• HABARI MPYA

    Wednesday, September 18, 2013

    UMEFIKA WAKATI YANGA WABADILIKE, WAJIFUNZE KUUKUBALI UKWELI

    IMEWEKWA SEPTEMBA 18, 2013 SAA 1:30 ASUBUHI
    UNAWEZA ukadhani kazi ngumu ni kubeba zege tu, au ukorokoroni, lakini hapana, hata kezi ya Uandishi wa Habari ni ngumu pia. Unaweza kufikiri kazi za hatari ni kurusha ndege hewani, kuongoza meli baharini au kwenda vitani kupigana- hapana, hata Uandishi wa Habari ni kazi ya hatari pia.
    Waandishi wa Habari tunakutana na mitihani mingi, inayomaanisha ugumu na kuhatarisha maisha yetu wakati mwingine, haswa unapoifanya kazi yako kwa uadilifu bila woga kama inavyopaswa.
    Tangu mwaka 1996 hadi leo, ni orodha ndefu ya matukio niliyowahi kukutana nayo yenye kumaanisha ugumu na kuhatarisha maisha yangu. Kuvamiwa na kundi la wapenzi wa klabu kubwa za Simba na Yanga na kutaka kupigwa, mara nyingi tu, kisa tu umeandika habari ambayo haijawapendezea, pasipo kuzingatia ukweli wa mambo.
    Kutiwa kashikashi na mikwara na viongozi wa klabu kubwa, makocha au wachezaji kisa umeandika habari ambayo hawajaipenda mara kibao tu kwangu. Kujengewa chuki na kufitinishwa, kusingizwa kashfa mbaya, watu kuingilia hadi maisha yako binafsi, zote ni changamoto ambazo nimekutana nazo katika tasniya hii ya Habari.
    Sitasahau, nimewahi kutekwa na askari mjini Kinshasa, DRC nikiwa natokea kwenye kambi ya klabu ya Azam Desemba mwaka jana kurejea hoteli nilipifikia- wakanipeleka ‘chakani’ na kunisulubu kabla ya kunipora fedha na simu na kunitelekeza. Namshukuru Mungu hawakunipiga risasi tu, wangefanya hivyo na kunitupa popote, na bado wasingejulikana. Mungu aliyenisimamia tangu natoka tumboni mwa mama yangu, Bi Fatuma Mnubi, Machi 3, saa 2:15 usiku mwaka 1978 katika hospitali ya Ocean Road, Dar es Salaam aliendelea kunisimamia siku hiyo pia kama ilivyo siku zote- na leo familia yangu, ndugu zangu na marafiki wa kweli bado wanafurahia na mimi.
    Nilizaliwa siku moja tu hiyo na kifo changu kitakuja siku moja tu ambayo siijui ni lini- naamini nipo duniani kwa ajili ya kutekeleza wajibu na majukumu yangu pasipo kuvunja Amri za Mungu wala sheria za nchi. Kama wewe unategemea pumzi ya Mungu kuishi kama mimi, usitarajie nitakuogopa au kukuabudu. Nitakuheshimu, hususan nawe ukinihesimu na kujiheshimu.
    Kwa sababu, tayari maandiko ya kitabu kitukufu ninachokiamini, Quran yamekwishaniambia; “Hapana Mola apasaye kuabuduiwa kwa haki, isipokuwa Mwenyezi Mungu mmoja”. Nani wewe? Shangaa sasa. Mali, utajiri, ufukara na umasikini, yote matokeo na yanawezekana kwa yoyote kabla hajakata pumzi yake ya mwisho. Wangapi waliitwa matajiri, leo ni mafukara. Wangapi waliitwa mafukara leo ni matajiri. Kila anayetafuta anatarajia kupata, na kabla hajafa hawezi kujihesabu amekosa. 
    Nataka niwahakikishie wapendwa wasomaji wangu- maelfu waliojenga imani na mimi kwamba, nitaendelea kuandika ukweli bila woga. Nitaendelea kutenda haki katika kazi. Nitajitahidi, kutoegemea upande wowote, bali kuzingatia misingi ya haki katika Uandishi bila kumuonea mtu.
    Namshukuru Mungu, mimi ni mwepesi wa kusamehe, kwa sababu najua siku ya mwisho nami nitahitaji msamaha wa Mola wangu. Nasamehe na kusahau, nasonga mbele na daima desturi inabaki kuwa ile ile, mtu yule yule. 
    Nipo Mbeya tangu Alhamisi wiki iliyopita kuripoti mechi za Ligi Kuu baina ya mabingwa watetezi, Yanga SC na wenyeji wa hapa Mbeya City na Prisons. Mchezo dhidi ya Mbeya City ulifanyika Jumamosi na timu hizo zikatoka sare ya 1-1 na leo, Yanga wanaingia katika mchezo wa pili dhidi ya Prisons.
    Baada ya mechi ya Jumamosi, nilifanya mahojiano na kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi na akatoa maoni yake juu ya mechi na kwa ujumla kuzungumzia mustakabali wa timu yake na Yanga pia katika msimu huu wa Ligi Kuu. 
