• HABARI MPYA

    Tuesday, September 24, 2013

    UBINGWA COPA COCA COLA NI SALAMU KWA WATEUZI WA TIMU ZA VIJANA ZA TAIFA

    IMEWEKWA SEPTEMBA 24, 2013 SAA 6:35 USIKU
    JUMAPILI ya tarehe 15 Septemba, mwaka huu, mitaa ya manispaa ya Zanzibar ilikuwa imehanikiza kwa hoihoi na furaha kubwa baada ya timu ya vijana walio chini ya miaka 15 (U-15), ya mkoa wa Mjini Magharibi, kurudi kutoka Dar es Salaam ambako ilitwaa ubingwa wa mashindano ya Copa Coca Cola mwaka 2013.
    Timu hiyo ilionesha uwezo mkubwa katika mashindano hayo tangu hatua ya makundi hapa Zanzibar na baadae kule Kibaha Pwani, hadi kuvuka robo, nusu na hatimaye kutinga fainali.

    Licha ya kupambana na timu ngumu ya mkoa wa Ilala kisoka, vijana hao waliendelea kucheza kwa kujamini na kuibuka nma ushindi wa bao 1-0, na hivyo kutawazwa ubingwa ulioambatana na zawadi nono ya shilingi milioni nane, medali za dhahabu na kikombe.
    Bila shaka, wapenda soka wa Zanzibar na wananchi wengine kwa jumla, wana haki ya kushangiria na kujivunia hatua hiyo kubwa katika soka la Zanzibar, ambapo timu yake kubwa ya taifa, imeshindwa kuleta mataji ya ukanda wa Afrika Mashariki tangu ilipofanya hivyo mnwaka 1995.
    Lakini kwa upande mwengine, sisi wadau wa michezo hasa mpira wa miguu, tunakiona kitendo kilichofanywa na vijana hao ni salamu tosha kwa mamlaka zenye dhamana ya kuteua na kusimamia timu za taifa za vijana za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serengeti Boys (U-17) na Ngorongoro Heroes (U-20).
    Tunaamini kuwa ubingwa huo umepeleka ujumbe kwa mamlaka hizo ambazo kimsingi zimekabidhiwa jukumu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
    Kwa miaka mingi sasa, wasimamizi hao wa timu za taifa za vijana, wamekuwa wakishindwa kuviona vipaji vilivyosheheni hapa Zanzibar, na hivyo kuzifanya timu hizo kukosa sura halisi ya muungano.
    Hata pale wanapokuwemo wachezaji kutika Zanzibar, huwa wachache na mara nyingi huchaguliwa kwa hatua ya kwanza tu na baadae kuenguliwa wakati wa mchujo.
    Aidha, kama atakuwemo walau mchezaji mmoja, si aghalabu kusikia amepangwa katika mechi za kimataifa ambazo timu hizo hushiriki.
    Kwa hivyo, kama walikuwa wakifanya kwa bahati mbaya, au kwa kuwa hawakupata muda wa kufika Zanzibar kwa ajili ya kusaka vipaji hivyo, kitendo cha timu yetu ya Mjini
    Magharibi kiwe fundisho kwa makocha na maofisa wa TFF kwamba Zanzibar nako viko vipaji, na pia nasi tuna haki ya kupata nafasi yetu katika timu hizo.
    Ninaamini hakuna atakayekuja na dhana kwamba timu yetu imefanikiwa kutwaa ubingwa huo kwa kubahatisha, kwani kila aliyewaona ameamini kwamba vijana wanaujua mpira kweli kweli.
    Ni ukweli usiofichika kuwa, Zanzibar inaongoza kwa kuwa na mfumo mzuri wa kuendeleza timu za watoto na vijana kuliko nyengine wote katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
    Ligi za vijana za ngazi za 'junior, juvenile na central', Unguja na Pemba, zimeiwezesha Zanzibar kuwa na rasilimali kubwa na nzuri ya vipaji vinavyozinufaisha klabu mbalimbali za ndani na nje ya nchi yetu.
    Utaratibu huo ulioasisiwa na marehemu Maalim Hija Saleh, ndio kama ule unaotumika katika nchi za ng'ambo kama za Ulaya, Marekani na nchi za Afrika zilizopiga hatua kubwa kisoka.
