• HABARI MPYA

    Monday, September 30, 2013

    NGASSA AJIFUA KIVYAKE COCO, AAANZA RASMI KUCHANGISHA FEDHA ZA KUPOZA MACHUNGU YA MILIONI 45 ZA SIMBA SC

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA SEPTEMBA 30, 2013 SAA 7:27 MCHANA
    MSHAMBULIAJI nyota Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa leo alifanya mazoezi mara mbili, baada ya kumaliza awamu ya pamoja na wenzake Yanga SC chini ya kocha wake, Mholanzi Ernie Brandts akaenda katika ufukwe wa Coco kufanya mazoezi binafasi. 
    Pamoja na hayo, Ngassa ameomba wanachama na wapenzi wa Yanga walioguswa na kitendo cha kulazimika kujilipia mwenyewe fedha za Simba SC, Sh. Milioni 45 kumchangia katika akaunti namba 01J2095037800 katika benki ya CRDB kwa jina la Mrisho Halfan Ngasa. 
    “Naomba wanachama na wapenzi wa Yanga SC walioguswa kunichangia fedha katika akaunti hiyo ili tuwe tumesaidiana kulipa deni hilo,”alisema.
    Ngassa akijifua Coco Beach




    Kuhusu kufanya mazoezi ya ziada, Ngassa alisema ni kwa sababu pia anakabiliwa na kazi ya ziada kuisaidia timu yake katika Ligi Kuu, hivi sasa ikiwa inazidiwa na wapinzani wa jadi, Simba SC kwa pointi tano kileleni.  
    Ngassa anadai Simba SC ilimuhadaa anasaini kucheza kwa mkopo kumalizia Mkataba wake wa Azam, lakini kumbe ni Mkataba mpya wa kuichezea klabu hiyo baada ya ule wa mkopo.
    Ngassa alifungiwa mechi sita za mashindano na TFF baada ya kubainika alisaini mikataba na timu mbili, Simba na Yanga SC. Pamoja na hayo, mshambuliaji huyo alitakiwa kurejesha fedha alizodaiwa kuchukua kusaini Mkataba wa Simba SC, Sh. Milioni 30 na fidia ya Sh. Milioni 15, ambazo alilipa Ijumaa jumla ya Sh. Milioni 45.
    Pamoja na hayo, Ngassa aliwashauri wachezaji wenzake kuwa makini wanapotaka kuingia Mikataba na klabu ili yasije yakawakuta kama yaliyomkuta yeye
    “Nawashauri wachezaji wenzangu kwamba, wanapoingia mikataba na klabu, wahakikishe wanakuwa na mawakili, ili wawasaidie kujua kilichomo ndani yake na wasaini mikataba ambayo wanaielewa,”. 
    Sakata la Ngassa linaanzia Agosti mwaka jana alipoukera uongozi wa iliyokuwa klabu yake, Azam FC kwa kwenda kubusu jezi ya Yanga SC baada ya kufunga bao la ushindi katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya AS Vita ya DRC, Uwanja wa Taifa.
    Baada ya kuiwezesha Azam, kutinga fainali ya michuano hiyo kwa ushindi wa 2-1, uongozi ulimuamuru kocha Stewart Hall asimpange mchezaji huyo kwenye fainali dhidi ya Yanga SC, lakini akakaidi na kumpanga na timu ikafungwa.
    Kilichofuatia, Azam FC iliamua kutangaza kumuuza mchezaji huyo kwa mkopo na Simba SC wakashinda tenda hiyo, wakati Stewart alifukuzwa na kwenda Sofapaka ya Kenya. Mserbia, Boris Bunjak aliajiriwa Azam, lakini hata kabla ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu uliopita akafukuzwa na Stewart akarejeshwa kazini.
    Ngassa aligoma kuuzwa bila idhini yake, lakini Simba SC wakaketi naye mezani na kufikia makubaliano, kabla ya kumtangaza rasmi kujiunga na klabu hiyo. Baadaye Simba SC ikasema ilimuongezea Mkataba mchezaji huyo na kumpa Sh. Milioni 30, wakati yeye mwenyewe anasema alipewa fedha hizo, ili akubali kucheza kwa mkopo.
    Yanga SC wakaamini maneno ya Ngassa na alipomaliza muda wake wa kuitumikia Simba SC kwa mkopo kumalizia Mkataba wake na Azam, akasaini kurejea Jangwani.
    Hata hivyo, TFF ikabaini mchezaji huyo alisaini Simba SC pia hivyo kumfungia mechi sita na kumtaka arejeshe Sh. Milioni 30 na fidia ya Sh. Milioni 15.     
    Ngassa alijiunga na Yanga SC kwa mara ya kwanza mwaka 2007 akitokea Kagera Sugar ya Bukoba na baada ya misimu mitatu akahamia Azam FC, ambako mwaka jana alivuruga na kuuzwa kwa mkopo Simba, kabla ya kurejea rasmi Jangwani, miezi mitatu iliyopita.
    Ngassa aliichezea Yanga SC kwa mara ya kwanza Jumamosi katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam akitoa pasi ya bao pekee la ushindi lililofungwa na Mganda, Hamisi Kiiza.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: NGASSA AJIFUA KIVYAKE COCO, AAANZA RASMI KUCHANGISHA FEDHA ZA KUPOZA MACHUNGU YA MILIONI 45 ZA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top