• HABARI MPYA

  Jumamosi, Septemba 21, 2013

  SALUM TELELA KUWAKOSA AZAM KESHO TAIFA, KAZI YA WAJELAJELA HIYO

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA SEPTEMBA 21, 2013 SAA 4:35 ASUBUHI
  MFUNGAJI wa bao pekee la ushindi la Yanga SC katika mchezo wa Ngao ya Jamii ndhidi ya Azam FC Agosti 17, mwaka huu, Salum Abdul Telela ataukosa mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baina ya timu hizo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Telela aliumia katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu wa timu hiyo dhidi ya Prisons, Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na hadi leo ameshindwa kuamka mazoezini.
  Wazi kumkosa Telela katika mchezo huo wa kesho ni pigo kwa kocha wa Yanga SC, Mholanzi Ernie Brandts ambaye ametokea kumuamini sana katika siku za karibuni, kwani anacheza kwa uelewano mkubwa na Athumani Iddi ‘Chuji’.  
  Simon Msuva kulia akimpongeza Salum Telela baada ya kufunga bao pekee dhidi ya Azam, Agosti 17, mwaka huu. Kesho hatakuwepo.
  Bila shaka sasa, katika mchezo wa kesho Brandts anaweza kumuingiza ndani katikati ya Uwanja Haruna Niyonzima acheze pamoja na akina na Chuji na Frank Domayo na Nizar Khalfan na Simon Msuva wakacheza pembeni.
  Yanga SC wanamenyana na Azam FC kesho wakiwa wanalingana kwa pointi, sita kila timu baada ya kucheza mechi nne, hivyo kuzidiwa pointi nne na Simba SC waliopo kileleni kwa sasa kwa pointi zao 10.
  Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) inaingia katika Raundi yake ya tano leo kwa mechi kadhaa, huku vinara Simba wakiwakaribisha Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Uwanja wa Mkwakwani, Tanga utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mgambo Shooting Stars na Rhino Rangers ya Tabora. Mtibwa Sugar itakuwa mgeni wa Tanzania Prisons katika pambano litakalochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
  Nayo Kagera Sugar itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wake wa Kaitaba mjini Bukoba kuvaana na Ashanti United ya Dar es Salaam katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Jacob Adongo kutoka Mara.
  Ligi hiyo itakamilisha mzunguko wake wa tano kesho kwa mechi tatu moja ndiyo hiyo ya Azam na Yanga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku JKT Ruvu ikikwaruzana na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Azam Complex.
  Ruvu Shooting inayokamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi itakuwa mgeni wa Coastal Union katika mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: SALUM TELELA KUWAKOSA AZAM KESHO TAIFA, KAZI YA WAJELAJELA HIYO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top