• HABARI MPYA

  Alhamisi, Septemba 19, 2013

  DHAIRA AFUFUA MAKALI SIMBA SC, AWEKA BONGE LA REKODI LIGI KUU, KASEJA SASA…

  Na Mahmoud Zubeiry, Mbeya, IMEWEKWA SEPTEMBA 19, 2013 SAA 2:15 ASUBUHI
  KIPA Mganda wa Simba SC, Abbel Dhaira ameonekana kuimarika baada ya kudaka mechi tatu mfululizo bila kuruhusu hata bao moja katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara- hali ambayo inaweza kuwafanya wapenzi wa timu hiyo wasahau kuhusu Juma Kaseja.
  Dhaira alikuwa ana mwanzo mbaya ndani ya Simba SC, akifungwa mabao 18 katika mechi 11 alizoidakia klabu hiyo tangu Januari mwaka huu alipojiunga nayo hadi Agosti 24, hali ambayo iliibubua tetesi za klabu hiyo kutaka kumrejesha kipa wake namba wa muda mrefu, Kaseja iliyemtema mwishoni mwa msimu.
  Lakini baada ya kufungwa mabao mawili rahisi katika sare ya 2-2 na Rhino Rangers Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora, Dhaira aliyetua Msimbazi akitokea IBV ya Ligi Kuu ya Iceland, amedaka mechi tatu bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa, Simba ikishinda 1-0 dhidi ya JKT Oljoro mjini Arusha, 2-0 na Mtibwa Sugar na jana 6-0 na Mgambo JKT, Dar es Salaam  
  Sasa hafungiki; Abbel Dhaira amesimama langoni dakika 270 bila kufungwa  REKODI YA DHAIRA TANGU ATUE SIMBA

  Simba SC 1-1 Bandari (Kombe la Mapinduzi, alifungwa moja)
  Simba SC 0-1 U23 Oman (Kirafiki, alifungwa moja)
  Simba SC 1-3 Qaboos (Kirafiki, alidaka nusu akafungwa mawili)
  Simba SC 0-4 R. de Libolo (Ligi ya Mabingwa, alifungwa manne) 
  Simba SC 2-1 Coastal Union (Ligi Kuu, alifungwa moja)
  Simba SC 2-2 Azam FC (Ligi Kuu, alifungwa mbili)
  Simba SC 1-0 Kahama United (Kirafiki, Kahama hakufungwa)
  Simba SC 1-2 URA (Kirafiki, Taifa, alifungwa mbili)
  Simba SC 0-1 Coastal (Kirafiki, Tanga alifungwa moja)
  Simba SC 4-1 SC Villa (Simba Day, Taifa alifungwa moja)
  Simba SC 2-2 Rhino (Ligi Kuu, alifungwa mbili)
  Simba SC 1-0 JKT Oljoro (Ligi Kuu, hakufungwa)
  Simba SC 2-0 Mtibwa Sugar (Ligi Kuu, hakufungwa)
  Simba SC 6-0 Mgambo JKT (Ligi Kuu, hakufungwa)
   Mechi ya kwanza Dhaira kuidakia Simba SC ilikuwa ni dhidi ya Bandari Uwanja wa Amaan, Zanzibar katika Kombe la Mapinduzi Januari mwaka huu, ambako alifungwa bao moja, timu hiyo ikitoa sare ya 1-1.
   Baada ya hapo, akaidakia Simba ikicheza dhidi ya U23 ya Oman, ambako alifungwa moja, timu hiyo ikifungwa 2-1 na akadaka dhidi ya timu ya Jeshi Oman na kufungwa mara mbili, timu hiyo ikilala 3-2. Bao lingine alifungwa Juma Kaseja, ambaye ametemwa msimu huu. 
   Akadaka tena katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Recreativo de Libolo ya Angola na kufungwa mabao manne, timu hiyo ikilala 4-0.
   Akarudi Dar es Salaam na kudaka katika mchezo wa Ligi Kuu msimu uliopita dhidi ya Coastal Union ya Tanga na kufungwa bao moja, timu hiyo ikishinda 2-1.
   Akadaka tena katika Ligi Kuu dhidi ya Azam na kufungwa kafungwa mabao mawili, moja la penalti timu hizo zikitoka 2-1, huo ukiwa mchezo wake wa mwisho Simba SC msimu uliopita.
   Akarejea kwenye mechi za kujiandaa na msimu huu, akadaka dhidi ya Kahama United mkoani Shinyanga na kwa mara ya kwanza tangu ajiunge na timu hiyo alifanikiwa kumaliza mechi bila kufungwa. 
   Akadaka tena dhidi ya URA ya kwao, Uganda katika mchezo wa kirafiki na kutunguliwa mara mbili timu hiyo ikilala 2-1 katika mchezo huo wa kirafiki, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Akaenda Tenga kwenye mchezo wa kirafiki na Coastal, akafungwa moja, Wekundu wa Msimbazi wakilala 1-0. 
   Akadaka tena dhidi ya SC Villa ya kwao, Uganda na kufungwa bao moja, timu hiyo ikishinda 4-1 kabla ya kufungwa mawili katika sare ya 2-2 na Rhino, hiyo ikiwa mara ya mwisho nyavu zake kutikiswa.
   Sasa yuko madhubuti; Abbel Dhaira ameanza kuwa tishio Ligi Kuu ya Bara 
   Kisoka, Dhaira aliibukia Express mwaka 2006 ambako alicheza hadi 2008 akahamia URA, alikocheza hadi 2010 akahamia AS Vita ya DRC ambayo ilimuuza IBV mwaka 2012 alikodaka mechi 30 bila kufungwa bao hata moja, hadi anahamia Simba mwaka huu.
   Amekuwa akiidakia timu ya taifa ya Uganda tangu mwaka 2009 na tangu 2011 amekuwa kipa namba moja wa timu hiyo, ingawa kwa sasa anakabiliwa na ushindani wa aliyekuwa kipa wa kwanza wa timu hiyo kabla yake, Dennis Onyango pamoja Muwonge Hassan anayeibukia vizuri.
   Ndiyo basi tena; Juma Kaseja kulia alikuwa akizungumziwa kurejeshwa Simba SC wakati Abbel Dhaira hafanyi vizuri. Kushoto Amri Kiemba
   Dhaira alidaka mechi moja tu na kuumia katika Kombe la Challenge mwaka jana na baada ya hapo, Muwonge akadaka hadi kuipa timu ubingwa. Muwonge tena akaipa Uganda tiketi ya CHAN- na sasa anajitengenezea mazingira mazuri The Cranes mbele ya Onyango na Dhaira. 
   • Blogger Comments
   • Facebook Comments
   Item Reviewed: DHAIRA AFUFUA MAKALI SIMBA SC, AWEKA BONGE LA REKODI LIGI KUU, KASEJA SASA… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
   Scroll to Top