• HABARI MPYA

  Wednesday, September 25, 2013

  MANJI AWATULIZA WACHEZAJI YANGA SC, AWAAMBIA HANA NOMA NAO, AMVUTA NGASSA PEMBENI WAYAMALIZA 'KIKUBWA'

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA SEPTEMBA 25, 2013 SAA 7:11 MCHANA
  MWENYEKITI wa Yanga SC, Alhaj Yussuf Mehboob Manji amewaambia wachezaji wa timu hiyo kwamba hana matatizo nao kwa matokeo ya awali ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na amewataka waelekeze nguvu zao katika mechi zijazo.
  Yanga imeambulia pointi sita katika mechi tano za awali za Ligi Kuu ya Vodacom, kutokana na sare tatu, kushinda moja na kufungwa moja, hivyo kuachwa kwa pointi tano kileleni na wapinzani wao wa jadi, Simba SC.
  Jana Manji alikutana kwa chakula cha jioni na wachezaji wa timu hiyo katika hoteli ya Serena, Dar es Salaam akiwa ameambatana na Makamu wake Mwenyekiti, Clement Sanga, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Isaac Chanji na Mjumbe wa Sekretarieti, Patrick Naggi.
  Manji akipeana mkono na Chuji alipokutana na wachezaji hao mwaka jana.

  Katika kikao hicho, Manji aliwaambia wachezaji wa Yanga hamlaumu yeyote kwa matokeo hayo, kwani ligi bado mbichi, ila akawataka waunganishe nguvu zao kuelekea mechi zijazo, ili kurejesha ushindi na furaha klabuni.
  Pamoja na hilo, Manji alizungumzia suala la madai ya baadhi ya wachezaji ya fedha za usajili na akaliweka sawa kwa wale ambao walikuwa wanadai kuwawekea utaratibu wa malipo haraka, jambo ambalo Naggi ametakiwa kuhakikisha analishughulikia mara moja.
  Aidha, Manji baada ya kikao cha pamoja na wachezaji wote, alimvuta pembeni Mrisho Ngassa kujadiliana naye faragha.
  Haikujulikana mara moja Manji alizungumza nini na Ngassa, lakini inaweza kuwa kuhusu deni analotakiwa kuilipa Simba SC, Sh. Milioni 45 kwa kosa la kusaini Mikataba na timu mbili. Ngassa alifungiwa mechi sita za mashindano na kutakiwa kurejesha fedha alizochukua Simba SC Sh. Milioni 30 pamoja na fidia ya Sh Milioni 15.
  Habari za ndani zinasema, Yanga SC inaweza kulipa deni hilo ili Ngassa aanze kucheza, lakini italazimika kurejeshewa fedha hizo na mchezaji mwenyewe, kwa kuwa klabu ilikwishamalizana naye katika usajili wake. 
  Kuna uwezekano deni hilo likatumika kumuongezea Mkataba Ngassa Yanga SC kutoka wa miaka miwili aliosaini sasa. Ngassa mwenyewe hakupatikana alipotafutwa leo kuzungumzia suala hilo. 
  Yanga SC itamenyana na Ruvu Shootings Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mfululizo wa ligi hiyo, wakati leo Rhino Rangers wanaikaribisha Ashanti United Mwinyi, Tabora.
  Mechi nyingine zitapigwa Jumapili, Simba SC ikishuka dimbani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na JKT Ruvu, Rhino Rangers na Kagera Sugar Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora, Mbeya City na Coastal Union Sokoine, Mbeya, Mgambo JKT na JKT Oljoro Mkwakwani, Tanga na Ashanti United na Mtibwa Sugar, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: MANJI AWATULIZA WACHEZAJI YANGA SC, AWAAMBIA HANA NOMA NAO, AMVUTA NGASSA PEMBENI WAYAMALIZA 'KIKUBWA' Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top