• HABARI MPYA

  Tuesday, September 24, 2013

  SIMBA SC NA OKWI SASA KITAELEWEKA NDANI YA WIKI MOJA TU...KUSUKA AU KUNYOA ITAJULIKANA

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA SEPTEMBA 24, 2013 SAA 2:43 USIKU
  SIMBA SC itaamua hatima ya msambuliaji wake wa zamani, Emmanuel Okwi mwishoni mwa mwezi huu kama itamrejesha au la, baada ya kufika kwa tarehe ya mwisho ya klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia iliyomnunua Januari mwaka huu ya kulipa fedha za manunuzi yake, dola za Kimarekani 300,000 zaidi ya Sh Milioni 480. 
  Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameiambia BIN ZUBEIRY juzi kwamba, Septemba 30 ndio wataamua wafanye nini baada ya kufika tarehe ya mwisho ya kulipwa fedha zao.
  Tarehe 30; Fedha za Okwi zitawasilishwa Septemba 30?

  Kwa sasa, tayari Okwi, mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda yupo Dar es Salaam akiwa amesusa kurejea Tunisia kutokana na madai ya klabu hiyo kushindwa kumlipa mishahara kwa miezi mitatu.
  Okwi amekaririwa akisema kwamba tayari kesi yake ameifikisha Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), wakati Etoile nayo imekaririwa kudai imemshitaki mchezaji huyo FIFA pia kwa kushindwa kuripoti kazini kwa muda mrefu sasa, baada ya ruhusa ya kwenda kujiunga na timu yake ya taifa miezi miwili iliyopita. 
  Baada ya kumnunua mchezaji huyo Januari mwaka huu, Etoile iliahidi kutuma fedha za manunuzi yake mjini Dar es Salaam, lakini siku zilikatika hadi katikati ya mwaka, uongozi wa Simba ulipolazimika kwenda Tunisi kufuatilia fedha hizo.
  Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Hans Poppe aliongozana na Katibu wa klabu, Mwanasheria, Evodius Mtawala hadi Tunis na wakiwa huko, klabu hiyo iliahidi kulipa fedha hizo ifikapo Septemba 30. 
  Kapteni ndani ya Tunis; Hans Poppe akiwa Tunis kufuatilia fedha za Okwi. Ahadi ya Septemba 30 itatimizwa? 

  Katikati ya ahadi hiyo, Okwi naye akasusa kwa madai ya kutolipwa mishahara- jambo ambalo linazidi kuiweka pagumu biashara hiyo, ingawa kwa mujibu wa sheria, Etoile wanatakiwa kuilipa Simba SC fedha zake kisha kuendelea na kesi yao na mchezaji huyo.
  Tayari Simba SC imepata hasara ya kumkosa mchezaji huyo katika mzunguko wote wa pili wa Ligi Kuu msimu uliopita na mzunguko wote wa kwanza msimu huu- na haijulikani hata ikimrejesha watasaini Mkataba mpya na kumlipa fedha tena au itakuwaje.
  Mkataba ambao Simba SC ilisaini na Etoile kuhusu Okwi, mbali na kulipwa dola 300,000 pia una kipengele cha atakapouzwa timu yoyote, Wekundu wa Msimbazi wapewe sehemu ya fedha. Hii ni kesi ngumu.    
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: SIMBA SC NA OKWI SASA KITAELEWEKA NDANI YA WIKI MOJA TU...KUSUKA AU KUNYOA ITAJULIKANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top