• HABARI MPYA

  Wednesday, September 25, 2013

  BEKI LA NGUVU KAZE GILBERT NA MSHAMBULIAJI HATARI TAMBWE WAREJEA KAZINI SIMBA SC

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA SEPTEMBA 25, 2013 SAA 6:00 MCHANA
  BEKI Kaze Gilbert aliyeumia nyonga Jumamosi Simba SC ikimenyana na Mbeya City na kutoka sare ya 2-2 katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, anatarajiwa kurejea mazozini leo baada ya kupona.
  Aidha, Mrundi mwenzake Amisi Tambwe aliyeumia pia nyama katika mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua, naye anatarajiwa kuanza mazoezi leo.
  Daktari wa Simba SC, Yassin Gembe ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, mbali na Warundi hao wawili waliosajiliwa kutoka Vital’O ya Burundi, majeruhi mwingine ni kiungo Henry Joseph ambaye anasumbuliwa na maumivu ya goti.
  Warundi wawili; Kaze Gilbert na Amisi Tambwe wote wanarejea mazoezini leo

  “Henry bado kidogo, nadhani kuanzia kesho tunaweza kujua anaweza kuanza lini mazoezi. Lakini Kaze na Tambwe wote tunawatarajia leo wataanza mazoezi,”alisema.
  Simba SC inayofundishwa na mwalimu mkongwe, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ imeweka kambi Bamba Beach Resort, Kigamboni, Dar es Salaam kwa ajili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inayoendelea nchini.    
  Hadi sasa, Wekundu hao wa Msimbazi wanashika usukani wa Ligi Kuu kwa pointi zao 11, baada ya kucheza mechi tano, wakiwazidi mabingwa watetezi, Yanga SC kwa pointi tano na washindi wa pili wa msimu uliopita, Azam kwa pointi mbili.
  Dk Yassin Gembe akimtibu Kaze Gilbert Jumamosi

  Simba SC itashuka dimbani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumapili kumenyana na JKT Ruvu katika mfululizo wa ligi hiyo, wakati Rhino Rangers itamenyana na Kagera Sugar Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora, Mbeya City na Coastal Union Sokoine, Mbeya, Mgambo JKT na JKT Oljoro Mkwakwani, Tanga na Ashanti United na Mtibwa Sugar, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Mechi nyingine itachezwa Jumamosi, Yanga SC na Ruvu Shootings Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati leo Rhino Rangers wanaikaribisha Ashanti United Mwinyi, Tabora.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: BEKI LA NGUVU KAZE GILBERT NA MSHAMBULIAJI HATARI TAMBWE WAREJEA KAZINI SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top