    Habari yenyewe ni hii; KOCHA Mkuu wa timu ya Mbeya City ya hapa, Juma Mwambusi amesema kwamba kocha Mholanzi wa Yanga SC, Ernie Brandts ameshindwa kuiunganisha timu hiyo kuweza kucheza kitimu hadi sasa na hilo ndilo tatizo kubwa kwenye kikosi chake kwa sasa.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY mjini hapa, Mwambusi alisema mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wana wachezaji wazuri, lakini tatizo kubwa hawachezi kitimu, bali wanacheza kwa uwezo binafsi wa kila mchezaji.
    “Unajua tatizo ambalo nimeliona Yanga SC ni kwamba wana wachezaji wapya kwenye timu yao, sasa huyu mwalimu nadhani bado hajawaunganisha waweze kucheza timu, anatakiwa kuharakisha kuiunganisha timu icheze kitimu,”alisema.
    Hata hivyo, Mwambusi alisema bado ana matumaini sana na Yanga SC kwamba inaweza kutetea ubingwa wake, kwa kuwa ina wachezaji wazuri, bali tu Brandts anatakiwa kufanya kazi ya ziada kuiunganisha timu.
    Kuhusu malalamiko ya Yanga SC kwamba walitoa sare ya 1-1 na Mbeya City kwa sababu ya kucheza kwenye Uwanja mbovu wa Sokoine, Mwambusi alisema; “Si kweli, timu zote Tanzania zinafanya mazoezi kwenye viwanja vibovu pengine kuliko hata ule wa Sokoine,”.
    Mwambusi aliwashauri Yanga kuachana na visingizio wanapofanya vibaya, bali wafanyie kazi mapungufu yao ili kurekebisha makosa katika timu yao na ndiyo itawasaidia.
    Akiizungumzia timu yake ambayo pamoja na kucheza mechi tatu za awali za Ligi Kuu nyumbani imeambulia ushindi mmoja na sare mbili, Mwambusi alisema; “Si mbaya, kwa kuwa timu yangu ni mpya katika Ligi Kuu, na tumecheza zote ngumu, Yanga ni mabingwa na Kagera Sugar pia ni timu nzuri na hata Ruvu Shooting ni wazuri pia,”alisema.
    Mbeya imetoa sare na Yanga na Kagera na kuifunga Ruvu na jana imeondoka hapa kwenda Manungu, Morogoro kwa ajili ya mchezo wa kwanza ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar Jumatano.
    “Hatuna wasiwasi na mechi za ugenini, sisi hata kupanda kwetu Ligi Kuu tulicheza mechi nyingi sana ugenini. Na baada ya kupanda, pia tumecheza mechi nyingi za kuijipima nguvu ugenini, hivyo tunakwenda kuanza mechi za ugenini tukiwa na matumaini ya kufanya vizuri,”alisema Mwambusi, kipenzi cha wana Mbeya. Hii ndiyo habari yenyewe.
    Kilichofuata ni vitisho sasa, eti nimeikandia Yanga haikucheza kitimu. Kwanza hayakuwa maoni yangu, lakini hata kama name ningetoa maoni yangu, kuhusu mchezo ule wa Jumamosi, yasingepishana sana ya Mwambusi.
    Yanga walikuwa wanapiga tu mipira mbele, bila malengo na ilikuwa vigumu hata kuelewa wanacheza mfumo gani, zaidi tu ya kujua walicheza na washambuliaji watatu, viungo watatu na mabeki wanne, yaani 4-3-3.
    Kweli Uwanja ni mbaya, lakini bado Yanga wangeweza kucheza mipira mirefu ya pasi chache ili kufika langoni kwa wapinzani haraka, badala yake mipira ilikuwa inapigwa mbele kuelekea lango la Mbeya ili washambuliaji wapambane. Walikuwa wana kazi ngumu na mara nyingi waliishia kugongana wenyewe kwa wenyewe.
    Mchezo ulibadilika baada ya kuingia Jerry Tegete ambaye alikuwa anaombea mipira pembeni na kutengenenza mashambulizi yenye kuonekana, hadi wakafanikiwa kupata bao la kusawazisha. Jerry alikaribia kufunga mara mbili kwa mashuti, ambayo yalitoka nje sentimita chache. 
    Siku zote nawaambia Yanga lazima wabadilike. Lazima wakubali mapungufu yao, ili wayafanyie kazi.  Yanga haiwezi kuwa nzuri (kama mbaya) kwa kumtisha Mwandishi, bali kocha kufanyia kazi mapungufu.
    Dunia nzima kinachofuata baada ya mchezo ni tathmini, kwa nini timu ilishinda, kwa nini ilishindwa, kwa nini timu ilicheza vizuri, kwa nini timu ilicheza ovyo. Yanga wamekuwa wakisifiwa sana wanapofanya vizuri, ajabu hata wanapofanya vibaya wanataka wasifiwe pia. Kitu kimoja nataka niwaambie Yanga wote, ufike wakati wawe wanaukubali ukweli juu ya mapungufu yao- kama ambavyo huwa wanafurahia wanaposifiwa kwa mazuri yao. Nimefika.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: UMEFIKA WAKATI YANGA WABADILIKE, WAJIFUNZE KUUKUBALI UKWELI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top