IMEWEKWA SEPTEMBA 17, 2013 SAA 11:35 JIONI
  LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi ya nne kesho (Septemba 18 mwaka huu) kwa mechi saba katika viwanja saba tofauti.
  Vinara wa ligi hiyo, JKT Ruvu wanaonalewa na Kocha Mbwana Makata watakuwa ugenini Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani dhidi ya Ruvu Shooting ya Charles Boniface Mkwasa. Mechi hiyo inatarajiwa kuwa kivutio kikubwa kwa washabiki mkoani Pwani kutokana na aina ya soka inayochezwa na timu hizo.
  Wachezaji wa Yanga wakifanya mazoezi ya kushangilia bao katika Uwanja wa Sokoine jioni ya leo, baada ya kumaliza mazoezi yao kujiandaa na mchezo dhidi ya Prisons kesho kwenye Uwanja huo 

  Baada ya sare dhidi ya Mbeya City wikiendi iliyopita, Yanga inaendelea kubaki Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya ambapo itacheza na Tanzania Prisons katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Simon Mbelwa kutoka Pwani.
  Nayo Simba itaumana na Mgambo Shooting Stars ya Tanga katika mechi itakayopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Mechi hiyo itakuwa chini ya Kamishna David Lugenge kutoka Iringa.
  Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Oljoro JKT kutoka Arusha na wenyeji Kagera Sugar wakati Azam na Ashanti United zitakwaruzana kwenye uga wa Azam Complex ulioko Chamazi jijini Dar es Salaam.
  Mwamuzi Jacob Adongo kutoka Mara ndiye atakayechezesha mechi kati ya Coastal Union na Rhino Rangers itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Mtibwa Sugar inarejea uwanja wake wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro ambapo inaikaribisha Mbeya City ya Kocha Juma Mwambusi.
  Yanga mazoezini Sokoine leo

  Wakati huo huo, Ligi Daraja la Kwanza (FDL) nayo inaendelea kesho (Septemba 18 mwaka huu) kwa mechi moja ambapo Lipuli ya Iringa ambayo wikiendi iliyopita ilicheza Mkamba mkoani Morogoro inapita mjini Morogoro kuikabili Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri.
  Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni atashiriki warsha ya wakufunzi wa makocha wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) itakayofanyika kuanzia Oktoba 22-24 mwaka huu.
  Warsha hiyo iliyoandaliwa na CAF kwa ajili ya wakufunzi wake itafanyika nchini Cameroon. Wakufunzi 18 wa CAF kwa upande wa makocha watahudhuria warsha hiyo.
  Madhumuni ya warsha hiyo ni kuainisha majukumu yao, kubadilishana uzoefu. Pia kuwapa methodolojia mpya ya ufundishaji na muongozo kuhusu mfumo wa leseni za makocha ambao watautumia katika nchi wanazotoka.
  Kocha wa makipa wa Yanga SC, Razack Ssiwa

  Mbali ya Kayuni Tanzania, wakufunzi wengine ni Ahmed Babiker (Sudan), Amadou Shaibu (Nigeria), Boy Bizzah Mkhonta (Swaziland), Duodu Fred Osam (Ghana), Edussei Anthony (Ghana), Fathi Nossir (Misri), Faouzy Altaisha (Sudan) na Fran Hilton Smith (Afrika Kusini).
  Wengine ni Francis Oti-Akenteng (Ghana), Honour Janza (Zambia), Kasimawo Laloko (Nigeria), Mahmoud Saad (Misri), Paul Hamilton (Nigeria), Serame Letsoaka (Afrika Kusini), Shawky Abdel Shafy (Misri), Thondoo Govinder (Mauritius) na Ulric Mathiot (Seychelles), 
  Aidha, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imesema uwakilishi wa ujumbe kwenye Mkutano Mkuu unaanzia kwenye chama cha mpira wa miguu cha mkoa, kufuatiwa na chama shiriki na baadaye klabu ya Ligi Kuu.
  Mwongozo huo juu ya uwakilishi wa wajumbe kwenye Mkutano Mkuu umetolewa kutokana na maombi ya Sekretarieti ya TFF kwa kamati hiyo iliyokutana jana (Septemba 16 mwaka huu) baada ya kubaini baadhi ya wajumbe wanashikilia nafasi mbili kwenye vyama tofauti.
  Kwa mujibu wa Ibara ya 5 ya Katiba, kuna makundi ya aina tatu ya wanachama wanaounda TFF. Makundi hayo ni vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu.
  Sekretarieti ya TFF imebaini kuwa kuna baadhi ya viongozi wa kuchaguliwa wa mikoa ambao pia ni viongozi wa vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu, hivyo wana nafasi zaidi ya moja ya kuingia kwenye Mkutano Mkuu.
  Hivyo, kutokana na mwongozo huo ushiriki wa wajumbe kwenye Mkutano Mkuu wa TFF utaanzia chama cha mkoa, kufuatiwa na chama shiriki na baadaye klabu za Ligi Kuu.
  Pia nafasi ambazo zinaweza kuwakilishwa kwenye Mkutano Mkuu kama mhusika hayupo ni za Mwenyekiti atakayewakilishwa na Makamu Mwenyekiti, na Katibu atakayewakilishwa na Katibu Msaidizi.  Nafasi za ujumbe wa Mkutano Mkuu na ile ya mwakilishi wa klabu hazina uwakilishi kama mhusika hayupo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: REFA WA PWANI KUCHEZESHA YANGA NA PRISONS KESHO SOKOINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top