• HABARI MPYA

  Tuesday, September 24, 2013

  JE LIGI YETU INAKIDHI VIWANGO!

  IMEWEKWA SEPTEMBA 24, 2013 SAA 6:40 USIKU
  DUNIANI kuna ligi mbalimbali zenye msisimko kuanzia kwa washabiki hadi kwa wachezaji. Ligi hizi pia zina timu zenye viwango bora na ushindani wa kweli. Mathalani Ligi ya Uingereza, Ujerumani na Hispania. 
  Kwa Afrika pia ziko ligi mbalimbali zenye mvuto na ushindani wa hali ya juu kwa timu mbalimbali na wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu kama Ligi ya Misri, Tunisia, Morocco, Ghana, Algeria, Afrika kusini, Angola na Congo DR. 
  Inasemekana kwa Afrika mashariki ligi yetu ndio ligi yenye washabiki wanaopenda mpira na wenye hamasa na soka kuliko nchi nyingine. Hili limedhibitishwa hata na wachezaji wa kigeni wanaokuja hapa Tanzania. Pamoja na kusifia msisimko,malipo mazuri na hamasa ya washabiki na mapenzi ya soka waliyonayo watanzania, bado wachezaji wengi wa kigeni hasa wa Nchi kama Ivory Coast, Uganda, na Kenya wamekua wakisema kuwa ligi yetu si bora na kwamba kiwango chake ni cha chini kulinganisha na ligi za kwao.
  Sasa hapa swali linakuna je, kama ligi yetu si bora hata kwa kulinganisha na ligi za nchi nyingine za Afrika Mashariki ni nini tatizo?.
  Kuna sababu mbali mbali ambazo zinachangia ligi yetu kutokuwa bora. Katika makala hii nitajaribu kuainisha sababu kadha wa kadha au mambo machache ambayo aghalabu yametufikisha hapa tulipo na hatua za kuchukua ili tutoke hapa tulipo.
  Moja ya sababu kubwa inayochangia kuwa na Ligi dhaifu ni mfumo wa ligi yetu. Kwa kiasi kikubwa mfumo wa ligi yetu hauwezi kumfanya mchezaji kuwa katika kiwango cha kiushindani ipasavyo. Kwa mfano mchezaji mwaka huu anashiriki ligi ya Taifa Mechi za makundi timu yake ikishinda inacheza mechi chache za timu zilizochujwa ikishinda inapanda daraja la kwanza. Daraja la Kwanza zinapangwa kwenye makundi. Kisha timu chache zinapita zinaingia kwenye ligi ya muda mfupi kisha timu tatu zinapanda ligi kuu. Sasa ona kwa staili hiyo kweli twaweza kuwa na timu bora? 
  Kwa mfano zamani kulikuwa na Ligi za Wilaya za mikoa mbalimbali. Timu zinazoshinda zinaingia Ligi daraja la nne  ndani ya mikoa husika. Kisha zikifanikiwa zinaingia ligi Daraja la tatu, Baada ya hapo timu bora inaingia Ligi Daraja la pili Taifa wachacheza ligi kwa mwaka mzima kisha timu kadhaa za juu zinapanda ligi kuu. Kwa mantiki hiyo kama timu imeanzishwa inashiriki michezo ya mchangani, basi kwa mfumo huo wa kuanzia daraja la nne, la tatu , la pili, la Kwanza (ligi kuu) inabidi timu itumie takribani miaka minne au tano kuweza kufika ligi kuu. Tena hii ni kama timu hiyo itakuwa inashinda kila daraja husika. 
