• HABARI MPYA

  Jumamosi, Septemba 28, 2013

  SIMBA SC: DHAIRA NI WETU HADI MSIMU UJAO, NA TUKO NAYE POA SANA

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA SEPTEMBA 28, 2013 SAA 4:19 ASUBUHI
  MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba kipa Abbel Dhaira aliingia Mkataba wa miaka miwili na Wekundu hao wa Msimbazi, hivyo ataendelea kuichezea klabu hiyo hadi msimu ujao.
  Pamoja na hayo, Hans Poppe amesema wanaishi vizuri na kipa huyo Mganda na hawana tatizo naye lolote, ingawa amesema katika Mkataba wao, mlinda mlango huyo anaweza kuondoka wakati wowote akipata timu nyingine.
  Miaka miwili; Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe akipeana mikono na kipa Abbel Dhaira baada ya kusain naye Mkataba, Januari mwaka huu. 

  “Katikati alikuwa ana mpango wa kurejea klabu yake ya Iceland, lakini ikashindikana kwa kuwa ile klabu ilisajili kipa mwingine. Na sisi tulijua huyu anaweza kuondoka wakati wowote, ndiyo maana tukamsajili Andrew Ntalla,”alisema.
  Alipoulizwa kuhusu mpango wa kurejeshwa Juma Kaseja, Poppe alisema; “Mimi nashangaa sana hizi kelele za Kaseja, Kaseja zinatoka wapi. Sisi hatuna tatizo na Kaseja, huyu ni mpenzi wa Simba na ni mwenzetu na hadi leo bado anakwenda mazoezini anasaidia kufundisha makipa pale,”.
  “Kaseja alimaliza Mkataba wake na tulipomuita kuzungumzia Mkataba mpya hakuja, ukafika wakati tukafunga usajili. Hatukumuacha sisi, sasa nisingependa kuendelea kuzungumzia habari za Kaseja,”alisema.
  Juu; Kulia Dhaira akizungumza na Hans Poppe kabla ya kusaini Mkataba, kulia Wakala wa Dhaira akihesabu dola za Kimarekani alizolipwa kipa huyo baada ya kusaini. Chini; Kulia Dhaira akisaini Mkataba na Katibu wa Simba SC, Evodius Mtawala na kulia akitia dole gumba.

  Poppe alisema kwa sasa Simba SC inafanya vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na uongozi unajipanga kuhakikisha timu inaendelea kuwa kileleni, hivyo usingependa kuvurugwa kwa mambo mengine yasiyo na tija kwa sasa.
  “Na ninaomba pia hata kwa viongozi wenzangu, Wajumbe wa Kamati ya Utendaji na Wajumbe wa Kamati ndogo ndogo na hata watu wa Sekretarieti yetu, kuwa makini na kauil zao na mipango yao yoyote, ambayo inaweza kuivuruga timu kwa sasa,”.
  “Tumesajili timu, tumeajiri makocha, tuwaache wafanye kazi, tuwape sapoti, badala ya kuanza kufikiria vitu vingine kwa sasa,”alisema.
  Simba SC iliyopokonywa ubingwa na wapinzani wao wa jadi, Yanga SC msmu uliopita, imerejea vizuri msimu huu ikiwa kileleni mwa Ligi Kuu baada ya mechi tano, kwa kujikusanyia pointi 11 na kesho itashuka tena dimbani kumenyana na JKT Ruvu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: SIMBA SC: DHAIRA NI WETU HADI MSIMU UJAO, NA TUKO NAYE POA SANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top