• HABARI MPYA

  Alhamisi, Septemba 19, 2013

  MAKOCHA WAZAWA WAWAFUNIKA WAZUNGU LIGI KUU

  Na Mahmoud Zubeiry, Mbeya, IMEWEKWA SEPTEMBA 19, 2013 SAA 1:47 ASUBUHI
  MSIMU uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ulitawaliwa na makocha wa kigeni, Mholanzi Ernie Brandts akiipa ubingwa Yanga SC na Muingereza, Stewart Hall akiiweka nafasi ya pili Azam FC, lakini msimu huu mambo yanaelekea kubadilika.   
  Baada ya Raundi nne za awali za Ligi Kuu msimu huu, nafasi tatu za juu zinashikwa na timu ambazo zinafundishwa na makocha wazalendo na wote wachezaji wa zamani nchini.
  Simba SC  inayofundishwa na mshambuliaji wake nguli wa zamani, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 10, ikifuatiwa na JKT Ruvu, inayofundishwa na kipa wa zamani wa Yanga SC, Mbwana Makatta yenye pointi tisa.
  Kocha bora; Kocha Abdallah Kibaden akiwa na kiungo Amri Kiemba kushoto. Simba SC inaongoza Ligi Kuu baada ya Raundi nne 

  Nafasi ya tatu inashikiliwa na timu ya kiungo wa zamani wa Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa, Ruvu Shooting yenye pointi tisa pia.
  Ikumbukwe, Kibadeni ndiye kocha bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, taji ambalo alilipata kutokana kazi nzuri aliyoifanya akiwa Kagera Sugar kabla ya kununuliwa na Simba SC msimu huu, akirithi mikoba ya Mfaransa, Patrick Liweig.
  Brandts ndiye kocha wa kigeni aliye juu ya hadi sasa, akiiweka Yanga SC nafasi ya nne, akifuatiwa na Stewart aliyeiweika Azam nafasi ya tano.
  Mambo magumu; Kocha Stewart Hall ameshinda mechi mojta tu baada ya Raundi nne  

  Na hao ndiyo makocha pekee wa kigeni msimu huu katika Ligi Kuu- ambao pamoja na timu zao kusuasua lawama zinalekezwa kwa wachezaji wao kucheza bila kujituma.
  Bado katika ufungaji wa mabao, wachezaji wa kigeni wanaelekea kuwazidi maarifa wachezaji wazawa, kwani baada ya msimu uliopita Kipre Tchetche wa Azam raia wa Ivory Coast kutwaa kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu, msimu huu ameibuka mkali mwingine wa mabao kutoka Burundi, Amisi Tambwe.
  Mwanzo mbaya; Kocha Ernie Brandts kulia ameambulia pointi sita baada ya Raundi ya nne 

  Tambwe anaongoza kwa mabao yake manne aliyovuna kwenye mechi moja tu jana dhidi ya Mgambo JKT, akifuatiwa na wazawa, Jerry Tegete wa Yanga SC mwenye mabao matatu sawa na Haroun Chanongo wa Simba SC.
  Jonas Mkude wa Simba SC amefungana na Mrundi Didier Kavumbangu wa Yanga SC, Elias Maguri wa Ruvu Shooting, Bakari Kondo wa JKT Ruvu na Saad Kipanga wa Rhino Rangers, wote kila mmoja akiwa ana mabao mawili.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: MAKOCHA WAZAWA WAWAFUNIKA WAZUNGU LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top