• HABARI MPYA

  Jumatano, Septemba 18, 2013

  SIMBA YAUNGURUMA TAIFA, YANGA NA AZAM TAABAN MSIMU HUU

  Na Prince Akbar, IMEWEKWA SEPTEMBA 18, 2013 SAA 12:31 JIONI
  SIMBA SC imeonyesha ni tishio msimu huu baada tya kushinda mabao 6-0 dhidi ya Mgambo JKT katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku mshambuliaji Mrundi, Amisi Tambwe akifunga mabao manne peke yake.
  Yanga mbona mmenuna? Amisi Tambwe akishangilia moja ya mabao yake Taifa leo. Wengine ni Betram Mombeki na Issa Rashid 'Baba Ubaya'. 

  Mabao mengine ya Simba leo yamefungwa na kinda mzalendo, Haroun Athumani Chanongo, huku wapinzani wao wa jadi, Yanga SC wakilazimishwa sare ya 1-1 na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya. 
  Matokeo hayo yanaipandisha kileleni Simba SC baada ya kufikisha pointi 10 kutokana na mechi nne, huku Yanga na Azam zinaendelea kusuasua kwa pointi zao sita kila mmoja baada ya mechi nne. 
  Tambwe aliyetokea Vital’O ya Burundi alifunga mabao manne leo katika dakika za nne, 41, 44 na 76 kwa penalti, baada ya beki Bashiru Chanache wa Mgambo kuunawa mpira kwenye eneo la hatari, wakati Haroun Chanongo alifunga mawili pia dakika ya 32 na 64.
  Kwa ujumla Simba SC iliwapa raha mashabiki wake leo kwa soka safi na ushindi mnono.
  Simba SC; Abbel Dhaira, Miraj Adam/William Lucian ‘Gallas’, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Kaze Gilbert, Joseph Owino, Jonas Mkude, Amri Kimeba, Henry Joseph/Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Betram Mombeki, Amisi Tambwe na Haroun Chanongo. 
  Mgambo JKT; Kulwa Manzi/Tony Kavishe dk46, Francis Anyosisye, Salum Mlima, Bakari Mtama, Novat Lufunga, Salum Kipaga, Nassor Gumbo, Peter Mwalyanzi, Mohamed Neto, Fully Maganga na Salum Aziz Gilla.
  Didier Kavumbangu kushoto na Simon Msuva kulia, wakimpongeza Jerry Tegete baada ya kuifungia Yanga SC bao la kuongoza kipindi cha kwanza

  Mbeya; Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Jerry Tegete alitangulia kuifungia Yanga SC dakika ya 37 akiunganisha krosi maridadi ya winga Simon Msuva kabla ya Michael Peter kuisawazishia Prisons dakika ya 77 akiunganisha krosi ya Omega Seme anayecheza kwa mkopo kutoka Jangwani.  
  Yanga SC ilicheza vizuri zaidi kipindi cha kwanza na kupoteza nafasi mbili nzuri za kufunga mabao zaidi dakika ya tatu, Didier Kavumbangu alipowababatiza mabeki shuti kali baada ya kupokea krosi ya Simon Msuva na Jerry Tegete dakika ya saba aliwatoka vizuri mabeki wa Prisons, lakini akapiga nje.
  Kipindi cha pili, Prisons walibadilika nao kuanza kushambulia langoni mwa Yanga na kwa ujumla katika ngwe hiyo timu zilishambuliana kwa zamu na mchezo ulikuwa mkali baada ya matokeo kuwa 1-1.
  Yanga walionekana kupigana zaidi kusaka bao la ushindi, lakini Prisons walisimama imara kuzuia na kushambulia pia na dakika ya 87 almanusra Prisons wapate bao la pili baada ya Ibrahim Isihaka kupiga kichwa juu kidogo ya lango kufuatia krosi ya Julius Kwanga.    
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva/Nizar Khalfan, Salim Telela/Frank Domayo, Didier Kavumbangu, Jerry Tegete/Said Bahanuzi, Hussein Javu na Haruna Niyonzima.
  Prisons; Beno David, Salum Kimenya, Laurian Mpalile, Jumanne Elfadhil, Nurdin Issa, Jimmy Shoji/Hamisi Rataon, Freddy Chudu, Ibrahim Isihaka, Six Ally/Julius Kwanga, Jeremiah Juma/Omega Seme na Lugano Mwagomba.    
  Chamazi; Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, Kipre Tchetche alitangulia kuifungia Azam dakika ya 21, kabla ya Anthony Matangalu kuisawazishia Ashanti United dakika ya 79.
  Katika mchezo huo, Azam ilimalioza pungufu baada ya Aggrey Morris kutolewa nje kwa kadi nyekundu. 
  Uwanja wa Mabatini, Mlandizi Ruvu Shooting iliichapa 1-0 JKT Ruvu, bao pekee la Cossmas lewis dakika ya 36.
  Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, wenyeji Kagera Sugar waliifunga JKT Oljoro 2-1.  Mabao ya Kagera yalifungwa na Godfrey Wambura dakika ya 25 na Maregesi Mwangwa dakika ya 90, wakati la Oljoro lilifungwa na Shaibu Nayopa dakika ya 35.
  Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro, wenyeji Mtibwa Sugar walilazimishwa sare ya bila kufungana na Mbeya City, wakati Coastal Union ililazimishwa sare ya 1-1 na Rhino Rangers ya Tabora.
  Mkenya Jerry Santo aliinusuru Coastal kuzama kwa bao la penalti dakika ya 81, kufuatia Salum Majjid kutangulia kuifungia Rhino dakika ya 26.       
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: SIMBA YAUNGURUMA TAIFA, YANGA NA AZAM TAABAN MSIMU HUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top