• HABARI MPYA

  Ijumaa, Septemba 27, 2013

  YANGA SC KUENDELEA KUMKOSA TELELA KESHO

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA SEPTEMBA 27, 2013 SAA 2:23 ASUBUHI
  YANGA SC itaendelea kumkosa kiungo wake hodari, Salum Abdul Telela katika mechi ya kesho ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kwa sababu bado majeruhi.
  Mfungaji huyo wa bao pekee la ushindi la Yanga SC katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC Agosti 17, mwaka huu, aliumia katika mchezo wa Ligi Kuu wa timu hiyo dhidi ya Prisons, Septemba 18, mwaka huu Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na hadi sasa ameshindwa kuamka mazoezini.
  Salum Telela bado majeruhi


  Wazi kumkosa Telela kwa sasa ni pigo kwa kocha wa Yanga SC, Mholanzi Ernie Brandts ambaye ametokea kumuamini sana katika siku za karibuni, kutokana na kucheza kwa uelewano mkubwa na Athumani Iddi ‘Chuji’.  
  Bila shaka sasa, katika mchezo wa kesho Brandts ataendelea kuwatumia kwa pamoja viungo Chuji na Frank Domayo katikati, wakati Haruna Niyonzima atacheza kushoto na Simon Msuva anaweza kuanzia benchi kumpisha Mrisho Ngassa kulia aliyemaliza adhabu yake ya mechi sita.
  Ngassa alifungiwa mechi na sita za mashindano baada ya kubainika alisaini mikataba na timu mbili, Simba na Yanga SC. Pamoja na hayo, mshambuliaji huyo ametakiwa kurejesha fedha za Simba SC, Sh. Milioni 30 na fidia ya Sh. Milioni 15.
  Tayari Yanga SC imekubali kumlipia deni hilo Ngassa kwa makubalino ya kumkata, ingawa haijulikani atakatwa katika Mkataba wa nyongeza au kwenye mishahara yake.    
  Yanga SC inamenyana na Ruvu kesho ikiwa imevuna pointi sita tu katika mechi tano ilizocheza hadi sasa, hivyo kuzidiwa pointi tano na Simba SC waliopo kileleni kwa sasa kwa pointi zao 11.
  Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) inaingia katika Raundi yake ya sita wikiendi hii kwa mechi kadhaa, mbali na  Yanga SC na Ruvu Shootings inayofundishwa na kiungo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Charles Boniface Mkwasa kesho, Jumapili, Simba SC itashuka dimbani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na JKT Ruvu, Rhino Rangers na Kagera Sugar Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora, Mbeya City na Coastal Union Sokoine, Mbeya, Mgambo JKT na JKT Oljoro Mkwakwani, Tanga na Ashanti United na Mtibwa Sugar, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: YANGA SC KUENDELEA KUMKOSA TELELA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top