  Uchache wa timu katika ligi yetu pia inaweza kuwa ni sababu nyingine ya kufanya ligi yetu isiwe na ushindani wa kutosha na hivyo kufanya wachezaji wengi kucheza mechi chache au hata kutocheza kabisa na hivyo kutoweza kufikia malengo yao. Ligi yetu ina timu kumi na nne tu na mpaka ligi inaisha mchezaji aliyecheza mechi zote anakuwa kacheza michezo 26 tu. Hizi ni mechi chache sana kwa nchi ambayo inafikiria kukuza soka lake. Kulingana na kumbukumbu zangu Shirikisho la Soka la mpira wa miguu Dunia (FIFA), linasema wazi kuwa ili mchezaji afikie kiwango cha kimataifa ni lazima acheze mechi zisizopungua 40 katika msimu mmoja na si vinginevyo. Sasa kwa mantiki hii kuna pengo la michezo 14 kati ya kiwango cha michezo cha FIFA na Michezo ya ligi yetu!.
  Kuna kipindi kocha wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ aliwahi kutamka kuwa ligi ya Tanzania ni mbovu, hata Stewart Hall Kocha wa Azam FC kwa kipindi kifupi alichoondoka Azam na kwenda kufundisha Timu ya Sofapaka FC ya Kenya Aliporudi Azam FC alikiri kwamba anarudi AZAM kwa sababu ya maslahi mazuri na mapenzi ya timu ya Azam kwake na si kwa sababu ya kiwango cha ligi yetu kwani Ligi ya Kenya ni bora kuliko yetu. 
  Kama kweli tunataka ligi bora kuna mambo mengi tunapaswa kufanya kama taifa. Jambo la kwanza kubwa kabisa ni mfumo wa ligi yetu. Mfumo wa kuendesha ligi unapaswa ubadilike, uwekwe mfumo ambao utafanya ligi yetu iwe ya ushindani. Moja wapo ni kurudisha mfumo wa zamani wa madaraja mengi kama daraja la nne,la tatu, la pili, la kwanza na ligi kuu. Hata nchi zenye soka la ushindani kama Uingereza, Ujerumani, Hispania, Italia, ufaransa, Ureno, Uholanzi, Ubelgiji zina madaraja mengi. Pia kuwa na timu za kutosha katika ligi. Wapo wadau wengi sana wa michezo wanaounga mkono jambo au wazo langu hili. 

  Katika makala ya Joseph Zablon iliyotoka gazeti la mwananchi la tarehe 17-09-2013 kumuhusu mchezaji wa Zamani Kombo Aboubakary inayosema ‘’ wachezaji wanaingia stars kwa miujiza’’ Mchezaji huyo wa zamani anashangaa udhaifu wa ligi ya sasa na wachezaji wa sasa kulinganisha na wa zamani. Anasema zamani soka lilikuwa la ushindani sana kulikuwa na timu ngumu kama Pamba,Ushirika,Tukuyu Stars,Mecco,Reli Moro, Pan Africa, Plisner,Sigara, Coastal na African Sports. Kombo anaendelea kusema kipindi hicho ligi ilikuwa na msisimko mwanzo mwisho tofauti na sasa. Anazungumzia jinsi ilivyokuwa vigumu kuitoa timu kutoka daraja la nne, la tatu, la pili hadi la kwanza.  Kila mchezaji wa wakati huo alikuwa na lengo la kuhakikisha timu yake inafika ligi daraja la kwanza.Akafafanua pia kuwa kuna timu ziliishia madaraja ya chini kutokana na ushindani huo. Kombo anazungumzia jinsi vipaji vya timu ya madaraja ya chini vilivyo hifadhiwa na kuboreshwa kwa lengo tu la siku moja kufika ligi daraja la kwanza. Kutokana na sababu hiyo ya ushindani uliokuwa madaraja ya chini, vipaji vilikuwa vingi na mfumo wa ligi ulipelekea kutoa baadhi ya timu zilizokuja kuchukua ubigwa wa Bara na Muungano ambazo ni nje ya Simba na yanga. Anatolea mfano wa Coastal Union na African Sports. Kutokana na mfumo wa ligi yetu wa sasa kutokuwa mzuri Kombo anasema ndio maana inatokea mchezaji anasajiliwa ghafla Simba au Yanga ama hata kuchezea timu ya taifa katika mazingira ambayo hata mchezaji mwenyewe anaona kama miujiza. Kombo anasisitiza kuwa kama mfumo wa awali ungekuepo ligi ingekuwa bora sana. Zaidi Kombo Abubakari anasisitiza soka la watoto na michezo au mashindano ya kutosha kwa ajili ya timu zetu. 
