• HABARI MPYA

  Jumamosi, Septemba 28, 2013

  NGASSA AREJEA NA NEEMA YANGA SC, YAPATA USHINDI WA KWANZA BAADA YA MECHI TANO LIGI KUU

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA SEPTEMBA 28, 2013 SAA 12:20 JIONI
  MRISHO Khalfan Ngassa leo ameanza kazi vizuri Yanga SC baada ya kuiongoza timu hiyo kupata ushindi wa kwanza ndani ya mechi tano, kwa kuilaza Ruvu Shooting ya Pwani 1-0- jioni hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Bao limefungwa na Mganda Hamisi Friday Kiiza, dakika ya 63 akiunganisha kwa tik tak krosi ya Ngassa, ambaye baada ya kupokea pasi ndefu ya Athumani Iddi ‘Chuji’, akamtoka beki wa Ruvu, Stefano Mwasyika.
  Amerudi kwa neema; Ngassa ameisaidia Yanga SC kushinda 1-0 Ligi Kuu

  Pamoja na ushindi huo, Yanga walikuwa katika wakati mgumu kipindi cha kwanza baada ya kuzidiwa katika eneo la kiungo na Ruvu, iliyoongozwa na Hassan Dilunga katika idara hiyo, akiwafunika Frank Domayo na Haruna Niyonzima.
  Lakini kuingia kwa Chuji kipindi cha pili, aliyekwenda kuchukua nafasi ya Domayo, kulileta uhai katika safu ya kiungo ya Yanga na haikuwa ajabu walipofankiwa kupata ushindi.
  Ngassa na Kiiza wakishangilia

  Kwa matokeo hayo, Yanga SC inatimiza pointi tisa baada ya kucheza mechi sita sawa na Azam ambao hata hivyo wamecheza mechi tano, wakati Simba SC waliocheza mechi tano wapo kileleni kwa pointi zao 11.
  Yanga SC; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo/Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva/Nizar Khalfan, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbangu, Hamisi Kiiza na Mrisho Ngassa.
  Ruvu Shooting; Abdul Seif, Michael Pius, Stefano Mwasyika, George Michael, Shaaban Suzan, Gedion David, Ayoub Kitala/Said Madega, Hassan Dilunga, Cossmas Lewis, Elias Maguri na Reuben Lambele/Kulwa Mfaume.  Katika mechi nyingine, Mbeya City imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Coastal Union Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya. Coastal walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya saba kupitia kwa Haruna Moshi ‘Boban’ kabla ya Mbeya kusawazisha kupitia kwa Mwagane ‘Morgan’ Yeya dakika ya 70.
  Katika mchezo huo, Richard Peter wa Mbeya City na Markus Ndeheli na Haruna Moshi wa Coastal walipewa kadi nyekundu.
  Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora Rhino Rangers walichapwa 1-0 na Kagera Sugar, bao pekee la Themi Felix dakika ya 66 katika mchezo ambao, kiungo wa wenyeji, Nurdin Bakari alitolewa nje kwa kadi nyekundu.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: NGASSA AREJEA NA NEEMA YANGA SC, YAPATA USHINDI WA KWANZA BAADA YA MECHI TANO LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top