    Maendeleo ya soka la vijana yanayoendelea kupatikana hapa nchini, bila shaka ni matunda ya jitihada za makocha wa madaraja hao waliojikita kuendeleza msingi iliyotandikwa na muasisi huo na wengine, kama vile marehemu Khatib Mzibindo na marehemu Maalim Rajab Mzee.
    Aidha, ushindi wa timu ya mkoa wa Mjini Magharibi, ni salamu kwa waandaaji wa mchakato wa kupata vipaji 'unaoitwa' wa Tanzania, Airtel Rising Stars, ambao wameifumbia macho Zanzibar na baadae kuunda timu iliyokwenda Nigeria kushiriki mashindano ya vijana. Eti katika mashindano hayo yanayoshirikisha vijana walio chini ya miaka 17, timu hiyo (ya TFF na Airtel), imeelzewa kuwa inaiwakilisha Tanzania ikipeperusha bendera ya Jamhuri ya Muungano.
    Hili pia liliwahi kulalamikiwa na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kupitia Katibu wake mkuu, ambaye alieleza, kuwa kimsingi mchakato wa kutafuta vipaji uliodhaminiwa na kampuni ya simu ya Airtel ulipaswa pia kuishirikisha Zanzibar.
    Hilo halikufanyika kwa vitendo wala angalau kuiandikia ZFA nayo ichague vijana wa kujiunga na timu hiyo, ambayo sasa inashiriki kwa jina la Tanzania mashindano yanayoendelea huko Nigeria.
    Katika mechi yake ya kwanza dhidi ya timu ya taifa ya Ghana, kikosi hicho kilikula mweleka wa mabao 2-1.
    Hatusemi kwamba kama wangekuwemo wachezaji wa Zanzibar kwenye kikosi hicho timu isingefungwa, lakini pengine kungekuwa na timu imara zaidi kwani Zanzibar pia inavyo vipaji vinavyoweza kuhimili vishindo hata vya wachezaji wa kimataifa.   
    Inashangaza kwamba kila mara ZFA inapokerwa na matendo ya TFF na kuamua kusema hadharani, TFF kupitia baraza la Michezo la Taifa (BMT), hujitoa kimasomaso kwa kuja na mazungumzo ya pamoja yanayoishia kwa pande hizo kusaini mkataba wa maelewano (Memorandum of Understanding-M.O.U).
    Lakini mikataba hiyo huwa mfano wa pipi ambayo ZFA hulishwa ili inyamaze, na utekelezaji wa mikataba hiyo hufanywa katika hatua za awali tu na baadae kusahaulika makabatini na mambo kurudi kama yalivyokuwa kabla.
    Hili la Zanzibar kutoshirikishwa katika mambo yanayopaswa kuwa ya kimuungano na mengine kadha wa kadha, ndiyo yanayochafua uhusiano wa TFF na ZFA ambao yaonekana wazi kuwa, bado upande mmoja haujawa na nia njema ya kuuimarisha.
    Mashindano haya ya kimataifa ya Airtel Rising Stars yanafanyika kwa mara ya pili, ambapo kwanza yalifanyika nchini Nairobi lengo lake likiwa ni kuzalisha vipaji vingi vya timu za taifa barani Afrika.
    Jambo la kusikitisha, ni kwamba mara zote hizo Zanzibar imewekwa kando bila kudhukuriwa.
    Kama bado TFF na makocha wa timu za taifa za vijana za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hawajaviona vipaji vinavyong’ara Zanzibar, kitendo cha timu ya mkoa wa Mjini Magharibi kubeba ubingwa wa Copa Coca Cola Tanzania mwaka huu, kitoshe kuwazindua iwapo  wametusahau, (sipendi nitumie neno wametudharau).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: UBINGWA COPA COCA COLA NI SALAMU KWA WATEUZI WA TIMU ZA VIJANA ZA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top