  Ushauri mwingine ni wa ligi kuwa na udhamini wa kuaminika, kwa mfano tunaweza kuipa kampuni kazi ya kuongoza ligi yetu. Na kuhakikisha pia timu mbali mbali zinazoshiriki mashindano makubwa mathalani ligi kuu zinakuwa na wadhamini.
  Kwa mantiki hiyo kuna umuhimu sasa kwa wadau mbalimbali wapenda soka wenye uwezo kuwekeza katika uanzishaji wa timu za vinaja na hasahasa Akademy za soka ili kukuza vipaji mbalimbali ambayo bado havijavumbuliwa. Zaidi ya hilo wadau ambao wanauwezo na ambao wapo shirika na timu mbalimbali za ligi kuu wanapaswa kuimarisha na kuzipa uwezo timu hizo ili ziweze kumiliki timu za watoto wadogo wa miaka mbalimbali kama vile U14 U17 na U20 kwani ndio umri sahihi zaidi wa kukuza vipaji na kugundua vipaji vilivyofichika. 
  Jambo jingine TFF inaweza kuanzisha mashindano mbalimbali ambayo ama yatachezwa ligi inaposimama au ikiisha. Mashindano kama Kombe la Muungano, Kombe la Hedex, Kombe la Taska, Kombe la AZAM (AZAM CUP) n.k achilia mbali makombe ya vijana kama kopa Coca Cola, Uhai Cup, Airtel Raising Stars n.k. Inapaswa pia TFF ifanye juhudi kutafuta wadhamini wa mashindano mbalimbali ili kuleta ushindani kwa mashindano husika. Hiyo ni mifano michache tu, bado kunaweza kubuniwa mashindano mengine mengi mbali na hayo kwa namna hiyo lazima mchezaji atacheza mechi zaidi ya 50 kwa msimu, hapo sasa hata mchezaji akifika katika timu ya taifa atakuwa amekomaa na ni rahisi kwa kocha kutengeneza muunganiko wa timu. 
  Ratiba ya ligi pia ni tatizo lingine linalochangia kushuka kwa ligi yetu Unakuta timu nyingine karibia kumaliza ligi imebakiza mchezo mmoja wakati kuna nyingine ina michezo mitatu au minne. Kwa hali kama hii ni raisi hata kupanga matokea matahalani kama zipo katika kupigania kutoshuka daraja au kupigania ubingwa! Kwa hali hiyo nazani ni wakati muafaka kwa TFF kuangalia upya namna inavyopanga ratiba ligi zake ili kurekebisha penye mapungufu ili kusaidia wachezaji wetu kuwa vyema kisaikolojia na kimashindano kwa muda mrefu vinginevyo tusitegemee miujiza. 
  Kwa upande wa vilabu vijitahidi kuepuka kuwa na viongozi wababaishaji bali wajitahidi kutafuta viongozi wazuri wenye historia ya soka zaidi wakiwa wasomi ni faida pia viongozi ambao wakatambua umuhimu wa wachezaji wa timu zao na kujali maslahi na afya zao. 
  Nipende kumalizia kwa kusema kwamba tusipozingatia ushauri huo niliotoa hapo juu ili tuweze kuendeleza soka letu tutakuwa na safari ndefu sana kuweza kufikia malengo tunayotarajia. Mathalani kushiriki mashindano ya Afrika au mashindano ya Dunia. Pia naomba jambo hili liwe ni changamoto kwa viongozi wapya wa TFF.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: JE LIGI YETU INAKIDHI VIWANGO! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top